HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

Lowassa aachiwa kwa dhamana

Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa ameachiwa kwa dhamana baada ya kuhojiwa kwa saa nne katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).
Lowassa ameondoka makao makuu ya polisi saa 8.15 na kuelekea nyumbani kwake.
Akizungumza baada ya mahojiano hayo, Mwanasheria wa Chadema, Peter Kibatala amesema Lowassa amejidhamini mwenyewe na ametakiwa kuripoti tena Alhamisi saa 6.00 mchana.
Kibatala amesema Lowassa amehojiwa kwa kosa la uchochezi na ameandika maelezo ya onyo juu ya kauli aliyoitoa wakati wa futari iliyoandaliwa na mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara.
"Mzee amehojiwa kwa kile wanachokiita kauli ya uchochezi aliyoitoa Juni 23, mwaka huu wakati wa futari iliyoandaliwa na Waitara. Baada ya kuhojiwa ameandika Maelezo ya Onyo na atatakiwa kuripoti tena Alhamisi, Juni 29," amesema.

Chadema wataka Katiba Jaji ya Warioba irejeshwe

Chadema imesema iwapo Tanzania inataka kunufaika na rasilimali zake na kushinda vita vya kutetea utajiri wake inapaswa kwanza kurejesha katiba iliyopendekezwa na Jaji Joseph Warioba na si vinginevyo.
Akitoa msimamo wa chama kutokana na kile kinachoendelea baada ya kutolewa kwa ripoti mbili za Rais kuhusu mchanga wa dhahabu, leo (Ijumaa) Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Vincent Mashinji amesema suluhisho la kudumu katika kulinda na kuhifadhi rasilimali za Taifa ni kurejea katika katiba ya wananchi.
“Chadema tunasema kuwa haya yote tunayoyapigia kelele itakuwa ni kazi bure iwapo haturejeshi hoja ya katiba mpya.
“Katiba ya Warioba iliweka mapendekezo ya jinsi ya kulinda rasilimali za taifa na kama tungefuata hayo yote hili la sasa halingepaswa kuwa na mjadala mkubwa kiasi hiki,” amesema wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya chama hicho Kinondoni.
Pia, chama hicho kimeitaka CCM kujipima na kujitafakari kama kinafaa kuendelea kuaminika kuongoza dola kutokana kushindwa kutetea vyema rasimali za taifa kwa kuruhusu mikataba mibovu.

Waziri Nchemba Ataja Sababu Zinazowafanya CHADEMA Wapigwe Marufuku Kufanya Sherehe Vyuoni

Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa alihoji bungeni sababu za wanafunzi wa CCM kupendelewa kufanya mikutano na sherehe za kumaliza masomo yao huku wanafunzi wa vyama vingine vya upinzani hasa CHADEMA kupigwa marufuku kufanya sherehe hizo.

Akijibu jambo hilo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba alisema kuwa wanafunzi wa Chama Cha Mapinduzi huwa wanafuata utaratibu ndiyo maana huwa wanapewa ruksa kufanya sherehe hizo pindi wanapomaliza vyuo na kusema hao wengine huwa hawafuati utaratibu ndiyo maana wanakuwa wanazuiliwa.

"Taratibu ziko wazi kama CCM walikuwa wamefuata utaratibu na kupewa mikutano, chama kingine chochote kinachotakiwa ni kufuata utaratibu zile zile waweze kupewa mikutano lakini wengine kama hawajafanya utaratibu hawatapewa tu kwa sababu CCM walipewa bali watapewa kwa kufuata utaratibu, kuna sehemu zingine CHASO hao hao wamepewa mikutano kwa hiyo linalotakiwa ni utaratibu tu wa kupewa mikutano hiyo" alisema Mwigulu Nchemba

Mbali na hilo Waziri Mwigulu Nchemba alisema mikutano ya hadhara haijazuiwa bali imewekewa utaratibu na kusema duniani kote sifa za mikutano ya hadhara ni kama ambavyo inafanyika hivi sasa Tanzania na kusema kuwa mtu aliyeshinda ndiye anaendelea na majukumu ya kuongoza na aliyeshindwa hapaswi kushukuru kwa wananchi.

