MAGUFULI APELEKA BOMOABOMOA MOROCCO

WAZIRI wa Ujenzi, Dk John Magufuli 


WAZIRI wa Ujenzi, Dk John Magufuli ameitaka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), kuanza kuvunja nyumba zilizopo ndani ya hifadhi ya Barabara ya Mwenge hadi Morocco, Dar es Salaam ili kupisha ujenzi wa barabara nne za lami.

Pia, ameitaka Tanroads kuacha kigugumizi katika ujenzi wa barabara za juu jijini Dar es Salaam (flyovers) kwa kuwa fedha kwa ajili ya kazi hiyo zipo.Waziri Magufuli alitoa wito huo Dar es Salaam jana, alipokuwa akizindua bodi mpya ya Mfuko wa Barabara na Bodi ya Tanroads.

“Barabara ya Mwenge- Morocco nyumba zinatakiwa kubomolewa. Zibomolewe haraka ili kupisha ujenzi. Nasema Tanroads acheni kigugumizi kwenye masuala haya,” alisisitiza Dk Magufuli.

Ingawa hakuzianisha nyumba zilizotakiwa kubomolewa katika barabara hiyo, sehemu kubwa ina nyumba za thamani kubwa hasa ghorofa jambo ambalo linatarajiwa kuwaweka katika wakati mgumu wamiliki wake.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanroads, Patrick Mfugale alisema: “Nyumba zitakazobomolewa siyo nyingi. Ni zile zilizojengwa ndani ya mita 30 ya hifadhi ya barabara. Kinachotuchelewesha ni kuondolewa kwa nyaya za umeme pamoja na mfumo mkubwa wa maji ili tuweze kuanza ujenzi.”

Waziri Magufuli alisema fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo zipo na hata za kuwalipa wamiliki wa nyumba hizo zipo, hivyo akasisitiza kuwa kazi ya kuzibomoa inapaswa kuanza mara moja.

“Wanaostahili kulipwa fidia walipwe na ambao hawastahili waondoke. Suala la kwamba mko kwenye mchakato life na libaki kuwa neno la wanasiasa tu,” alisema Magufuli.

Bajeti ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2012/13, imeonyesha kuwa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 4.3, ujenzi wake unafadhiliwa na Serikali ya Japan.
Kuhusu ujenzi wa barabara za juu, Waziri Magufuli alisema ni jambo linalowezekana na halihitaji kufanyiwa mchakato wowote.

Alisema ni muhimu bodi hiyo mpya ikasimamia ujenzi wa barabara hizo ili kupunguza msongamano wa magari Dar es Salaam.

“Tengenezeni ‘flyovers’ nyingi nyingi, ni kazi ndogo lakini inashangaza kwa nini Tanroads inakuwa na kigugumizi,” alisema Magufuli na kuongeza:
“Wahandisi wa Tanroads fanyeni hivyo, mbona kule Kenya mambo yamefanyika bila tatizo? Acheni kigugumizi na siasa mfanye kazi.”

Magari ya Serikali
Waziri Magufuli pia alizungumzia mchakato wa kukamata magari ya Serikali yanayotumika vibaya na kuzitaja Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi) kuwa vinara wa tatizo hilo.

Dk Magufuli alisema tangu kuanza kwa operesheni hiyo, magari 974 yalikamatwa baada ya watumishi wake kuyageuza kuwa ya kiraia kwa kubandika namba binafsi.

Alisema pamoja na kukamata kiasi hicho, bado kuna magari 746 ya Serikali ambayo hayajasajiliwa na mengi yako Wizara ya Sayansi, Mawasiliano na Teknolojia pamoja na Tamisemi.

“Hawa ndiyo wanaoongoza kwa magari yao kutokusajiliwa kiserikali. Tutaendelea na mpango huo hadi magari yote yatakapokamatwa na kusajiliwa.”
Awali, operesheni hiyo ilionekana kusuasua tangu waziri huyo alipotangaza kuanza kwake kwa washirikisha polisi.


Hivi karibuni, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, John Ndunguru alivieleza vyombo vya habari kwamba Serikali iliweka utaratibu unaozuia matumizi ya namba za kiraia kwenye magari yake isipokuwa kwa kibali maalumu.
Alisema hali ya kuzuia huko kuliibuka baada ya kubainika kwamba kupitia namba hizo, magari ya umma yamekuwa yakitumika vibaya na baadhi kupotea.

MWANANCHI

No comments

Powered by Blogger.