FAHAMU JUU YA KUCHANGIA DAMU KWA MAMA MJAMZITO (MASWALI NA MAJIBU)

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.

Aina za damu
Aina ya damu (pia huitwa kikundi cha damu) ni uainishaji wa damu kwa kuzingatia kuwepo au kutokuwepo kwa dutu za antijeni za kurithiwa kwenye uso wa chembechembe nyekundu za damu (RBCs). Aina ya damu (Kikundi cha damu) inaamuliwa kwa sehemu, na antijeni za aina ya damu ya ABO zilizo kwenye chembechembe nyekundu za damu.
Aina za damu huathiriwa na huwakilisha michango kutoka kwa wazazi wote wawili. Jumla ya mifumo 30 ya aina ya damu ya binadamu (ikiwa ni pamoja na mifumo ya ABO & Rh) sasa inatambuliwa na Shirika la Kimataifa la Upaji wa Damu (ISBT).
Aina ya damu kamili ni seti kamili ya dutu 30 kwenye uso wa chembechembe nyekundu za damu na aina ya damu ya mtu ni mojawapo ya miungano iwezekanayo ya antijeni za aina ya damu. Katika aina hizo 30 za damu, zaidi ya antijeni 600 tofauti za aina ya damu zimepatikana, lakini nyingi ya hizi ni nadra sana au kwa kiasi kikubwa hupatikana katika makabila fulani.
Mfumo wa ABO ni mfumo muhimu zaidi wa aina ya damu katika kuongezewa damu kwa binadamu. Kingamwili kinza-A na kingamwili kinza-B zinazohusika kwa kawaida ni kingamwili za Immunoglobulini M, inayofupishwa IgM. Mfumo wa Rh ni mfumo wa pili muhimu zaidi wa aina ya damu katika kuongezewa damu kwa binadamu ukiwa na antijeni 50 kwa sasa.

