Kiongozi wa Uamsho ashtakiwa, ulinzi mkali watanda, apelekwa rumande
KIONGOZI wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kislamu, Sheikh
Faridi Hadi Ahmed, na wenzake sita jana walipandishwa katika Mahakama ya
Wilaya Manakwerekwe visiwani hapa, wakikabiliawa na tuhuma za kufanya
uchochezi na kusababisha vurugu.
Mwendesha Mashtaka wa Serikali kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka
(DPP), Maulid Ame, aliwataja viongozi wengine kuwa ni Sheikh Mselem Ali
Mselem (Kwamtipua), Sheikh Musa Juma Issa (Makadara) na Sheikh Azani
Khalid Hamdani (Mfenesini).
Wengine ni Sheikh Suleiman Juma Suleiman (Makadara), Sheikh Khamis Ali
Suleiman (Mwanakwerekwe) na Hasan Bakari Suleiman mkazi wa Tomondo.
Wote kwa pamoja walidaiwa kuwa Agosti 17, mwaka huu, majira ya saa 11
jioni huko kiwanja cha Magogoni Msumbiji katika Wilaya ya Magharibi
Unguja wakiwa wahadhiri kutoka Jumuiya ya Uamsho na mihadhara ya
Kiislamu walitoa matamko ya uchochezi.
Kwamba maneno hayo yaliashiria uvunjifu wa amani na kusababisha fujo
na maafa mbalimbali na mtafaruku kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
(SMZ).
Mwendesha mashtaka huyo alisema kitendo hicho kilikwenda kinyume na
kifungu cha 45 (1) (a) (b) sheria na 6 ya mwaka 2004 sheria za
Zanzibar.
Hata hivyo wakili wa washtakiwa hao, Abdalla Juma, alisema kuwa makosa
ya wateja wake si miongoni mwa yale yanayopaswa kunyimwa dhamana, hivyo
aliomba mahakama kuwapatia dhamana kwa masharti mepesi.
Alisema kuwa kitendo cha kutaka barua ya sheha na wadhamini ambao ni
watumishi wa serikali kwa ajili ya dhamana ni kuwakwamisha wateja wake
kwani watu hao ni vigumu kuwapata.
Hata hivyo, mwendesha mashtaka wa serikali hakuwa na pingamizi na ombi
la dhamana hiyo na kusema anaiachia mahakama itoe uamuzi.
Naye hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Ame Msaraka Pinja, alisema wa
kuwa dhamana ni haki yao haitakuwa busara kwa mahakama yake kutoa
uamuzi wa haraka wala kuchelewesha dhamana za washtakiwa hao.
Aliiahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 25 mwaka huu ambapo itakuja
kusikizwa uamuzi wa dhamana zao, na hivyo watuhumiwa wote walirudishwa
rumande.
Hata hivyo, wakati wote kesi hiyo ikiendelea, ulinzi mkali wa polisi
ulitanda kuzunguka mahakama hiyo, huku watu wakizuiwa kuingia ndani.
Sheikh Faridi na wenzake walifikishwa mahakamani hapo majira ya saa
5:00 asubuhi chini ya ulinzi mkali wa polisi wenye magari saba aina ya
Landrover.
Dk. Slaa amkaba JK
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk.
Willibrod Slaa, amemtaka Rais Jakaya Kikwete kuvunja ukimya wake na
kuchukua hatua sahihi kumaliza chokochoko za udini zinazolielemea taifa.
Dk. Slaa alisema kuwa yanayoendelea ndani ya nchi yametengenezwa na
watawala wenyewa, hivyo amemtaka Rais Kikwete kujifunza kwa Rais
mstaafu Alli Hassan Mwinyi.
Alisema kuwa kiongozi huyo aliweza kuchukua hatua za kitaasisi
kumaliza mizozo iliyoanzishwa na makundi ya Wakristo wenye imani kali na
Waislamu miaka ya 90, ambayo yalikuwa yakishambuliana kwa mahubiri na
hotuba kalikali.
Akihutubia mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya
Bugarama, Kahama juzi, Dk. Slaa alisema kuwa hatua hiyo ni moja ya vitu
vinavyomfanya Rais Mwinyi akumbukwe na Watanzania.
“Hali ya sasa hivi ni tofauti kwani matatizo yanayoendelea nchini
yamezalishwa na viongozi wenyewe, wanaotafuta visingizio vya kuvuruga
nchi baada ya kushindwa kuongoza na kuweka fursa za wananchi kujipatia
maendeleo,” alisema.
Dk. Slaa aliongeza kuwa yanayoendelea sasa ni kama vile nchi haina
kiongozi, haina serikali na hakuna chama kinachoongoza serikali, kwani
wote wanaowajibika kukemea na kuchukua hatua sahihi kumaliza tatizo
wamekaa kimya.
Alisema kuwa Watanzania wote wema, bila kujali itikadi zao za dini
wala siasa, wanaoipenda nchi yao, wanapaswa kupaza sauti zao kabla nchi
haijatumbukia katika matatizo.
Kwamba hali hii imetokana na watawala walioko madarakani kuwatumia
viongozi wa dini kuwagawanya Watanzania ili wasiwe na muda wa kuhoji
masuala ya msingi.
“Sasa tunamtaka Kikwete kama nchi imemshinda atangaze kuwa ameshindwa
ili asaidiwe. Na CCM yao hawana tena uwezo wa kuhubiri amani, maana
nilishawaambia amani haihubiriwi majukwaani,” alisema.
TANZANIA DAIMA
Post a Comment