Dar es Salaam. Siku moja baada ya gazeti hili kuchapisha habari juu ya Serikali kuchelewa kutangaza wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ualimu, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imesema majina hayo yatatangazwa leo.
Msemaji wa wizara hiyo, Bunyanzu Ntambi alisema jana kuwa, majina hayo yatatangazwa leo shughuli itakayofanyika katika ofisi za wizara hiyo.
“Kesho (leo) saa nne, selected (waliochaguliwa) watatangazwa,” alisema Ntambi.
Awali Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo alisema majina ya wanafunzi hao yatatangazwa siku yoyote ndani ya juma hili.
Jana gazeti hili lilichapisha habari juu ya Serikali kuchelewa kutangaza majina hayo, tofauti na miaka mingine, ambapo wanaochaguliwa kujiunga na kidato cha tano hutangazwa mapema na kuwasili shule kabla wenzao wa kidato cha sita hawajafungua.
Endelea kusoma habari hii kwa kubofya hapa chini
Mulugo jana alisema majina hayo hayajachelewa kutangazwa na kwamba wanafunzi wa kidato cha sita hufungua wiki ya tatu ya Julai na kwamba hata sasa bado hawajafungua.
“Matokeo tutayatoa wiki hii na hatujachelewa kuyatangaza kwa sababu kwa kawaida kidato cha tano na sita wanafungua shule wiki ya tatu Julai , kwa hiyo tukitoa wiki hii tutakuwa hatujachelewa,” alisema Mulugo.
Wakati Mulugo akisema hayo, uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa shule za Serikali zimeshafunguliwa na wanafunzi wa kidato cha sita tayari wamewasili shuleni. Mmoja wa walimu wa Shule ya Sekondari ya Jangwani jijini Dar es Salaam, alisema kuwa kwa kawaida wanafunzi wa kidato cha tano huripoti shuleni wiki mbili kabla ya wale wa kidato cha sita kitu ambacho mwaka huu kimekuwa tofauti.
“Mpaka sasa hatujaambiwa kwa nini hii hali imekuwa hivi, kwa kawaida kidato cha tano huripoti shuleni wiki moja kabla ya kidato cha sita, lakini mpaka sasa waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano bado hawajatangazwa,” alisema Mwalimu huyo.
Wakati majina hayo yakitarajiwa kutangazwa leo, ni dhahiri kuwa shule za Serikali zenye kidato cha tano na sita zitaendelea kupata idadi ndogo ya wanafunzi tofauti na uwezo huku baadhi zisizo za Serikali zikitishia kuachana na biashara ya shule.
Hali hiyo inatokana na idadi kubwa ya wanafunzi kushindwa mtihani wa kidato cha nne, ambapo kwa mwaka 2012 waliofaulu kwa daraja la kwanza mpaka la tatu ni 35,349. Wwanafunzi walio katika nafasi kubwa ya kuchaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha tano ni wale waliofaulu kwa daraja la kwanza mpaka la tatu.
Kwa sasa shule za Serikali zenye kidato cha tano na sita, zina uwezo wa kuchukua wanafunzi 45,000 kwa kidato cha tano.
Kwa hali hiyo, hata kama wanafunzi wote 35,349 waliopata daraja la kwanza mpaka la tatu wakichaguliwa na kuripoti kwenye shule za Serikali, bado shule hizi zitakuwa na upungufu wa zaidi ya wanafunzi 9,000.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment