Ndugu Wananchi;
Naomba nianze kwa kumshukuru
Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na kunipa fursa ya kuzungumza nanyi
kwa kupitia utaratibu wetu huu mzuri wa kila mwisho wa mwezi. Leo
ninayo mambo matatu ninayopenda kuzungumza nanyi.
Ziara ya Rais wa China Nchini Tanzania
Ndugu wananchi;
Jambo la kwanza ni ziara ya
Mheshimiwa Xi Jinping, Rais wa Jamhuri ya Watu wa China aliyoifanya
nchini kwetu kati ya tarehe 24 na 25 Machi, 2013. Lengo la ziara yake
ilikuwa kuimarisha uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya China na
Tanzania. Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wakazi wa Dar es
Salaam kwa kumpokea vizuri mgeni wetu na ujumbe wake. Wameondoka wakiwa
na kumbukumbu nzuri ya nchi yetu na watu wake.
Kwa niaba yenu, nimepokea salamu
za shukrani kutoka kwa Rais Xi Jinping akielezea kufurahishwa na
mapokezi mazuri tuliyowapatia. Naomba tuendelee kuonesha moyo wa upendo
na ukarimu kwa wageni wetu wengine mashuhuri watakaotutembelea siku za
usoni.
Ndugu wananchi;
Nami pia, nimemshukuru sana
Mheshimiwa Xi Jinping kwa kukubali mwaliko wangu na kufanya ziara ya
kihistoria na yenye mafanikio makubwa kwa nchi yetu. Ameifanyia nchi
yetu jambo la heshima kubwa na kumbukumbu isiyosahaulika. Tanzania
imekuwa nchi ya kwanza Barani Afrika kuitembelea, tena siku kumi tu
baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa nchi yake. Na, kubwa zaidi ni kutumia
fursa ya ziara yake hapa nchini kutangazia dunia Sera ya China kwa
Afrika katika kipindi cha uongozi wake.
Tumefarijika sana kusikia kuwa
uhusiano na Afrika bado unapewa kipaumbele cha juu na viongozi wapya wa
China. Pia, kuwa China itaendelea kukuza biashara na uwekezaji na
kuongeza misaada ya maendeleo kwa Afrika ikiwemo kutoa nafasi 18,000 za
mafunzo kwa vijana wa Kiafrika. Kama mtakumbuka nchi zetu mbili
zilitiliana saini mikataka 16 ya ushirikiano katika nyanja mbalimbali.
Misaada ya maendekeo kwa maeneo yetu ya kipaumbele nayo imejumuishwa.
Ndugu Wananchi;
Rais Xi Jinping alielezea na
kusisitiza dhamira yake na ya Serikali na Chama cha Kikomunisti cha
China ya kudumisha na kukuza uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na
China. Kama mjuavyo uhusiano huo ulianzishwa mwaka 1964 na waasisi wa
nchi zetu, yaani Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyekuwa Rais wa
kwanza wa Tanzania na Mwenyekiti Mao Zedong aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa
China na Waziri Mkuu wake Chou En Lai.
Rais wa China aliahidi kuwa nchi
yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika medani ya kimataifa na
kuchangia katika jitihada zetu za kujiletea maendeleo kwa kuongeza
misaada ya maendeleo. Katika miaka 49 ya uhusiano na ushirikiano na
China nchi yetu imepata misaada mingi ya maendeleo ikiwemo Ukumbi wa
Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere ambao ulizinduliwa na Rais Xi
Jinping wakati wa ziara yake.
Ndugu wananchi;
Kuna miradi kadhaa mikubwa
inayoendelea kutekelezwa nchini, Bara na Zanzibar, kwa msaada wa
Serikali ya China. Wakati wa ziara yake, Rais Xi Jinping iliahidi
kuendelea kutusaidia miradi mingine ya maendeleo kama tulivyoomba wakati
wa mazungumzo yetu licha ya ile ambayo ilitiwa saini siku ile.
Ajali ya Kuporomoka Jengo la Ghorofa
Jijini Dar es Salaam
Ndugu Wananchi;
Jambo la pili ninalotaka
kuzungumzia ni ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa 16 lililokuwa
linajengwa katika jiji la Dar es Salaam. Ajali hiyo iliyotokea juzi
tarehe 29 Machi, 2013 imeleta msiba na simanzi kubwa nchini. Mpaka sasa
maiti za ndugu zetu 30 zimepatikana. Watu 17 waliweza kuokolewa, wanne
kati yao bado wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili. Wengine walitibiwa na kuruhusiwa. Kazi ya kufukua eneo la
ajali inaendelea na sasa inakaribia kufikia ukingoni.
