RIPOTI MAALUM: TINDIKALI HATARI

Tindikali ikiwa katika ndoo tayari kwa kuuzwa, uchunguzi umebaini kuwa bidhaa hii hatari huuzwa kiholela jijini Dar es Salaam
Dar es Salaam. Siku chache baada ya wasichana wawili raia wa Uingereza kumwagiwa tindikali mjini Zanzibar, imebainika kuwa, tindikali za aina mbalimbali zinauzwa kiholela kama njugu jijini Dar es Salaam.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili unaonyesha kuwa jijini Dar es Salaam yapo maduka mengi yanayouza tindikali ya kila aina na bidhaa hiyo inauzwa bila ya udhibiti wowote kuanzia Kariakoo hadi Vingunguti.
Wiki iliyopita, Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manyele alitoa miezi mitatu kwa wafanyabiashara wa tindikali kujisajili ili kuzuia kuongezeka kwa matukio ya uhalifu kwa kemikali hiyo nchini.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika mitaa ya Dar es Salaam, umebaini kuwa tindikali za aina mbalimbali zinapatikana kwa wingi katika maduka ya rejareja na jumla, huku wauzaji wa bidhaa hizo wakishindwa kutoa tahadhari yoyote kwa wateja wao.
Imebainika kuwa tindikali zinazopatikana kwa urahisi zaidi ni Sulphonic Acid ambayo imetajwa kutumika kutengeneza sabuni za maji (multipurpose detergents), Sulfuric acid inayotumika kutengeneza maji ya betri na Hydrochroric acid inatumiwa na wajasiriamali kutengeneza dawa za usafi.
Kemikali nyingine ambayo imeelezwa na watumiaji wake kuwa ni hatari ni Hydrogen Peroxide ambayo hutumika kusafisha mafuta ya mawese yanayotumika kutengenezea sabuni za kipande.
Endelea kusoma habari hii kwa kubofya hapa chini 
Katika Mtaa wa Gerezani Kariakoo, kuna duka maalumu la kuuza kemikali mbalimbali kwa bei ya rejareja na jumla, kemikali hizo zinauzwa kati ya Sh4,000 hadi Sh6,000 kwa kilo moja kutokana na aina yake.
Muuza kemikali mmoja katika mitaa ya Sinza wilayani Kinondoni, ambaye hakutaka kutaja jina lake gazetini kuhofia usalama wake, alisema biashara hiyo ilianza kushamili miaka mitatu iliyopita baada ya kuanzishwa kwa mafunzo ya kutengeneza bidhaa mbalimbali zinazotumia kemikali.
“Matangazo yanayotolewa katika vyombo vya habari kuhusu ujasiriamali wa kutengeneza sabuni aina mbalimbali, ndiyo yaliyochochea kuongezeka kwa mahitaji ya tindikali hapa nchini. Kwa mfano, (anamtaja mhusika) anafundisha namna ya kutengeneza maji ya betri za magari kwa kutumia Sulphuric acid, unategemea wajasiriamali wakanunue wapi hiyo tindikali?” anahoji.
Matukio ya kujeruhiwa na tindikali
Agosti 7 mwaka huu raia wawili wa Uingereza, Kate Gee na Kirstie Trup wote miaka 18 walishambuliwa kwa tindikali na watu wasiojulikana wakati wakitembea kwenye mitaa ya Stone Town mjini Zanzibar. Raia hao walisafirishwa na kurudishwa Uingereza ambako wanaendelea na matibabu.
Kabla ya kuondoka nchini, Rais Jakaya Kikwete aliwatembelea raia hao hospitali na kusema kuwa tukio hilo limeitia aibu nchi kwa mataifa ya nje na kuliamuru Jeshi la Polisi kuhakikisha linawakamata na kuwafungulia mashtaka wote waliohusika.

