MCHAKATO WA KATIBA:Mtikila aibua mapya

Mchungaji Christopher Mtikila 

ATAKA RAIS AAPISHWE BAADA YA SIKU 90,AONDOLEWE KINGA,WANAHABARI WALIA NA SHERIA KANDAMIZI
 
MAKUNDI maalumu jana yaliendelea kutoa maoni yao kwenye mchakato wa Katiba Mpya, huku DP kikipendekeza Rais aapishwe baada ya siku 90 tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu.
Mbali na maoni hayo yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Mchungaji Christopher Mtikila, makundi mengine; wakulima, wafugaji, wanahabari na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) nayo yalijitokeza kutoa moyoni.
Mtikila alisema kipindi hicho cha siku 90 kitatoa fursa kwa watu wanaotaka kuwasilisha pingamizi dhidi ya ushindi wa Rais mteule kufanya hivyo, kabla ya kuapishwa.
Alisema pingamizi linaweza kufanyiwa kazi kwa kipindi hicho cha miezi mitatu ili kuhakikisha kuwa taifa linapata kiongozi halali mwenye ridhaa ya wananchi.
“Pia tunataka kinga ya Rais ikome pale anapomaliza muda wake wa uongozi, kama alifanya makosa yoyote ya jinai aweze kushtakiwa ili kujenga nidhamu ya uongozi katika ofisi ya umma. Utaratibu wa kumwondoa madarakani uimarishwe asisubiriwe hadi amalize muda wake wa uongozi.”
Alisema kuwa Katiba ya nchi inapaswa kuwa mali ya wananchi wenyewe ili watawala wasijihusishe katika kuwaundia wananchi Katiba kama ilivyo kwa mchakato unaoendelea sasa wa kupata Katiba Mpya.
“Kumekuwa na hoja ya kuwapo kwa Serikali ya Tanganyika, hilo ni jambo muhimu na watu kutoka Tanganyika ni lazima wawe na Serikali yao ndani ya mipaka ya ardhi yao kupitia Katiba Mpya,” alisisitiza Mchungaji Mtikila.
Aliongeza kuwa nafasi za wabunge wa viti maalumu bungeni ziondolewe ili viti hivyo vishindaniwe kidemokrasia. Alisema wanawake wanatakiwa waelimishwe na kupikwa ili wahimili ushindani katika medani za kisiasa. Alisema kuwa taifa linahitaji viongozi bora na siyo kustarehesha jinsia.
Jukwaa la Wahariri
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limependekeza Katiba ijayo kutambua uhuru wa vyombo vya habari, haki ya kupata habari na uhuru wa kutoa mawazo.
“Kwa Katiba hii na sheria nyingine yoyote isiyoendana na Katiba hii, milele haitaruhusiwa kudhibiti habari nchini Tanzania,” ilieleza taarifa hiyo.
TEF ilisema kuwa haitakiwi kuwe na vikwazo katika kuanzisha magazeti au vyombo vya habari binafsi, kwamba wahariri na wachapishaji wa magazeti na vyombo vingine vya habari hawatakiwi kudhibitiwa au kuingiliwa na Serikali.
“Chombo chochote cha habari chenye wajibu wa kusambaza taarifa kwa jamii ambacho kinachapisha taarifa kuhusu, au dhidi ya mtu yeyote kinawajibika kutoa fursa ya kuchapisha mawazo ya upande wa pili, ikiwa yapo, kutoka kwa mtu ambaye taarifa au chapisho linamhusu,” ilieleza taarifa hiyo.
Vilevile, wamependekeza kuwe na sheria ya Bunge ya kuanzisha Baraza la Habari la Taifa, ndani ya miezi sita tangu siku ya kuanza kutumika kwa Katiba Mpya, baraza ambalo litakuwa na wajumbe 15 kutoka katika taaluma mbalimbali.
“Wajibu wa Baraza la Habari la Taifa itakuwa ni kusimamia vyombo vya habari, kuweka viwango vya kitaaluma kwa vyombo vya habari, kufuatilia utekelezaji wa viwango vilivyowekwa, kukuza taaluma na weledi katika vyombo vya habari,” ilisema taarifa hiyo na kuongeza;
“Kusikiliza mashauri au malalamiko dhidi ya vyombo vya habari, gharama za uendeshaji wa baraza. Kwa mujibu wa Katiba hii, Baraza la Habari la Taifa ndicho kitakuwa chombo cha mwisho katika kusimamia tasnia ya habari nchini.”
Katika suala la haki ya kupata habari, TEF imesema kila mwananchi ana haki ya kupata taarifa zozote hata zile zilizopo mikononi mwa Serikali.
Katika suala la uhuru wa kutoa mawazo Jukwaa hilo limeeleza kwamba kila mtu ana uhuru wa mawazo unaohusisha uhuru wa kutafuta, kupokea au kutoa taarifa au mawazo.