Ndugu Wananchi;
Mimi na viongozi wenzangu tulipata
nafasi ya kwenda kuangalia eneo la ajali. Hali niliyoiona pale
imenihuzunisha sana. Lazima nikiri, hata hivyo, kwamba nimeridhishwa
sana na juhudi kubwa za uokoaji zilizokuwa zinafanywa na wanajeshi wetu
wakishirikiana na taasisi, mashirika binafsi na wananchi. Napenda
kutumia nafasi kutoa shukrani maalum kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Ndugu Saidi Meck Sadick kwa uongozi wake madhubuti. Pia nampongeza Mkuu
wa Wilaya ya Ilala, Ndugu Raymond Mushi, na Kamanda wa Polisi Kanda
Maalum ya Dar es Salaam, Ndugu Suleiman Kova pamoja na Maafisa na askari
wa JWTZ, na wale wote walioshiriki na wanaoendelea kushiriki katika
juhudi za uokoaji.
Nawapongeza pia madaktari na
wauguzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na hospitali nyinginezo kwa
jitihada zao za kuokoa maisha ya waliojeruhiwa. Nawapa pole wale wote
waliofiwa na wapendwa, ndugu na jamaa zao katika ajali hii. Nawaomba
wawe na moyo wa subira huku sote tukiungana nao kuwaombea marehemu wetu
wapate mapumziko mema peponi. Kwa waliojeruhiwa, tunawaombea wapone
upesi.
Ndugu Wananchi;
Maneno mengi yanasemwa kuhusu
chanzo cha ajali ile. Alimradi kila mtu ana dhana yake. Niliagiza
vyombo na mamlaka husika wachukue hatua zipasazo kuchunguza sababu za
ghorofa hilo kuanguka na watakaothibitika kusababisha maafa hayo
wachukuliwe hatua zipasazo. Wa kushtakiwa Mahakamani washitakiwe na wa
kufutiwa leseni za kufanya shughuli za ujenzi au taaluma zao wafutiwe
bila ajizi. Jambo la msingi la kusisitiza ni kuwa mamlaka zinazohusika
na usimamizi wa ujenzi lazima zitimize ipasavyo wajibu wake. Naamini
kama mamlaka hizo zingetimiza ipasavyo wajibu wake ajali hii
ingeepukika. Halmashauri za miji na wilaya zina wajibu maalum kwenye
ujenzi katika maeneo yao. Watimize wajibu wao. Yaliyotokea Dar es
Salaam yawe fundisho kwa wote.
Ndugu Wananchi;
Ni matumaini yangu kuwa Bodi ya
Usajili wa Wakandarasi na Bodi ya Usajili wa Wahandisi itakamilisha
mapema uchunguzi wake ili ukweli ujulikane. Bodi ya Usajili wa
Wasanifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi na Baraza la Taifa la Ujenzi nao
washirikishwe kwa ukamilifu ili ukweli upatikane na hatua stahiki
zichukuliwe. Pia naomba washauri namna bora ya kukomesha ajali za aina
hiyo siku za usoni.
Uhusiano wa Wakristo na Waislamu
Ndugu Wananchi;
Jambo la tatu ninalopenda
kuzungumza nanyi leo ni uhusiano wa Waislamu na Wakristo nchini. Jambo
hili nimeshalizungumzia mara kadhaa siku za nyuma, lakini nalazimika
kulisemea tena kutokana na hali ilivyo sasa. Tumefikia mahali ambapo
kama viongozi na waumini wa dini hizi kubwa mbili hawatakubali kubadili
muelekeo wa sasa, tunakoelekea ni kubaya. Nchi yetu nzuri tutaivuruga
na sifa yake ya miaka mingi ya Waislamu na Wakristo kuishi pamoja
kidugu, kwa upendo, ushirikiano na kuvumiliana itatoweka. Tanzania
itaacha kuwa kisiwa cha amani na kuingia katika orodha ya nchi zenye
migogoro na hata vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Ndugu Wananchi;
Nyaraka na kauli kali kali
zinazotolewa na viongozi wa dini za Kikristo na Kiislamu zinanishawishi
kuamini haya niyasemayo. Nyaraka na kauli hizo zina mambo mawili
makuu. Kwanza, kwamba kila upande unatuhumu, kushutumu na kulaumu
upande mwingine kwa kufanya vitendo viovu dhidi ya dini yake. Kauli na
mihadhara ya kudhalilisha dini za wengine, kunajisi vitabu vitakatifu,
kuchoma moto nyumba za ibada, mzozo kuhusu nani achinje na kuuawa kwa
viongozi wa dini ni baadhi ya mambo yanayotolewa mifano.
