WATANZANIA TEKNOLOJIA INATUPELEKA WAPI HAKUNA HATA STAHA YA UBINADAMU

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Kwenu Watanzania wenzangu popote pale  mlipo. Bila shaka kila mmoja wetu anaendelea na majukumu yake ya kila siku kuhakikisha mkono unaenda kinywani.
Binafsi mimi ni mzima wa afya. Naendelea na majukumu ya kila siku likiwemo hili la kuwaandikia barua.
Madhumuni ya kuwakumbuka Watanzania wenzangu leo ni kuhusu maendeleo ya teknolojia hususani suala zima la mitandao ya kijamii na simu hizi za kisasa.

Ndugu zangu, nimelazimika kuwakumbusha suala hili sababu hali sasa imekuwa mbaya. Busara haipo, utamaduni na maadili ya Mtanzania yanazidi kuporomoka, hakuna staha tena ya kibinadamu. Tumefika hatua sasa, mtu anaona tukio ambalo kwa kawaida linapaswa kustiriwa lakini yeye anaamua kuliposti katika mitandao ya kijamii, anawatumia rafiki zake kupitia simu ya mkononi.
Mtu anaona tukio liwe ni la ajali, watu wamefariki kwa kuharibika vibaya miili yao, pasipo kutumia busara anaziposti picha hizo katika mitandao ya kijamii sambamba na kuwatumia marafiki zake, jamani hivi kweli huu ni uungwana?
Nazungumza hivi sababu juzi tumeona kwenye tukio la kifo cha Mbunge wa Mbinga Magharibi (CCM), John Damiano Komba. Sekunde kadhaa tu baada ya kifo chake, picha ya mwili wake ilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Mbaya zaidi picha hiyo haikuwa na staha hata kidogo. Chukulia kama yule angekuwa ni baba yako, ungeweza kuisambaza picha ya namna hiyo? Kama huwezi kwa nini uisambaze ya mzazi wa  mwenzako? Hii siyo sawa.
ENDELEA KUSOMA MAKALA HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI

Kinachonisikitisha zaidi, mbali na kuweka picha hizo ambazo si za kistaarabu, bado wengine wamekuwa wakisindikiza na maneno ya kejeli. Tunamkejeli marehemu kweli? Tuna uhakika kwamba sisi ni wasafi? Tuna uhakika wa kuishi milele? Tubadilike.
Ni wakati sasa wa watu kubadilika. Kuheshimu staha ya ubinadamu, desturi zetu zinatufundisha kutokejeli maiti, basi tusifanye hivyo hata kama mhusika ana  mapungufu yake, tusihukumu  maana kazi hiyo si yetu bali ni ya Mwenyezi Mungu.
Umeona tukio, toa taarifa kwa wenzako na si kuweka picha ambazo hazina staha. Katika hili, serikali kupitia Wizara ya Sayansi na Teknolojia, ianze kudhibiti vitendo hivi kwani naamini inawezekana, kwani mifano ipo mingi tu, kuna nchi nyingi duniani wamefanikiwa kudhibiti matumizi ya mitandao ya kijamii.
Mtu huwezi tu kukurupuka na kuposti picha mbaya na serikali ikakuachia. Inakusaka na kukutia hatiani. Baadhi ya vyombo vya habari (siyo Global Publishers Ltd) pia vimekuwa vikifanya makosa ya aina hiyo, vibadilike.
Siku zote tusimamie weledi wa habari. Kamwe tusichapishe picha za watu ambao hazina staha au hazipendezi kuonwa hadharani.Ni matumaini yangu mwenye masikio amesikia, tubadilike. Tuongozwe na busara katika maisha yetu.

No comments

Powered by Blogger.