VIFO AJALI YA BASI LA LUHUYE VYAONGEZEKA NA KUFIKIA 15

Na Samwel Mwanga-Simiyu

IDADI ya vifo vilivyotokea kufuatia ajali mbaya ya basi la Luhuye Express linalofanya safari zake kati ya mji wa Tarime mkoani Mara na Jijini Mwanza iliyotokea April 21 mwaka huu majira ya saa 5:11 asubuhi katika kijiji cha Itwimila wilayani Busega mkoa wa Simiyu imeongezeka na kufikia 15.

Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa polisi mkoa wa Simiyu,Kamishina Mwandamizi wa Polisi(SACP),Charles Mkumbo kwa vyombo vya habari inaeleza kuwa idadi hiyo imeongezeka kufuatia kufariki kwa majeruhi wanne wa ajali hiyo waliokuwa wakipatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa ya Bugando.

Kamanda Mkumbo aliwataja marehemu ambao hadi sasa wametambuliwa kuwa ni Mohama Kidela(32) mkazi wa Bugarika Jijini Mwanza,Alex Masatu(42)mkazi wa Musoma,Wangwe Morice(30) Afisa Elimu Msaidizi Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Mahemba Chacha(42)mkazi wa Serengeti mkoani Mara,Thomas Mwita(40)ambaye ni Mchungaji wa kanisa la SDA mjini Kahama mkoani Shinyanga.

ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
 
Wengine ni pamoja na Esther Morice(18) mkazi wa Tarime mkoani Mara, Rose Willison(21) mkazi wa Igoma Jijini Mwanza,Shepa Msongoma(58) mkazi wa Nassa wilayani Busega na Mtoto Baarka Alex(1) ambaye makazi yake hayajajulikana.

Pia Kamanda Mkumbo amewaomba watu mbalimbali kufika katika hospitali ya Rufaa ya Bugando  Jijini Mwanza  ili kuweza kutambua miili ya ndugu zao kwani hadi sasa maiti sita bado hazijatambuliwa.

Majeruhi 33 bado wanaendelea na matibabu katika hospitali ya Bugando Jijini Mwanza na majeruhi 11 bado wanaendelea na matibabu katika hospitali ya wilaya ya Magu mkoani Mwanza.

Katika hatua nyingine jeshi la polisi mkoani humu linamshikilia mmiliki wa basi hilo,Masalu Jackson mkazi wa Majengo mjini Bunda mkoani Mara ambaye alikamatwa wilayani Busega mkoani humu kufuatia ushirikiano wa jeshi la polisi na wananchi huku wakiendelea kumtafuta aliyekuwa dereva wa Basi hilo ambaye jina lake halijapatikana alitoroka mara baada ya ajali kutokea.

Basi la Luhuye Express lenye namba za usajiri T 410 AWQ liliacha njia na kugonga nyumba ya marehemu Mwalimu,Lazaro Mbofu na kuibomoa yote na kisha kupinduka na watu 10 kufa papo hapo.

NA GEITA  YETU

No comments

Powered by Blogger.