Na, pili kwamba kila upande
unailamu Serikali kwa kupendelea upande mwingine. Wakristo wanalaumu
kwamba mihadhara ya kudhalilisha Ukristo inaendeshwa na Serikali
haichukui hatua. Aidha, Wakristo wanateswa na viongozi wao kuuawa na
Waislamu, lakini Serikali haichukui hatua. Kwa ajili hiyo wanadai kuwa
Serikali imeshindwa kulinda uhai wa raia wake. Wanasema pia kwamba
Serikali inapendelea upande wa Waislamu.
Ndugu Wananchi;
Waislamu nao wanadai kuwa kitabu
chao kitakatifu, yaani Quran Tukufu, kinadhalilishwa kwa kuchanwa,
kuchomwa moto na kukojolewa na Wakristo na Serikali haichukui hatua yo
yote ya maana. Waislamu wananyanyaswa katika nchi yao, wanakamatwa ovyo,
hawapewi fursa sawa na kwamba Serikali inawapendelea Wakristo.
Wanasema nchi inaendeshwa kwa mfumo wa Kikristo. Mimi binafsi
wananishutumu kuwa napendelea kushiriki zaidi kwenye shughuli za
Wakristo kuliko za Waislamu kama vile harambee za kujenga Makanisa na
shule za Makanisa. Naambiwa kuwa mwepesi kushiriki maziko ya Maaskofu
kuliko Masheikh wanapofariki. Ipo Misikiti mitatu hapa Dar es Salaam
wamenisomea itikafu nife. Katika itikafu hiyo wamewajumuisha Inspekta
Jenerali wa Polisi, Said Mwema na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya
Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Ndugu Suleiman Kova.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuwahakikishia Watanzania
wenzangu kuwa mimi na Serikali ninayoiongoza, hatupendelei upande wo
wote. Hatufurahishwi na kitendo cha mtu kudhalilisha dini ya mwenzake
ndiyo maana wapo wahadhiri wa dini ya Kiislamu na wahubiri wa dini ya
Kikristo wamekamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa nyakati mbalimbali.
Vyombo vya usalama vinatambua wajibu wake huo na kama haifanyiki ni
ulegevu wa mtu tu katika kutimiza wajibu wao na siyo kwamba ni sera na
maelekezo yangu au ya Serikali. Mtakumbuka kuwa mara kadhaa
nimewakumbusha Wakuu wa Mikoa na Wilaya na wakuu wa vyombo vya usalama
kuacha ajizi katika kutimiza wajibu wao kwenye suala hili.
Ndugu Wananchi;
Mimi binafsi sibagui, hushiriki
shughuli za Waislamu na Wakristo kila ninapoalikwa labda nikose nafasi
kwa sababu nyinginezo. Nimeshafanya shughuli nyingi za Waislamu kama
vile Maulid ya Mtume Muhamad S.A.W., safari za Hija, ujenzi wa misikiti
na madrasa na mengineyo mengi. Nimeshashiriki mazishi ya Masheikh kama
nifanyavyo kwa Maaskofu na watu mbalimbali Waislamu na Wakristo. Pale
ambapo sikushiriki mazishi ya Sheikh au Askofu itakuwa ni kwa sababu ya
kubanwa na shughuli nyingine ambazo lazima nifanye mimi, au taarifa
ilikuwa ya muda mfupi. Kwa upande wa Waislamu desturi yetu ya kuzika
mara mtu anapofariki huwa kikwazo kwangu kushiriki hasa ikiwa ni nje ya
Dar es Salaam kwa sababu ya taratibu za kumsafirisha Rais kutoka mahali
pamoja kwenda pengine siyo nyepesi. Wakristo hawana utaratibu huo,
huwa wanaweza kusubiri hivyo huniwia rahisi kushiriki.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuwahakikishia kuwa
Serikali yetu haijashindwa kulinda usalama wa raia wake au viongozi wa
dini na nyumba za ibada. Kama ingekuwa hivyo, tungeshuhudia mauaji ya
raia, viongozi wa dini na matukio ya kuchomwa nyumba za ibada yakiwa
mengi hapa nchini. Lakini hivyo sivyo. Nawasihi sana ndugu zangu
Wakristo na Waislamu kuwa tusiyachakulie matukio ya kuuawa kwa Mchungaji
Mathayo Kachila kule Buseresere, Geita, na Padri Evaristus Mushi kule
Zanzibar, au kumwagiwa tindikali Sheikh Fadhili Soroga, Naibu Mufti wa
Zanizbar, kupigwa risasi Padri Ambrose Mkenda na kuchomwa moto kwa
Makanisa Zanzibar na Mbagala, Dar es Salaam kuwa ni kielelezo na
ushahidi wa Serikali kushindwa kutimiza wajibu wake.