Wanawake wengi wajawazito hubeba kijusi kilicho na aina ya damu tofauti na yao na mama huweza kutengeneza kingamwili dhidi ya chembechembe nyekundu za damu za kijusi. Wakati mwingine kingamwili hizi za mama zinaweza kuvuka kondo na kusababisha hemolosia ya chembechembe nyekundu za damu, ambayo inaweza kusababisha ugonjwa wa hemolitiki wa mtoto mchanga (HDN), ugonjwa wa hesabu ya chini ya damu ya kijusi.
Karibu kila mara, mtu ana aina moja ya damu maisha yake yote, lakini mara chache sana aina ya damu ya mtu hubadilika kwa sababu ya kuongezeka au ukandamizaji wa antijeni katika maambukizi, donda ndugu au ugonjwa kinga mwili nafsi.
Aina/Makundi ya damu na Upatanifu wa Chembechembe nyekundu za Damu
  1. Watu wenye damu ya aina ya AB wana antijeni zote mbili za A na B kwenye uso wa chembechembe zao nyekundu za damu na majimaji yao ya damu hayana kingamwili zozote dhidi ya antijeni A au B. Kwa hivyo, mtu mwenye damu ya aina ya AB anaweza kupokea damu aina yoyote (aina ya AB inapendekezwa) lakini anaweza kutoa damu kwa mwingine mwenye aina ya AB pekee.
  2. Watu wenye damu ya aina ya A wana antijeni ya A kwenye uso wa chembechembe zao nyekundu za damu na majimaji yao ya damu yana kingamwili za IgM dhidi ya antijeni ya B. Kwa hivyo, mtu mwenye damu ya aina ya ya A anaweza kupokea damu kutoka kwa watu wenye aina ya A au 0 pekee (aina ya A inapendekezwa) na anaweza kutoa damu kwa watu wengine wenye aina ya A au AB.
  3. Watu wenye damu ya aina ya B wana antijeni ya B kwenye uso wa chembechembe zao nyekundu za damu na majimaji yao ya damu yana kingamwili za IgM dhidi ya antijeni ya A. Kwa hivyo, mtu mwenye damu ya aina ya B anaweza kupokea damu kutoka kwa watu wenye aina ya B au O (aina ya B inapendekezwa) na wanaweza kutoa damu kwa watu wenye aina ya B au AB.
  4. Watu wenye damu ya aina ya O (au kikundi cha damu cha sifuri katika nchi kadhaa) hawana antijeni A au B kwenye uso wa chembechembe zao nyekundu za damu lakini majimaji yao ya damu yana kingamwili kinza-A na kingamwili kinza-B za IgM dhidi ya antijeni za aina ya damu za A na B. Kwa hivyo, mtu mwenye damu ya aina ya 0 anaweza tu kupokea damu kutoka kwa mtu mwenye aina ya 0, lakini anaweza kutoa damu kwa watu wa aina yoyote ya ABO (yaani kundi A, B, AB & O).
Masuala ya kuzingatia kabla ya kuchangia damu kwa mama mjamzito
Kabla ya Kuchangia damu
  1. Zingatia ulaji wa vyakula vyenye madini chuma kama nyama nyekundu (mfano nyama ya ng'ombe), samaki, maharage n.k
  2. Pata chakula bora chenye afya yaani mlo kamili. Epuka vyakula vyenye mafuta hasa vilivyokaangwa.
  3. Kunywa maji mengi angalau glasi 6 hadi 8.
  4. Pata usingizi mzuri wa usiku.
  5. Kumbuka kuwa na kitambulisho chako chochote.
Wakati wakuchangia damu
  1. Vaa nguo inayoweza kukunjwa hadi juu ya kiwiko.
  2. Muonyeshe mtoa damu mkono unaotaka utolewe damu, ikiwezekana muonyeshe na mshipa uliofanikisha kutolewa damu wakati uliopita kama umewahi kuchangia damu.
  3. Kuwa mtulivu wakati wa kutolewa damu ikiwezekana ongea na mchangiaji damu aliyekaribu yako au sikiliza muziki wa taratibu.
  4. Punde umalizapo kuchangia damu, tumia muda wako kufurahia vyakula na vinywaji laini vilivyoletwa na wahamasishaji wa kuchangia damu.
Baada ya kuchangia damu
  1. Kunywa maji mengi zaidi na jiepushe na pombe ndani ya masaa 24 yajayo.
  2. Ondoa bandeji/pamba iliyowekwa pale ulipotobolewa kuzuia damu isitoke baada ya saa 1 baada ya kuchangia damu.
  3. Sehemu iliyochomwa sindano kama bado inatoa damu, izibe kwa nguvu na pamba kavu kisha nyoosha mkono juu kwa dakika 5 hadi 10.
  4. Ili kuepuka maambukizi ya ngozi na muwasho osha kwa maji na sabuni sehemu ya mwili iliyotumika kutoa damu.
  5. Usifanye kazi ngumu yoyote kama kubeba vitu vizito ndani ya siku yote ambayo umetoa damu.
  6. Kama unasikia kizunguzungu na kuishiwa nguvu & pumzi baada ya kuchangia damu unapaswa kukaa chini au kulala hadi utakapojisikia vizuri.
  7. Kula vyakula vyenye protini kwa wingi baada ya kuchangia damu mfano nyama ya ng'ombe, kuku, kunde n.k
Mawali na majibu juu ya Uchangiaji damu
Inachukua muda gani kuchangia damu?
Hatua zote mpaka damu kuwa imetolewa inachukua kama saa moja na dakika 15. Muda mahususi kwa kutoa damu chupa moja ya damu ni dakika 8 hadi 10, ingawa muda hutofautiana kwa sababu tofauti kama hali ya afya ya mchangia damu na mahudhurio ya sehemu za kuchangia damu.
Wakati gani mjamzito hupungukiwa damu?
Upungufu wa damu wakati wa ujauzito unaweza kutokea katika mabidiliko ya kawaida ya ujauzito ambapo chembechembe nyekundu huongezeka kwa kiwango kidogo kuliko maji(Physiological hemodilution), hata hivyo mabadiliko haya yanaweza kurekebishwa kwa kutumia madini chuma na folic acid bila kuhitaji kuongezewa damu. Matatizo yanayoweza kusababisha upungufu mkubwa mpaka kuhitaji kuongezewa ni pamoja na lishe duni(isiyo na madini chuma na vitamin stahiki), maambukizi ya minyoo, malaria, kupasuka kwa mimba iliyotungwa nje ya mfuko wa uzazi (Ruptered Ectopic Pregnancy), kutoka/kutoa mimba, kutokwa damu ukeni kabla, wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua.
Mama mjamzito huhitaji kuchangiwa damu wakati upi?
Mama mjamzito huhitaji kuchangiwa damu wakati wowote kabla hajapata matatizo yatakayopelekea kupungukiwa damu. Damu inaweza kuhifadhiwa na kusubiri hali ya dharula ikitokea.
Nini madhara ya mjamzito kupungukiwa damu?
Upungufu wa damu wa muda mrefu unaweza athiri maisha ya mama na mtoto aliyetumboni.Mama anaweza kujikuta moyo ukashindwa kufanya kazi vizuri na kupoteza maisha. Mtoto hataweza kukua vizuri na anaweza fia tumboni au akazaliwa akiwa na uzito mdogo sana.Endapo mjamzito atatokwa na damu nyingi sana ukeni kabla ya kujifungua au baada ya kujifungua anaweza kuishiwa nguvu kabisa, kuzimia au hata kupoteza maisha.
Nini hufanyika baada ya kuishiwa damu?
Mgonjwa hukaguliwa haraka na kujua chanzo cha tatizo lake na kuzuia utokaji wa damu zaidi, huku wakizuia asizimie/kupoteza fahamu kwa kumpatia huduma stahiki ikiwa ni pamoja  kurejesha kiwango cha maji yaliyopungua mwilini haraka sana kwa maji ya drip, wakati jitihada za kutafuta kumwongeza damu zinaendelea.
Wapi watakiwa kwenda kuchangia damu?
Nchini Tanzania, sehemu za kuchangia damu zimegawanyika kikanda kama ifuatavyo :-