Tukio jingine ni lile lililotokea Julai 18, 2013 ambapo mmiliki wa Kampuni ya Home Shopping Centre (HSC), Said Mohammed Saad alimwagiwa tindikali usoni watu wasiojulikana jijini Dar es Salaam.
Julai 12, 2013, Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Said Juma Makamba alijeruhiwa kwa kumwagiwa maji yanayohisiwa kuwa tindikali na watu wasiojulikana usiku akiwa nyumbani kwake jijini Arusha.
Novemba 5, 2012, Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Suleiman Soraga alimwagiwa tindikali na mtu asiyefahamika iliyomwathiri sehemu kubwa ya mwili wake.
Tukio hilo lilitokea karibu na nyumba yake Mwanakwerekwe, saa 12:00 asubuhi wakati alipokuwa akifanya mazoezi muda mfupi baada ya kumaliza swala ya Alfajiri.
Katika hatua nyingine mkazi wa Sinza jijini Dar es Salaam, John Simon Mabula anasema kuwa hivi sasa watu wengi wakiwamo ndugu zake wamenunua wanaitumia tindikali kama silaha ya kujilinda dhidi ya vibaka na wezi.
“Hivi sasa tindikali zina matumizi mengi, ndugu zangu wanaitumia kwa ajili ya kujilinda dhidi ya vibaka na wezi,” anasema.
Maeneo inakouzwa tindikali
Uchunguzi uliofanywa katika mitaa ya maeneo ya Vingunguti yenye viwanda vingi, umebaini kuwa kuna viwanda viwili vinavyouza tindikali na kwamba viwanda hivyo ndivyo vinavyotajwa kuwa wasambazaji wakubwa wa kemikali hiyo hatari hapa nchini.
Katika kiwanda cha kwanza mwandishi wetu alijifanya kuwa ni mteja anayehitaji kununua kemikali kwa ajili ya kutengeneza sabuni za mche, aliambiwa bei ya sulphuric acid ni Sh45,000 kwa lita 50 na Hydrogen Peroxide Sh60,000 kwa lita 30.
Muuzaji katika kiwanda hicho ambaye jina lake linahifadhiwa, alikiri kusikia agizo la serikali linalowataka kufuata sheria za uuzaji na usambazaji wa tindikali na kwamba baada ya miezi mitatu hawataruhusiwa kumuuzia mtu yeyote ambaye hatakuwa na leseni.
“Hata wewe tutakuuzia kwa sababu muda tuliopewa haujakwisha, lakini baada ya miezi mitatu hatutakuuzia haya madawa hadi uwe na kibali…hapa unaweza kupata mzigo kiasi chochote unachokihitaji hata lita 1,000,” alisema muuzaji huyo.
Katika kiwanda cha pili, ambacho kipo hatua chache kutoka kile cha kwanza, mwandishi wetu alijitambulisha getini kuwa ni mteja anayehitaji kununua kemikali kwa ajili ya kutengeneza sabuni za mche na maji.

Muuzaji alichukua karatasi yenye orodha ya kemikali na bei zake kisha aliandika pembeni; sulphonic acid kilo10 Sh 35, 000 na Hydrogen Peroxide kilo 30 Sh53,100.
Hata hivyo, mwandishi wetu alinunua Sulphonic acid pekee yake na kukabidhiwa risiti (Tax Invoice) yenye kumbukumbu namba 129412 bila ya kupewa elimu ya tahadhari ya kuitumia.
Mtaalamu wa kemikali
Mtaalamu wa kemikali, Wiseborn Makaka, anasema kuwa kemikali za Hydrochroric acid, Sulphuric acid na Sulphonic acid zote zipo katika kundi moja lenye madhara makubwa kwa binadamu kulingana na wingi wa kemikali iliyotumika.
“Ukiwa umezinunua kama zilivyo yaani haujachanganya na maji, kitaalamu tunaita concentrated acid ni hatari sana. Iwapo utadondokewa hata na tone moja sehemu hiyo itaunguzwa na kuchimbwa kwa ndani, usipowahi kuosha kwa maji inaweza kuchimba hata mfupa ukaonekana,” anasema Makaka na kuongeza kuwa:
“Ukimwagiwa machoni unakuwa kipofu labda uoshe kwa maji mengi sana.”Mtaalamu huyo anaongeza kuwa kemikali hizo si rafiki wa nguo, kwani zikidondokea huiacha nguo ikiwa na matundu na kwamba mtu yeyote atakayekunywa tindikali atapoteza maisha yake.
“Ukiwekewa kwenye chakula huwezi kuishi, utakufa hii inatokana na kwamba mwili una protein, na protein ni amphoteric, hivyo endapo utakutana na acid tu lazima reaction itatokea,” anafafanua Makaka.
Vilevile, Makaka anasema kemikali za Hydrochloric acid na Nitric acid zina athari kubwa kwa binadamu iwapo atavuta hewa yake bila kuvaa kifaa cha usalama puani.
Anasema kwa ujumla kemikali zinazotumika kutengenezea sabuni za maji zimebainika kuwa na madhara makubwa zaidi zikilinganishwa na zile za mche.
Mtumiaji wa tindikali
Mkurugenzi wa Mode Integrated Solution, Mahmoud Omar ambaye kampuni yake inafundisha mafunzo ya kutengeneza sabuni na bidhaa nyingine anasema kuwa serikali inapaswa kutafakari upya uamuzi wake wa kudhibiti tindikali kwa kuwa utawaathiri wajasiriamali wengi wadogo.
Anasema wafanyabiashara wadogo wananufaika kwa kutengeneza bidhaa mbalimbali zinazotumia tindikali, hivyo udhibiti uliowekwa na serikali utaifanya bidhaa hiyo kuuzwa kwa njia za panya. “Tamko la serikali linawaua wajasiriamali. Watu wengi tumewaokoa, sasa hivi kila mtu ana kiwanda kidogo nyumbani…kwa namna hii biashara itakuwa ya magendo,” anasema Omar.
MWANANCHI

No comments

Powered by Blogger.