Kila tukio lina mazingira yake,
hakuna ushahidi wa vyombo vya Serikali kuzembea. Hakuna ushahidi wa
matukio hayo kuunganika. Mpaka sasa hatujapata ushahidi wa kuwepo
kikundi cha Waislamu wanaopanga kuua viongozi wa Kikristo na kuchoma
moto Makanisa hapa nchini.
Ndugu Wananchi;
Kifo cha Mchungaji Mathayo Kachila
wa Buseresere ni matokeo ya vurugu zilizosababishwa na mzozo kati ya
Wakristo na Waislamu kuhusu kama nyama iliyochinjwa na Wakristo Kanisani
nayo iuzwe kwenye bucha iliyopo pale kijijini ambayo kwa mazoea huuzwa
nyama iliyochinjwa na Waislamu. Katika ugomvi na vurumai hizo ndipo
watu kadhaa wa pande zote walijeruhiwa na Mchungaji kupoteza maisha. Si
tukio unaloweza kulihusisha na mengineyo nchini. Ni la pale pale
Buseresere na limeanzishwa na kuhusisha Wakristo na Waislamu wa
Buseresere kwa sababu zao.
Hivi kama kusingekuwepo na mzozo
wa nyama ile kuuzwa katika bucha ile kuumizana kule na mauaji yale
yangetokea? Kabla ya mzozo ule Wakristo na Waislamu wa Buseresere
hawakuwa na ugomvi baina yao. Walikuwa wanaishi kidugu na kushirikiana
katika shughuli zao za kujitafutia riziki huku kila mmoja akimuabudu
Mungu kwa misingi ya dini yake. Hivyo kutumia tukio hilo kutoa wito kwa
Wakristo wote kuwa kuuawa kwa Mchungaji Kachila ni sawa na kuuawa kwa
Wakristo wote nchini kulikofanywa na Waislamu ni kulikuza tatizo
isivyostahili. Busara ituongoze kutafuta njia ya kuwapatanisha Wakristo
na Waislamu wa Buseresere wazungumze, waelewane na waendelee kuishi
pamoja kama ilivyokuwa awali. Hata mzozo wa kuchinja wanaweza
kuumaliza. Mbona bucha za kitimoto zipo na watu hawajapigana. Kutumia
mzozo wa Buseresere kueneza chuki kati ya Wakristo na Waislamu nchi
nzima si sawa. Hatuwatendei haki Watanzania.
Ndugu Wananchi;
Kuuawa kwa Padri Evaristus Mushi
wa Zanzibar ni tukio linalojitegemea halina uhusiano kabisa na lile la
Buseresere, Geita. Hapakuwa na mzozo kuhusu nani achinje. Bado
uchunguzi wake unaendelea na tumehusisha vyombo vya upelelezi vya nje
vishirikiane na vyetu kufanya uchunguzi. Tumefanya hivyo kwa sababu ya
ugumu uliopatikana katika uchunguzi wa matukio ya kabla yake. Yaani ile
la kupigwa risasi na kujeruhiwa kwa Padri Ambrose Mkenda na kumwagiwa
tindikali kwa Naibu Mufti wa Zanzibar Sheikh Fadhili Soroga. Bado
hakuna mafanikio ya kutia moyo. Na bado tunajiuliza kama matukio hayo
matatu yanahusiana. Je, Makanisa kuchomwa moto kule Zanzibar nako kuna
uhusiano wowote na matukio yale matatu? Uchunguzi unaoendelea unaweza
kufumbua fumbo hilo.
