Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro awapa siku moja wenyeviti wa vitongoji Hai kufafanua wanataka kufanya kazi za serikali ama la
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Leonidas Gama akizungumza na wanahabari (pichani chini ) kuhusiana na maandalizi ya Sensa katika mkoa huo.
Na Dixon Busagaga wa
Globu ya Jamii, Hai.
WENYEVITI
wa vitongoji 116 katika wilaya ya Hai,wametishia kutoshiriki zoezi la
sensa ya watu na makazi inayotarajia kufanyika usiku wa kuamkia Agosti
26 nchini kote kwa madai wanaidai halmashauri hiyo kiasi cha Sh Mil
280.8 ikiwa ni fedha zao za posho kuanzia mwaka 2009 hadi sasa.
Mkuu
wa mkoa huo,Leonidas Gama, aliyasema hayo katika mkutano wake na
wanahabari akizungumzia maandalizi ya zoezi hilo ambalo alisema
limekamilika kwa asilimia kubwa .
Pamoja
na kuwepo kwa tishio hilo,mkuu wa mkoa alisema wenyeviti hao wamepewa
muda wa siku moja kufafanua msimamo wao iwapo wanataka kuendelea kufanya
kazi za serikali ama la kutokana na kwamba madai yao
hayahusiani na shughuli ya sensa.
“Kwa
sasa tunachangamoto mbili kubwa, hii ya kikundi cha waislamu na
hawa wenyeviti wa vitongoji wilayani Hai….nimeongea na viongozi wa
wilaya yao nikawataka kama msimamo wao ni kutoshiriki zoezi hili, basi
waandike barua ya kujiondoa katika nafasi zao za uenyekiti”alisema Gama..
Aidha
Gama amesema kwa mujibu uongozi wa halmashauri ya wilaya, madai ya
wenyeviti hao hayakulipwa mapema kutokana na kukosekana kwa fedha katika
bajeti lakini kwa mwaka huu ni miongoni mwa madai yatakayopewa
kipaumbele katika malipo.
Kuhusu
kikundi cha waislamu wanaopinga zoezi hilo kilichopo katika wilaya za
Same,Mwanga,Moshi mjini na Hai ,Gama alisema tayari jitihada zimefanyika
kuwashirikisha viongozi wa madhehebu ya dini ili kuwaelimisha waumini
wao kushiriki zoezi hilo.
Alisema
mkoa una makarani wa sensa 4937 ambao wamegawanyika katika makundi
mawili moja likiwa na makarani 2156 kwa ajili ya kujaza dodoso refu na
2279 kwa ajili ya Dodoso fupi huku makarani wa akiba wakiwa 153 na
wasimamizi 349.
Akizungumzia
vituo kwa ajili ya zoezi hilo alisema kuna vituo 3357 vilivyogawanywa
katika makundi mawili ya Dodoso fupi vilivyopo 2279 na dodoso refu vipo
1078 na kwamba Agosti 23 imetengwa kwa ajili ya kutambua maeneo ya kazi
ambapo wataongozwa na wenyeji wao ambao ni wenyeviti wa vitongoji,vijiji
na mitaa.
Mkuu
wa mkoa aliwataka wananchi kutunza kumbukumbu za taarifa za
watu watakaolala katika nyumba zao kwa usiku wa kuamkia Agosti 26 na
kwamba zoezi hilo litafanywa kwa siku saba na wasihofu iwapo makarani
hawatafika tarehe 26 bali wasubiri hadi watakapofika kwa takribani siku saba
Post a Comment