SHEREHE ZA MEI MOSI ZAINGIA DOSARI, MFANYAKAZI WA IKULU AFIA UWANJANI

Wafanyakazi wa Chama cha Msalaba Mwekundu wakitoa msaada kwa Rashid John Chilwangwe mara bada ya kuanguka.
 Baadhi ya jamaa aliyoambatana nao wakimwangalia mara baada ya kufikishwa chumba cha huduma ya kwanza.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI

Wafanyakazi wa Chama cha Msalaba Mwekundu wakitoa msaada wa huduma ya kwanza kwa mfanyakazi wa Ikulu, Rashid John Chilwangwe (45), ambaye alidondoka na kupoteza fahamu wakati wa Maadhimishisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam. Hata hivyo baadae aliripotiwa kufariki dunia. (Picha na Francis Dande)
Mwili wa marehemu Rashid John Chilwangwe ukiwekwa katika gari la wagonjwa kwa ajili ya kwenda kuhifadhiwa katika hospitali ya Temeke. 
Gari la wagonjwa lililombeba likiondoka uwanjani kuelekea hospitali.

Na Mwandishi Wetu
MAADHIMISHO ya Siku ya Wafanyakazi Kitaifa, maarufu kama Mei Mosi yaliyofanyika leo jijini Dar es Salaam yameingia dosari baada ya mmoja wa wafanyakazi kufariki dunia uwanjani kwa ghafla akiwa katika maadhimisho hayo.
Mfanyakazi huyo anayedaiwa kufanyakazi Ikulu alizidiwa ghafla akiwa katika maandamano na kupatiwa huduma za kwanza lakini hali yake ilizidi kuwa mbaya na hatimaye kudaiwa kupoteza maisha akipatiwa huduma na madaktari na wahudumu kutoka kikosi cha msalaba mwekundu waliyokuwa katika maadhimisho hayo.
Thehabari.com ilishuhudia mfanyakazi huyo akiletwa katika kambi ya watu wa huduma ya kwanza iliyokuwa katikati ya uwanja wa Uhuru, kisha kupatiwa huduma ya kwanza bila mafanikio na baadaye alifariki dunia. Kwa mujibu wa taarifa kutoka katika kundi ambalo lilimleta mfanyakazi huyo baada ya kuzidiwa ghafla lilimtaja kuwa jina lake ni Rashid John Chilwangwa.
Mmoja wa wafanyakazi waliyokuwa wameandamana na mfanyakazi huyo ambaye hakupenda kutaja jina lake kwa kuwa yeye si msemaji akisimulia tukio hilo, alisema John Chilwangwa (45) walikuwa naye katika sherehe za maadhimisho na hali yake ilibadilika kabla ya kuingia uwanjani na aliomba aende kujisaidia haja ndogo baada ya hapo alianza kuishiwa nguvu.
“…Si tulishangaa alikaa muda kidogo akijisaidia baada ya kumfuata tulimkuta ametoka ndani ya choo na kuja nje na kisha kukaa kwenye tofali huku akisema anajisikia kuishiwa nguvu na hali ilibadilika ndo tukamleta hapa,” alisema shuhuda huyo.
Alipoulizwa hali yake kwa sasa ambapo alikuwa ameingizwa kwenye hema la huduma ya kwanza kwa wahudumu kutoka kikosi cha msalaba na madaktari alisema wamejaribu kumuhudumia lakini bahati mbaya amefariki dunia tayari. “…Tumeambiwa na madaktari kuwa ameshafariki tayari,” alisema shuhuda huyo ambaye alikuja na mgonjwa huyo.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia madaktari wakijaribu kumtundikia dripu huku wakijaribu kurudisha mapigo ya moyo kwa kushtua mara kadhaa lakini juhudi ambazo hazikuzaa matunda. Baada ya kubaini amefariki dunia walisita kumwekea dripu ambayo ilikuwa inaandaliwa na badaye walimfunika kwa shuka nyeupe na kuita gari la wagonjwa tayari kwa kumpeleka hospitali kwa uchunguzi zaidi. Hata hivyo hakupatikana mara moja daktari kuzungumzia kilichomsibu Chilwangwa.

No comments

Powered by Blogger.