Kuna watu wanadhani yanahusiana na
kwa sababu nzuri. Lakini inabaki kuwa ni dhana ya kibinadamu mpaka
ukweli halisi utakapobainika. Bado kazi ya uchunguzi inaendelea
kufanywa na vyombo vya usalama vya nchi yetu wakishirikiana na wenzao wa
nje. Katika mazingira hayo, ni mapema mno kumnyooshea kidole mtu ye
yote na kuilaumu Serikali ya Muungano au Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar. Serikali siyo mshirika katika mauaji hayo, na haina sababu
ya kufanya hivyo. Ndiyo maana tunahangaika usiku na mchana kupata
jawabu.
Ndugu Wananchi;
Hali kadhalika tukio la Makanisa
ya Mbagala, Dar Es Salaam kuvamiwa, kubomolewa, mali kuibiwa na kuchomwa
moto tarehe 12 Oktoba, 2012 nalo lina mazingira yake maalum. Chanzo
chake ni mzozo uliotokana na tukio la kusikitisha la kijana mmoja
Mkristo kukojolea Kitabu Kitakatifu cha Waislamu, yaani Quran Tukufu.
Pamoja na maelezo kuwa walikuwa na ubishi wa kitoto na kijana mwenzake,
lakini kitendo hicho kiliwakasirisha Waislamu. Kijana huyo alifikishwa
kituo cha Polisi. Baadhi ya Waislamu wenye msimamo mkali walifika
kituoni hapo wakidai wapewe huyo kijana wamuadhibu wao. Jeshi la Polisi
lilikataa. Kukatokea mzozo kati ya waumini hao na Polisi na baada ya
kushindwa walichokitaka baadhi yao walipotoka pale, wakaenda kufanya
uhalifu wa kuvunja, kuiba na kuchoma moto Makanisa.
Ndugu Wananchi;
Baada ya tukio la Mbagala
hapajakuwepo na tukio la kuchomwa Kanisa mahali popote kwa upande wa
Bara. Aidha, hapajawahi kuwepo tishio lililothibitika la watu kutaka
kuchoma Kanisa popote. Lakini maneno ya vitisho vya kuchoma Makanisa
yako mengi hasa kupitia mitandao ya simu za mkononi. Kila ujumbe wa
namna hiyo ulipofikishwa kwenye vyombo vya usalama uchunguzi umefanywa
na hata hatua za tahadhari kuchukuliwa lakini hakuna hata taarifa moja
iliyothibitika kuwa na chembe ya ukweli. Hata dalili hazijakuwepo.
Tulichojifunza ni kuwa ujumbe na
vitisho vya aina mbalimbali hupelekwa kote, kwa Wakristo na Waislamu.
Upo unaowalenga Wakristo ukiwaambia wenzao Waislamu wanapanga
kuwadhuru. Na upo wanaopelekewa Waislamu wakiambiwa Wakristo wanao
mipango mibaya dhidi yao. Watanzania wenzangu nawaomba mtanabahi na
mjue kuwa wapo watu wanacheza mchezo mchafu wa kuwagonganisha na kutaka
kuwagombanisha Wakristo na Waislamu kwa sababu wanazozijua wao na kwa
faida yao. Wanapandikiza chuki kwa lengo la kutaka Wakristo na Waislamu
wagombane. Wanapandikiza chuki baina ya Serikali na waumini wa dini
zetu kuu mbili ili ionekane Serikali imewatelekeza raia wake. Ni mchezo
mbaya, tusikubali kucheza ngoma tusiyoijua. Hivi ndugu zangu mmekaa
chini na kujiuliza kumetokea nini kipya hata leo kuwa na mhemko kama huu
kati ya Wakristo na Waislamu na kutishia kuleta vita baina nchini kote?