(a) Kanda ya Mashariki; inayohudumia mikoa ya Dar es salaam, Morogoro, Dodoma & Pwani. Ofisi kuu za kanda zikiwa Mchikichini, Ilala, Dar es salaam. Simu ni 0715339282.
(b) Kanda ya Ziwa; inayohudumia mikoa ya Mwanza, Mara, Kagera & Shinyanga. Ofisi kuu za kanda zikiwa Mwanza karibu na Hospitali ya Bugando. Simu ni 0768479381.
(c) Kanda ya Magharibi; inayohudumia mikoa ya Tabora, Kigoma & Singida. Ofisi kuu za kanda zikiwa Tabora karibu na Hospitali ya Kitete. Simu ni 0785733606.
(d) Kanda ya Kusini; inayohudumia mikoa ya Lindi & Mtwara. Ofisi kuu za kanda zikiwa Mtwara karibu na Hospitali ya Ligula. Simu ni0786852051.
(e) Kanda ya Kaskazini; inayohudumia mikoa ya Kilimanjaro, Tanga, Arusha & Manyara. Ofisi kuu za kanda zikiwa Moshi, Kilimanjaro karibu na Hospitali ya KCMC. Simu ni 0716231406.
(f) Kanda ya nyanda za juu Kusini; inayohudumia mikoa ya Mbeya, Iringa & Songea. Ofisi kuu za kanda zikiwa Mbeya karibu na Hospitali ya Meta. Simu ni 0767502430.

