MWANASHERIA MKUU AMGEUKA PINDA

Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Jaji Frederick Werema
Awataka polisi wasitumie nguvu kubwa kudhibiti raia

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, amelitaka Jeshi la Polisi nchini, kuacha kutumia nguvu zilizopita kiasi, pindi linapokuwa likituliza ghasia.


Amesema, pamoja na kwamba jeshi hilo linaruhusiwa kisheria kutumia nguvu wakati wa kutuliza ghasia, nguvu hizo hazitakiwi kuzidi kipimo kwa kuwa kufanya hivyo ni kuvunja sheria.

Jaji Werema alitoa kauli hiyo mjini hapa jana, alipokuwa akifungua mkutano wa mawakili wafawidhi wa Serikali, wakuu wa upelelezi wa makosa ya jinai wa mikoa na vikosi vingine vya polisi.


“Sheria inaruhusu polisi kutumia nguvu katika baadhi ya maeneo, lakini utaratibu lazima ufuatwe. 


“Tusitumie nguvu kubwa kupita kiasi, polisi mmejifunza kutumia mabomu, bunduki na mmejifunza pia kutumia bunduki na kulenga shabaha, usimpige mtu kichwani, hilo ni kosa, lenga kwenye mguu,” alisema Jaji Werema.


Kauli hiyo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, inaonekana kwenda kinyume na kauli iliyotolewa hivi karibuni na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda dhidi ya wanaokaidi maagizo ya polisi.


Katika maelezo yake wakati akijibu swali na papo kwa papo aliloulizwa wakati wa Bunge la Bajeti lililopita, Waziri Mkuu Pinda, aliruhusu polisi wawapige raia pindi wanaposhindwa kutii sheria.


Wakati huo huo, jana Jaji Werema alilitaka Jeshi la Polisi nchini pamoja na wanasheria wa Serikali, kuacha tabia ya kuwabambikia kesi raia badala yake watafute ushahidi wa kutosha.


Alisema kama wanamfahamu mhalifu, wanatakiwa kutumia akili kwa kumkamata kwa kufuata utaratibu wala siyo kumbambikia kesi isiyo na ushahidi.


“Katika baadhi ya kesi tusimkamate mtu kama hatuna ushahidi wa kutosha, tunamkamata mtu siku ya Ijumaa ili tumkomeshe akae ndani halafu Jumatatu anatoka.

Endelea kusoma habari hii kwa kubofya hapa chini



“Unamjua mtu ni mhalifu, lakini unashindwa kumkamata matokeo yake unambambikizia kesi ya mauaji, sio vizuri, tuache tabia hiyo,” alisema.


Alisema kwamba, kama polisi na wanasheria watafanya kazi kwa kufuata utaratibu, utafika wakati wananchi watajenga imani na vyombo vya dola kwa kuwa watumishi hao watakuwa wakizingatia maadili ya kazi yao.


Alitaka pia uwepo ushirikiano wa kutosha kati ya wapelelezi na wanasheria wa Serikali, kwa kuwa bila kufanya hivyo, hakutakuwa na mafanikio katika utendaji kazi wao.


“Kipindi hiki ni kigumu, tunahitaji kushirikiana zaidi kuliko kipindi chochote kingine, wapelelezi na waendesha mashtaka ushirikiano wenu siyo kitu cha hiari bali ni lazima, kwani kama hamshirikiani, hatuwezi kushinda vita dhidi ya uhalifu,” alisema.


Jaji Werema alisema ingawa mawakili wa Serikali wana mamlaka ya kuondoa kesi mahakamani, hawatakiwi kufanya hivyo bila kuwasiliana na kamanda wa upelelezi wa mkoa husika, ili kujenga uwazi na kuondoa mianya ya rushwa.


Aliwataka watendaji hao kuhakikisha wanakuwa waaminifu katika kutunza majalada ya kesi na kuhakikisha wapelelezi hao na mawakili wa Serikali wanafanya uamuzi wa haraka.


Alisema kwamba, kitendo cha watumishi hao kuchelewa kutatua malalamiko ya wananchi, kinawafanya wananchi wakose imani na vyombo vya dola na hivyo kuwapo ukiukwaji wa sheria kwa wananchi.


“Jinsi tunavyotenda kazi zetu, tunaweza kusababisha dola kuchukiwa, halafu ikichukiwa tuwalaumu waandishi, mimi nawaambia, watuandike tu kama tunakosea.


“Tuwe makini pia na mawasiliano yetu kwenye magazeti, sisi ni dola, tusiwasiliane kupitia magazeti, tusitupiane lawama, tuwe na mawasiliano mazuri kati ya ofisi ya DPP (Ofisi ya Mkurugenzi Mashtaka), Ofisi ya DCI (Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai) na siyo kuwasiliana kupitia magazeti,” alisema.


Awali, akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), Elizer Feleshi, alisema ofisi yake kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama, imepokea agizo la Rais Jakaya Kikwete la kuwataka wahalifu kujisalimisha na wapo tayari kulitekeleza.


“Tunawaasa wahalifu watumie vizuri muda wa wiki mbili waliopewa na rais, vinginevyo watajutia vitendo vyao kwa sababu katika mkutano huu, tutajadili namna ambavyo tutawashughulikia wale ambao hawatatekeleza amri hiyo ya rais,” alisema.


Alisema mkutano huo ni miongoni mwa mikutano waliyoanzisha chini ya Jukwaa la Haki Jinai wenye lengo la kuwakutanisha wadau pamoja kujadili changamoto katika utoaji wa haki jinai.


Alisema changamoto mojawapo inayowakabili, ni kupunguza msongamano wa mahabusu na wafungwa magerezani na kwamba idadi yao imepungua kutoka wafungwa 45,000 mwaka 2003 hadi wafungwa 33,033 kufikia Julai mwaka huu.


Pamoja na hayo, alisema uwezo wa magereza yote nchini ni kuhifadhi wafungwa 29,552.


MTANZANIA

No comments

Powered by Blogger.