Ndugu Wananchi;
Serikali haijapuuzia kila
palipotokea matukio ya uhalifu. Watu 76 wanaotuhumiwa kuharibu na
kuchoma moto Makanisa kule Mbagala na kufanya fujo kituo cha Polisi
wamekamatwa na kesi zao zinaendelea Mahakamani. Kwa upande wa tukio la
Buseresere lililosababisha kifo cha Mchungaji Mathayo Kachila, watu 17,
wakiwemo waumini wa dini ya Kikristo na Kiislamu walikamatwa na kesi zao
zinaendelea. Wapo walioshitakiwa kwa mauaji na wapo walioshitakiwa kwa
kufanya vurugu. Jeshi la Polisi bado linawatafuta watu wengine
waliohusika na uhalifu huo ili na wao wakamatwe. Kwa upande wa Zanzibar,
watu 10 wanaotuhumiwa kuchoma Makanisa wamekamatwa na kesi zao
zinaendelea. Bado hajakamatwa mtu kwa tukio la mwisho la kuchoma Kanisa
baada ya kuuawa Padri Evaristus Mushi. Uchunguzi unaendelea.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa kujeruhiwa kwa Padre
Mkenda, bado uchunguzi haujakamilika pamoja na kuwapo taarifa kadhaa
zinazoendelea kufanyiwa kazi. Kuhusu uchunguzi wa mauaji ya Padre
Mushi, baada ya jitihada kubwa kufanyika ikiwa ni pamoja na kushirikisha
nchi zilizobobea katika uchunguzi wa makosa ya aina hii, hatua ya kutia
moyo imefikiwa. Mtu mmoja amekamatwa na wengine wanaendelea
kutafutwa.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa kanda na vituo vya
redio nako pia Serikali imechukua hatua. Watu kadhaa wamekamatwa na
kufikishwa Mahakamani katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwa kurekodi
na kusambaza kanda zinazochochea chuki na vurugu za kidini. Wapo
Waislamu na Wakristo. Wapo watu wengine ambao wanaendelea kutafutwa.
Zipo taarifa kuwa baadhi yao wamekimbilia nchi za nje. Jeshi la Polisi
limeomba msaada wa Polisi wa Kimataifa, yaani Interpol, kusaidia
kuwatafuta na kuwarejesha nchini. Vituo viwili vya radio yaani Kwa
Neema FM cha Sengereme na Radio Imani cha Morogoro vimefungiwa kwa muda
wa miezi sita. Baada ya muda huo kupita, Kamati ya Maudhui ya Mamlaka
ya Mawasiliano itaamua ipasavyo.
Ndugu Wananchi;
Nimeyaeleza haya kwa kirefu
kuwahakikishia kuwa Serikali inajali usalama wa raia wake wa mali zao na
amani na utulivu wa nchi yetu. Kamwe hatujashindwa kulinda raia wa
nchi wa yetu na yapo mambo mengi yaliyofanyika na yanayoendelea
kufanyika kuhakikisha kuwa Watanzania wa dini zote, makabila yote, rangi
zote na mahali po pote walipo wako salama. Tunataka kuona watu
wanaendelea kuishi kwa amani, upendo, ushirikiano na mshikamano kama
tulivyokuwa tunaishi siku zote. Tunapenda kuona Watanzania wanaepuka
mambo yanayowabagua na kusisitiza yale yanayowaunganisha. Tujiepushe
kuyapa kipaumbele yale yanayotugawa.
Ndugu Wananchi;
Athari za mzozo kuhusu kuchinja
kule Geita iwe fundisho kwetu sote. Tuazimie sote kuwa yaliyopita si
ndwele, tugange yajayo. Hebu tufikirie maisha yetu Watanzania
yatakuwaje kwenye shughuli za kijamii kama vile sherehe, harusi, ngoma
na misiba iwapo tutaanza kuwa na chakula tofauti kwa Waislamu na
Wakristo. Fikiria itakuwaje kwenye hospitali, shule na vyuo pawe na
majiko mawili au labda hata mabwalo mawili ya chakula kwa Waislamu na
Wakristo. Jeshini nako kuwe na majiko na mabwalo ya Waislamu na
Wakristo. Hali iwe hivyo hivyo kwenye migahawa na maeneo mengine yenye
huduma ya chakula.
Ndugu zangu, tunataka kuipeleka
wapi nchi yetu? Tunataka kujenga nchi ya namna gani? Mimi naamini
tukifanya hivyo huo utakuwa ndiyo mwanzo wa kubaguana kwa kila kitu na
kila jambo na kuligawa taifa kwa namna ambayo hatutakuwa wamoja tena.
Huko tunakoelekea siko, ni kubaya. Tubadilike, na wakati ni huu.
