JE UTAFUTAJI WA MASOKO YA BIASHARA YAKO HAUFANYI KAZI? KITU GANI KIFANYIKE?

Biashara zetu tunazianzisha zikiwa na makusudi fulani lakini kama hakuna njia sahihi ya kutafuta masoko kasi ya biashara huanza kuzorota. Ili kuboresha masoko inakubidi kila wakati kuboresha huduma zako, soko na wateja wako. Usisubiri wateja waje kwako kabla ya wewe kuwafikia; kuna maswali matano ambayo unatakiwa kuyajibu kama biashara yako haifanyi vizuri sokoni.


1. Je utendaji wenu haubadiliki badiliki? Kama wewe ni mfanyabiashara inabidi ufuatilie namna mnavyofanya kazi au jinsi mnavyouza bidhaa zenu. Kama mfumo wenu unabadilika kila mara wateja wanachanganyikiwa hivyo kushindwa kuwategemea sana. Mfano; Utoaji wa huduma ukoje tokea mwaka umeanza hadi sasa? Watoa huduma wako ni wale wale au wamebadilika? Je wateja wameathirika vipi na mabadiliko hayo?
Kitu ambacho unatakiwa kujua ni kwamba wateja wanahitaji mfanyabiashara mwenye msimamo na bidhaa au huduma yake. Unatakiwa kutobadiisha ubora wa bidhaa au huduma kwa wateja, ukishindwa kufanya hivyo unapoteza soko na wateja wanaacha kukwamini.

2. Je unakwenda na wakati? Unapotangaza bidhaa yako inakubidi uende na wakati, ujue kitu gani kinafaa kwa sasa au lugha gani utumie kwa sasa na kwa wateja wako. Teknolojia inavyokua na wewe unatakiwa kukua namna unavyofanya kazi, kushindwa kwenda na wakati unapoteza fulsa ya solo lako kukua.

3. Je unatangaza kwa njia sahihi? Kitu cha kushangaza wasomaji wengi hupenda kufuatilia bidhaa fulani kwenye mtandao wa kijamii. Kuna kitu cha ziada kwanini wanafuatilia bidhaa au huduma hiyo. Swali ni je unapotangaza bidhaa au huduma yako unaandika nini au inabeba ujumbe gani? Inakubidi uweke ujumbe utakaovutia watu kufuata bidhaa yako au huduma yako, usiweke huduma bila kuwa na habari nyuma yake inayohusu huduma au bidhaa hiyo.

ENDELEA KUSOMA MAKALA HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI



Kitu cha pili tafuta kujua wateja wako wanapatikana wapi na wewe unatangaza wapi? Ukishindwa kujua wateja wako au wateja unaowategemea wanapatikana wapi utajikuta unatangaza sehemu ambayo si sahihi na hivyo kupoteza fedha na muda.

4. Je unawasikiliza wateja wako? Hili ni mambo la msingi, haijalishi una huduma nzuri kiasi gani au bidhaa nzuri kiasi gani kitu unachohitaji ni kujua wateja wako wanahitaji nini. Utakapojua hivyo ndipo utakapoweza kulishinda soko. Usilete huduma ukifikiri watu wataipenda bila kufanya uchunguzi kuhusu bidhaa hiyo au huduma hiyo. Je unasikiliza?

5. Je washindani wako wanafanya nini kwa sasa? Unatakiwa kujua washindani wako wanafanya nini na kitu gani kinawafanya wafanikiwe na kitu gani ambacho hawajafanikiwa. Fanya uchunguzi jinsi gani washindani wako wanavyofanya, ujue udhaifu wako na utendee kazi.
Utafutaji wa masoko sio kutangaza tu bali ni kujua kitu gani wateja wanahitaji na namna gani utaweza kuongeza wateja na kukuza solo la biashara yako.

NA BONGO 5

No comments

Powered by Blogger.