ZITTO AVITIKISA VYAMA

Dar es Salaam. Maelekezo yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe kutaka kusitishwa kwa ruzuku kwa vyama vya siasa nchini kutokana na kutowasilisha taarifa za ukaguzi wa matumizi yake, yamevivuruga baadhi ya vyama vilivyotajwa.
Vyama vya siasa vinaonekana kutoa matamshi yanayolenga kujinasua katika hoja hiyo, vikiwemo vilivyomshutumu Zitto, kuilaumu Serikali na hata vingine vimediriki kutaka ruzuku hiyo ifutwe kwa maelezo kwamba ni ubadhilifu wa fedha za umma.
Juzi Zitto alisema tangu 2009 Serikali ilitoa kiasi cha Sh67.7 bilioni kama ruzuku kwa vyama tisa vya siasa, lakini vyama hivyo havijawahi kuwasilisha taarifa za ukaguzi hesabu zake msajili kama sheria inavyoagiza. Kwa sababu hiyo, Zitto aliamuru Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, kusimamisha utoaji wa ruzuku hadi hapo vitakapowasilisha ripoti ya ukaguzi na makatibu wake wakuu kuhojiwa.

ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI 
Kwa mujibu wa Sheria namba 5 ya 1992 ambayo ilifanyiwa marekebisho ya Sheria namba 7 ya 2009, Vyama vya Siasa vinawajibika kuwasilisha hesabu zake kwa CAG na ofisi hiyo inaweza kuamua kuzifanyia ukaguzi yenyewe au kuteua mkaguzi.
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh aliwahi kusema kuwa utaratibu ambao umekuwa ukitumiwa na vyama hivyo kwa kuteua kampuni binafsi siyo sahihi na ni kinyume cha sheria.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 14 cha Sheria ya Vyama vya Siasa, vyama vinatakiwa viwasilishe hesabu kwa CAG, ndipo tuzikague au tuamue kampuni ya kufanya ukaguzi huo, sasa wao walichagua kampuni binafsi moja kwa moja zikawafanyia ukaguzi,” alisema Utouh wakati akitangaza kuthibitisha ubora wa hesabu za vyama vitano vilivyoshiriki kwenye Uchaguzu Mkuu wa 2010.
Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila alipendekeza kufutwa kwa ruzuku hiyo kwa vyama vya maelezo kuwa ni inawanyonya wananchi.
“Badala ya kuvipa vyama vya siasa ruzuku, tuelekeze fedha hizo kwenye miradi mingine ya maendeleo,” alisema Mtikila huku akiahidi kwamba chama hicho kitawasilisha kwa Msajili wa Vyama vya Siasa taarifa yake ya fedha iliyokaguliwa katika kipindi cha wiki mbili kuanzia sasa.
CCM wang’aka
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimemshambulia kiongozi huyo, huku kikisema kuwa Zitto ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema anapaswa kushughulikia matatizo yaliyopo katika chama chake kwanza kabla ya kuzungumzia matatizo katika vyama vingine vya siasa.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema chama hicho hakihusiki na agizo la PAC la kusimaishiwa ruzuku ya kila mwezi, kwani hesabu zake zimekuwa zikifanyiwa ukaguzi. Alisema CCM ipo tayari kwenda mbele ya PAC kikiwa na hesabu zilizokaguliwa na wakaguzi wa nje, Shirika la Ukaguzi la Taifa (Tanzania Audit Corporation - TAC) kuanzia 1977/1978 hadi 2010/2011.
“Januari 29, mwaka huu niliandika barua yenye kumbukumbu namba CMM/F. 20/80/89 ili kuwasilisha rasimu ya hesabu za mwaka wa fedha 2011/2012 lengo likiwa CAG atupangie siku ya TAC kutukagua,” alisema Nape na kuongeza: “Hesabu zilizokaguliwa na wakaguzi wa nje TAC ambazo ni za 2009/2010 na 2010/2011 tayari ziliwasilishwa kwa CAG.”
Nape alifafanua kwamba hesabu za 2011/2012 bado ziko kwa wakaguzi wa nje, wakishakamilisha nazo zitawasilishwa kwenye vikao vya chama na hatimaye kwa CAG.
“Hesabu hizi zikikaguliwa kwa mujibu wa utaratibu, anapelekewa CAG ambaye ndiye anazipeleka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa na sio vinginevyo,” alisema.
Alidai kuwa Zitto anapaswa kuanza kutoa ‘boriti kwenye jicho lake ndipo aone kibanzi kwenye jicho la mwenzake’ kwa sababu chama chake ndicho kimekuwa na matumizi mabaya ya ruzuku. Alisema Zitto kama Naibu Katibu Mkuu wa Chadema ni vyema akawajibika ndani ya chama chake ili kuonyesha mfano kwa wengine.
“Wote tunakumbuka kelele zilizopo mtaani kuhusu matumizi mabaya ya ruzuku zinazoelekezwa na Chadema na viongozi wake kutoka kwa wanachama wao, hivyo si ajabu wakawa wanakiuka sheria hii na ndiyo chanzo cha kelele hizo za wanachama wao,”alisema.
Vyama vingine
Kwa upande wake, Chadema kilieleza kwamba hakijapata barua inayowaarifu kuhusu kutaka kufungiwa ruzuku kutokana na kutowasilisha taarifa ya ukaguzi.
Ofisa Habari Mwandamizi wa Chadema, Tumaini Makene ilisema hata barua ya kuitwa kwenye Kamati ya PAC, iliwafikia kwa kuchelewa. “Tunasubiri barua rasmi ya suala hili ndio mamlaka zinazohusika na masuala ya fedha ndani ya chama, hususan, Baraza la Wadhamini wa Chama kuweza kutafakari hatua,” alisema Makene.
Hata hivyo, alisema angependa umma utambue kwamba “Chadema ndicho kilichokuwa mstari wa mbele tangu kabla na baada ya mwaka 2009 kutaka ukaguzi na wazi katika mapato na matumizi ya vyama vya siasa.”
Alifafanua kuwa msimamo wa Chadema kwenye mkakakati huo ulikuwa ni kuibana CCM kutokana na madai ya baadhi ya vigogo wake “kukwapua fedha Benki Kuu ( Akaunti ya Madeni ya Nje – EPA) na kuzitumia kwenye uchaguzi wa mwaka 2005.”
Alijigamba kuwa hesabu za chama chake zimekuwa zikikaguliwa kila mwaka na kwamba wanasubiri maelezo ya barua kuhusu kile kinacholalamikiwa.
Kwa upande wa Chama cha Wananchi (CUF) kimesema hesabu zake ziko safi, ila imeshindikana kukaguliwa kwa vile Serikali haijatoa fedha za kugharimia ukaguzi huo.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Tanzania Bara, Julius Mtatiro alisema hesabu zao zimekwishakaguliwa na wakaguzi wa ndani.
 “Tunachosubiri ni Serikali kutuletea mkaguzi ambaye baada ya kufanya hivyo hesabu zetu zitakuwa zimekamilika na wananchi wataweza kuziona,” alisema.
Alisema chama hicho hakina fedha kwa ajili ya kugharimia mkaguzi wa nje na kwamba jukumu hilo ni la Serikali.
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Samwel Ruhuza alisema kuwa chama hicho kipo tayari kuwasilisha hesabu zake, kwani zipo tayari na kwamba walishindwa kuziwasilisha baada ya kuelezwa kuwa CAG ndiye anayepaswa kufanya ukaguzi.
Imeandaliwa na Aidan Mhando, Leon Bahati, Fidelis Butahe na Raymond Kaminyoge

MWANANCHI

No comments

Powered by Blogger.