Viongozi wa dini waongoze njia wawaepushe waumini wao na taifa letu na
janga hili.
Ndugu Wananchi;
Bado narudia kusisitiza umuhimu wa
viongozi wa dini zetu kubwa mbili kukutana na kuizungumzia hali hii na
kuipatia ufumbuzi. Ni wao kuliko mtu mwingine ye yote wenye majawabu ya
matatizo haya. Ni masuala yanayohusu imani za dini na yanafanywa na
viongozi wa dini na wafuasi wao kwa jina la dini zao. Serikali ina
wajibu wa kulinda amani. Kazi yetu itakuwa rahisi kama waumini
hawatafanya vitendo vitakavyosababisha uvunjifu wa amani. Wa kuongoza
waumini lipi jema na lipi baya ni viongozi wa dini.
Ndugu Wananchi;
Nimeshakutana na viongozi kadhaa
wa madhehebu na taasisi za dini za Kikristo na Kiislamu kuzungumza nao
kuhusu jambo hilo. Nimepata faraja kuona kuwa wote wanasikitishwa na
mambo yanayotokea hivi sasa na wameona busara ya viongozi wa dini
kuzungumza ili kuondoa tofauti zilizojitokeza. Wanakiri kuwa hali
ilivyo sasa siyo ya kawaida kwa Tanzania na Watanzania. Kuna upepo
mbaya wa shetani unapita ambao viongozi wa dini wana wajibu wa
kuhakikisha kuwa hali ya hewa inasafishwa na kurejesha nchi yetu na watu
wake katika maisha tuliyoyazoea. Maisha ambayo waumini wa dini tofauti
wanaishi pamoja kwa udugu, upendo, ushirikiano na mshikamano kwa
misingi ya ubinadamu wao na Utanzania wao.
Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo
Pinda, ameshaeleza dhamira ya Serikali ya kuitisha mkutano wa viongozi
wa dini mapema mwezi ujao. Ni matumaini yangu kuwa wote watashiriki
wenyewe bila ya kutuma wawakilishi. Lazima tupate jawabu kwa maslahi ya
taifa letu na watu wake.
Ndugu Wananchi;
Kabla ya kumaliza hotuba yangu
napenda kutumia nafasi hii kuwaomba na kuwasihi waandishi wa habari
wasaidie kuliepusha taifa letu kuingia katika vita vya kidini. Waache
kushabikia taarifa zinazochochea na kujenga uhasama baina ya waumini wa
dini zetu. Nawaomba wapime athari za taarifa zao kabla ya kuziandika au
kuzitangaza. Wawe makini na maneno wanayotumia. Katika hali
tuliyonayo sasa lazima sote tuazimie kuondoa tofauti za kidini na
kujenga umoja miongoni mwa Watanzania wa dini zote. Wasipofanya hivyo,
wataliingiza taifa katika mgogoro mkubwa ambao hauna msingi kama
ilivyotokea katika nchi jirani. Nawaomba wamiliki wa vyombo vya habari
kutambua kuwa wanao wajibu wa kuhakikisha vyombo vyao havitumiki kuleta
mifarakano kwa kuchochea uhasama baina ya Wakristo na Waislamu.
Hitimisho
Ndugu Wananchi;
Naomba kumaliza kuwa kusisitiza
kuwa wananchi wote kudumisha umoja na mshikamano wetu. Tuishi kwa
upendo, umoja, mshikamano na ushirikiano bila kujali tofauti ya dini
zetu, kabila, rangi au mahali atokako mtu. Hizo ndizo tunu za taifa
letu la Tanzania ambazo hatuna budi kuzienzi, kuzilinda na kuzidumisha.
Narudia kuwahakikishia kuwa Serikali haipendelei dini yo yote na wala
haina mpango wa kushiriki kuangamiza dini yo yote au waumini wao.
Serikali kupitia vyombo vyake vya usalama itaendelea kuhakikisha ulinzi
na usalama wa raia wake na mali zao kama inavyofanya siku zote. Kama
kuna mtu anaona kuwa maisha yake au mali zake zipo hatarini, aende kutoa
taarifa Polisi. Hatua zipasazo zitachukuliwa.
Ndugu Wananchi;
Mwisho nawatakia sikukuu njema ya Pasaka. Tusherehekee kwa amani na utulivu. Tusherehekee pamoja.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa Kunisikiliza.



No comments:
Post a Comment