HUKU TUNAKOELEKEA SIO PAZURI:UKATILI WA KUTISHA BABA AWANYONGA WATOTO WAKE WATATU NA KISHA KUWATUPA KISIMANI PAMOJA NA MAMA YAO.


UKATILI wa kusikitisha! Watoto watatu wa famila moja, wameuawa kikatili kwa kunyongwa huku mama yao akishuhudia. Miili yao pamoja na mama yao akiwa hai, wakatumbukizwa katika kisima cha maji. Baba wa watoto hao, Justine Albert (24) anatuhumiwa kufanya unyama huo.

Kabla ya mauaji hayo, inadaiwa baba huyo alimfunga kamba mkewe na kumziba mdomo kwa kitambaa ili asipige kelele, kisha akaanza kuwanyonga watoto wake wote watatu kwa zamu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari, alisema mauaji hayo ya kikatili yalifanyika juzi saa 11:30 alfajiri katika Kijiji cha Majimoto, Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Mlele mkoani humo.
Kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari, kisa cha kufanya mauaji hayo ni mzozo wa mtuhumiwa na mkewe, Jacqueline Luvika (21), kwamba baadhi ya watoto hao mama huyo kazaa na jirani yao.
Watoto hao ni Frank Justine (6), Elizabeth Justine (4) na kitinda mimba Maria Justine, mwenye umri wa miezi minne.
Baada ya kuwanyonga watoto hao, inadaiwa baba huyo alibeba miili ya watoto Frank na Eliza, na kwenda kuwatumbukiza kwenye kisima cha jirani yao, Kawaida Jonas. 
Kwa mujibu wa madai ya Kamanda Kidavashari, mtuhumiwa baada ya kuwatumbukiza watoto hao kisimani, alimfungua kamba mkewe na kumtoa kitamba alichomziba mdomoni, kisha akamburuta hadi kwenye kisima hicho na kumtumbukiza.
Kugundulika Baada ya matukio hayo yanayodaiwa kufanyika alfajiri, kulipopambazuka baadhi ya wakazi wa kijiji hicho, waliodamka kwenda katika shughuli zao, waliuona mwili wa mtoto ukiwa umetelekeza kando ya njia na kutambua kuwa ni Maria, ambaye ni kitindamimba katika familia hiyo.
Inadaiwa wakazi hao walisitisha safari yao na kwenda nyumbani kwa mtuhumiwa, kumpatia taarifa hiyo ya kuhuzunisha, huku wakiuliza mama wa mtoto aliko.
 Kamanda Kidavashari alidai mtuhumiwa aliwaeleza wakazi hao kuwa mama wa mtoto huyo, alikuwa ametoroka kwenda kusikofahamika na watoto wote.
Majibu hayo ‘rahisi’ kwa mujibu Kamanda Kidavashari, yalisababisha wakazi hao wamtilie shaka mtuhumiwa, wakaamua kutoa taarifa kituo cha Polisi kijijini hapo, ambao walifika ulipo mwili wa mtoto Maria.
Wakati wakiwa katika eneo la tukio, Kamanda Kidavashari alidai walibaini alama za mburuzo ardhini, wakaanza kuifuatilia na zikawafikisha kisimani. Walipofungua mfuniko wa kisima hicho, walishtuka kuona miili wa watu watatu, ikielea kwenye maji kisimani humo.
Askari Polisi kwa kushirikiana na wakazi wa kijiji hicho, waliopoa miili yote, lakini watoto hao wawili tayari walikuwa wamefariki, huku mama yao akiwa amekunywa maji mengi na kupoteza fahamu.
Kutokana na hali hiyo, wakazi hao walipandwa na hasira na kwenda kuvamia nyumba ya mtuhumiwa na kumkamata ili wamchome moto. Hata hivyo, Kidavashari alisema polisi walifanikiwa kufika kwa wakati katika eneo hilo na kumwokoa mtuhumiwa, ambaye kwa sasa bado ameshikiliwa Polisi kwa mahojiano.
Mama wa watoto hao kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari, alikimbizwa katika Kituo cha Afya cha Kijijini cha Mamba wilayani humo, ambako amelazwa kwa matibabu, lakini hadi jana bado alikuwa amezirai. Mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani mara tu baada ya uchunguzi wa awali wa shauri lake kukamilika




MTANZANIA

No comments

Powered by Blogger.