Baraza hilo limesema kuwa uhuru huo hautahusisha propaganda kwa ajili ya vita, uchochezi wa kuanzisha vurugu, hotuba za chuki, utetezi wa chuki, ukabila, ubaguzi kwa watu wengine au kuchochea mapambano.
Mtandao wa Jinsia
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) umetaka Katiba Mpya iwe na dira ya kitaifa inayosisitiza ustawi wa wananchi katika kujenga mazingira ya kuwezesha mihimili mitatu kufanya kazi zake.
Mwenyekiti wa TGNP, Mary Rusimbi alisema kuwa moja ya mambo muhimu ambayo Katiba kwa kupitia itikadi hiyo inapaswa kuyasimamia na kuyastawisha ni haki za wanawake.
“Mchango wa mwanamke ni lazima utambulike kikatiba. Wanawake wana mchango mkubwa katika suala zima la malezi na uzalishaji mali wa aina mbalimbali, hivyo rasilimali za nchi pamoja na bajeti ya nchi zinapaswa kuwanufaisha wanawake kama ilivyo kwa wanaume,” alisema Rusimbi.
Profesa Ruth Meena alisema ni wajibu wa Serikali kuhakikisha mwanamke hafi kwa matatizo ya uzazi kwa kuboresha huduma ya uzazi katika hospitali zote nchini.
“Pia tunataka kuwapo na uwajibikaji wa viongozi. Viongozi ambao hawatimizi wajibu wao wanapaswa kujiuzulu badala ya kusubiri hadi wamalize muda wao wa uongozi, uwe wa miaka mitano au zaidi. Katiba ya sasa haiwapi wananchi mamlaka ya kuwawajibisha viongozi wazembe,” alisema Prof Meena.
Kuhusu Viti Maalumu, Profesa Meena alisema vinapaswa kuboreshwa ili hata wanawake ambao hawana chama cha siasa waweze kuwa na fursa ya kuteuliwa au kuchaguliwa kushika nafasi za uongozi.
Alisema kuwa kwa mfumo wa sasa ni wanawake walio kwenye vyama tu ndiyo wenye haki ya kupata nafasi za viti maalumu.
Wakulima
Wakulima nchini wametaka Katiba Mpya iweke uwiano sawa katika ugawaji wa ardhi kati ya wakulima na wafugaji ili kuondoa migogoro ya mara kwa mara.
Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima Taifa (Taso), Engelbert Moyo alisema hatua hiyo itasaidia kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji na kuimarisha uchumi wa nchi.
“Tunapozungumzia wakulima hata ufugaji unaingia hapo ndiyo maana tukaona kuna haja ya kupendekeza kuwe na maeneo maalumu ya kufanyia shughuli hizo. Katiba iwe chanzo cha kuondoa migogoro hiyo kwa kuweka uwiano sawa katika ugawaji ardhi,” alisema na kuongeza;
“Kama Katiba Mpya itasema hivyo kwamba kutakuwa na ugawaji sawa wa ardhi kwa wakulima na wafugaji itasaidia kuondoa migogoro ambayo inaibuka mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji kitu ambacho hakileti picha nzuri kwa taifa letu.”
Alisema zaidi ya asilimia 80 ya uchumi wa taifa unategemea kilimo, lakini bado maisha ya wakulima yapo chini kitu ambacho ni vyema Katiba Mpya ikaliona.
Wafugaji
Umoja wa Wafugaji, umependekeza Katiba Mpya ijayo ianzishe sheria mpya ya ardhi kwa jamii pamoja na kutambua na kulinda mila na tamaduni za jamii mbalimbali nchini.
“Katiba itambue miliki ya pamoja ya ardhi kwa wafugaji inayoratibiwa na taasisi za jadi kwa mujibu wa sheria za mila za jamii mbalimbali,” alisema William Olenasha.
Alisema kitendo cha hakimiliki ya ardhi kuwa mikononi mwa Rais ni kuwanyima haki wananchi hususan wafugaji.
Rehema Mkalata, mfugaji kutoka Morogoro alisema kwa muda mrefu jamii ya wafugaji imeonekana kuwa ni jamii ya watu duni ndiyo maana hata matatizo yao hayapewi kipaumbele.
Alisema kuwa ni matarajio yake kwamba Katiba Mpya itawatambua jamii ya wafugaji kuwa na thamani sawa na watu wengine.
Pia alisema kuwa Katiba Mpya inatakiwa kuzitambua dawa asilia kuwa zinafaa kwa ajili ya matumizi ya binadamu.

Imeandikwa na Fidelis Butahe, Aidan Mhando, Ibrahim Yamola na Matern Kayela.
 MWANANCHI

No comments

Powered by Blogger.