Mawali na majibu zaidi juu ya Uchangiaji damu
Swali : Nitalipwa nikichangia damu?
Jibu : Hapana. Hakuna malipo baada ya kuchangia damu. Wachangiaji hutoa damu kwa kujitolea kwa hiari yao.
Swali : Je, ni salama kwa mjamzito kuchangiwa damu?
Jibu : Ni salama kwa kuwa vigezo vyote vya usalama huchukuliwa kwa uzito.
Swali : Je, ni kweli kuwa kila kundi la mchangia damu lazima liwe sawa na mjamzito anayechangiwa?
Jibu : Kwa kawaida damu ya mchangiaji hukusanywa bila kujali ni kundi gani, endapo mjamzito atahitaji kutiwa damu ndipo kundi la damu ya mchangiaji litatafutwa ili kuendana na kundi la mjamzito.
Swali : Kuna faida gani kuchangia damu?
Jibu : Kuokoa maisha, kufahamu kundi lako la damu, kufahamu hali yako ya maambukizi ya magonjwa kama UKIMWI, Kaswende na Mchochota wa aina B & C, pia ni uzalendo.
Swali : Kuna hasara gani anayopata mchangia damu tokana na kuchangia damu?
Jibu : Hakuna hasara anayopata mchangiaji damu kwa kuwa damu atakayochangia itatumika kuokoa maisha ya wenye uhitaji wa damu.
Swali : Je, damu huuzwa kwa wanaohitaji?
Jibu : Hapana, damu haiuzwi na hutolewa bure kwa anaehitaji
Swali : Ni kina nani watakaopata damu niliyochangia?
Jibu : Watu wenye upungufu wa damu hasa watoto, watu waliofanyiwa upasuaji mkubwa, wagonjwa wenye saratani, majeruhi wa ajari na kina mama wajawazito wenye matatizo ya uzazi kama kutokwa damu nyingi baada ya kujifungua.
Swali : Ni magonjwa gani yanaweza kusambazwa kwa njia ya damu?
Jibu : Magonjwa mengi husambazwa kwa njia ya damu kama UKIMWI, Kaswende & Mchochota wa aina B & C na bacteria.
Swali : Je, unaweza kupata maambukizi ya UKIMWI ukichangia damu?
Jibu : Hapana kabisa. Sindano na vifaa vingine vyenye ncha kali vinavyotumika ni safi & salama. Watumishi wa ukusanyaji damu wanafuata viwango vya usalama na kuzuia maambukizi kama walivyofundishwa.
Swali : Je, ni salama kuchangia damu?
Jibu : Ndiyo, ni salama kuchangia damu kwa kuwa kabla ya kuchangia damu mtu hukaguliwa na kuulizwa maswali kuona kama amekidhi vigezo vya kuchangia damu ikiwa ni pamoja na kuangaliwa wingi wa damu na kupimwa shinikizo la damu.
Swali : Ninaweza kuchangia damu ikiwa sijala?
Jibu : Ukichangia damu hujala unaongeza hatari ya kupata matatizo baada ya kuhangia damu, hivyo inashauriwa kula chakula chepesi ndani ya masaa 4 baada ya kuchangia damu.
Swali : Ni damu kiasi gani huchukuliwa kwa wakati mmoja?
Jibu : Ni kiasi cha Mililita 480 za damu ndio kiwango kinachokubaliwa kisheria.
Swali : Ninaweza kutoa damu kila baada ya muda gani?
Jibu : Unaruhusiwa kuchangia damu kila baada ya siku 52 ili kuhakikisha mwili umepata muda wa kutosha kurudisha chembechembe za damu zilizopotea baada ya kuchangia damu wakati uliopita.
Swali : Ninahitaji kula mlo maalumu baada ya kuchangia damu?
Jibu : Hapana, endelea na mlo wako wa kila siku pia unaweza kuhakikisha ni mlo kamili tu.
Swali : Itachukua muda gani kwa mwili kurudisha kiwango cha damu nilichokitoa?
Jibu : Sehemu ya maji (Plasma) ya damu huweza kuridi ndani ya masaa 24 wakati chembechembe za damu hurudi baada ya wiki mbili.
Swali : Je, damu yangu itapimwa magonjwa kama UKIMWI kabla sijatoa?
Jibu : Hapana, hutolazimika kupima UKIMWI kama hauko tayari kufanya hivyo.
Swali : Damu salama ni nini?
Jibu : Damu salama ni  ile imepimwa na kuonekana haina UKIMWI, Kaswende, Mchochota wa aina B & C wala vimelea vya bacteria.
Swali : Nitapata wapi majibu yangu ya vipimo nilivyofanya wakati wa uchangiaji damu?
Jibu : Utapata majibu katika ofisi za damu salama  zilizo karibu nawe au pale ulipochangia damu.
Swali : Nani anaruhusiwa kumchangia damu mama mjamzito?
Jibu : Mtu yoyote mwanamke au mwanaume anaweza kumchangia damu mama mjamzito ikiwa ana afya njema na anajisikia vizuri, umri kati ya miaka 18 hadi 65, uzito usiopungua kilo 50, wingi wa damu zaidi ya gramu 12 kwa desilita, kutokuwa na shinikizo la juu la damu na kwa mwanamke asiwe mjamzito au anayenyonyesha.

No comments

Powered by Blogger.