Serikali kubanwa kashfa ya mabilioni
MBUNGE wa Ubungo (Chadema), John Mnyika amesema
ataongeza nguvu ya wabunge wanaotaka Serikali kuchukua hatua za haraka
kuwataja baadhi ya viongozi na wafanyabiashara wanaodaiwa kuficha nje
mabilioni ya fedha yanayosadikiwa kupatikana kwa njia isiyo sahihi.
Mnyika aliyasema hayo jana katika mkutano wa
hadhara uliofanyika katika Kata ya Saranga Mbezi jijini Dar es Salaam,
ambapo tayari Mbunge wa jimbo la Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe
alishatoa kauli kama hiyo ya kuitaka Serikali kuchukua hatua za haraka
kuwataja watu hao kabla ya vikao vya Bunge vya mwezi Aprili.
Akizungumza katika mkutano huo, Mnyika alisema
Serikali itegemee kupata upinzani mkubwa katika vikao vya Bunge Aprili
mwakani kama haita jisafisha kwa kuwataja watu hao na kuwachukulia
hatua.
“Nia yetu ni kuhakikisha watu wote wanaodaiwa kuwa
na akaunti mbalimbali nje ya nchi Serikali inawachukulia hatua pamoja
na kuwataja kwa majina ili watanzania waeze kuwafahamu watu wanao
wasababisha waishi katika hali ngumu,” alisema Mnyika na kuongeza:
“Nijambo la kushangaza kusikia kwamba Serikali ya
CCM inasema wapinzani ndiyo tuwataje lakini suala hilo lipo wazi kwani
kama itakumbukwa, Septemba 15 mwaka 2010 katika viwanja vya Mwembeyanga
tulitaja majina hayo na wengine kwa sasa ndio Viongozi wakubwa ndani ya
Bunge.”
Mnyika alibainisha kwamba Chadema itaendelea na
kasi yake ile ile hadi kuhakikisha viongozi wote wanaodaiwa kuwa na
akaunti nje ya nchi wanajulikana wazi ili Watanzania wawafahamu watu
wanao tumia kodi zao kwa masilahi yao binafsi.
Katika hatua nyingine, Mnyika alisema suala la
usafiri katika jiji la Dar es Salaam bado ni tatizo kwani hata kuwapo
kwa usafiri wa treni sio suluhisho kutokana na Serikali kupata hasara ya
Sh10 milioni kila baada ya siku tano kutokana na undeshaji wa usafiri
huo.
Alisema kutokana na maandalizi duni Serikali
inapata hasara ya Sh10 milioni jambo ambalo ni hatari kwani itafikia
hatua usafiri huo wa Treni utasimama.
“Ni vyema Serikali ikajipanga vizuri kwani kwa
sasa wakazi wengi wa Jiji la Dar es Salaam wanafurahia usafiri wa Treni
lakini ipo siku usafiri huo utasimama kutokana na kuendeshwa kwa hasara
kubwa,” alisema na kuongeza;
“Jambo hilo linatokana na kuwa na miundombinu mibovu na maandalizi duni yaliyofanywa na mawaziri wa uchukuzi waliopita.”
CHANZO: MWANANCHI
Post a Comment