"Marekani mwaka jana walifanya uchaguzi mmemuona Hillary Clinton anashukuru kwa wananchi? Duniani kote aliyeshinda ndiye anaendesha serikali kwa utaratibu wa kiserikali hili liko wazi duniani kote" alisisitiza Mwigulu Nchemba

PICHA: MWILI WA MAREHEMU PHILLEMON NDESAMBURO WAAGWA KATIKA VIWANJA VYA MAJENGO MKOANI KILIMANJARO

Viongozi wa juu wa Chadema, Freeman Mbowe na Edward Lowassa wameupokea mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema, Kilimanjaro, Phillemon Ndesamburo baada ya kuwasili katika viwanja vya Majengo.

Ndesamburo alifariki ghafla wiki iliyopita wakati akipata matibabu katika hospitali ya KCMC.
Mwili wa Ndesamburo ambaye pia aliwahi kuwa mbunge wa Moshi Mjinim,utaagwa katika viwanja hivyo na leo saa kumi jioni utapelekwa nyumbani kwake kwa ajili ya taratibu za mazishi.
Wabunge na Viongozi mbalimbali wa Chadema, akiwamo muasisi wa chama hicho, Edwin Mtei, Frederick Sumaye wapo uwanjani hapo kwa ajili ya kumuaga Ndesamburo.
  Gari lililobeba mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani Kilimanjaro, Phillemon Ndesamburo lilielekea katika viwanja vya Majengo kwa ajili ya kuagwa mwili huo.

Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa akiwapungia mkono wananchi waliofika kwenye uwanja  huo mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Majengo kwa ajili ya kuagwa mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani Kilimanjaro, Marehemu Phillemon Ndesamburo.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe akiwasili atika viwanja vya Majengo kwa ajili ya kuagwa mwili wa  aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani Kilimanjaro, Marehemu Phillemon Ndesamburo.
Wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakiwa wamebeba jeneza lililobeba mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani Kilimanjaro, Marehemu Phillemon Ndesamburo. 
Viongozi mbalimbali wa Kisiasa na dini wakiwa wamesimama mara baada ya mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani Kilimanjaro, Marehemu Phillemon Ndesamburo kuwasili uwanjani hapo



 Baadhi ya wakazi wa mji wa Moshi mkoani Kilimanjaro wakiwa kwenye uzuni mara baada ya mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani Kilimanjaro, Phillemon Ndesamburo ulipokuwa unaelekea katika viwanja vya Majengo kwa ajili ya kuagwa mwili huo. 



  

  

  

Diwani wa Chadema Arusha ajiuzulu

Diwani wa Chadema, kata ya Bangata wilayani Arumeru (Arusha) Emmanuel Mollel amejiuzulu nafasi yake ikiwa ni siku chache baada ya kutuhumiwa na uongozi wa chama hicho kwa utovu wa nidhamu.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meru, Christopher Kazeri amethibitisha taarifa za kujiuzulu kwa diwani huyo na kusema kwamba ofisi yake imepokea taarifa za kujiuzulu kwake.
Mollel alipotafutwa kwa njia ya simu leo, Juni Mosi, 2017, alikiri kuandika barua ya kujiuzulu huku akisema kwamba amefanya uamuzi huo kwa utashi wake binafsi lakini akakanusha kupewa barua yoyote ya onyo na uongozi wa chama hicho.
Katibu wa Chadema mkoani Arusha,Aman Gorugwa amethibitisha taarifa za kujiuzulu kwa kiongozi huyo na kusema kuanzia leo Mollel sio mwanachama wa Chadema tena.
Gorugwa amesema kwamba uongozi wa chama chao ulimwandikia barua hivi karibuni ya kumtaka ajieleze sababu za kutowajibishwa kutokana na tuhuma zinazomkabili.
Ametaja tuhuma hizo kuwa ni pamoja na utovu wa nidhamu,mwenendo usiofaa ,kwenda kinyume na maagizo ya chama na usaliti.

Amesema hata kabla ya kujibu tuhuma hizo walipokea barua ya kujiuzulu kwake.
Katibu huyo amesema kwamba jina la Mollel lilikuwa kwenye orodha ya kitabu cheusi (black book) na alikuwa kwenye hatua za mwisho za kutimuliwa.

Bendera ya CHADEMA Kupeperuka Nusu Mlingoti

Kufuatia kifo cha mmoja wa Waasisi wa CHADEMA, Mzee Philemon Ndesamburo Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA), Dkt. Vincent Mashinji, ametoa maelekezo kwa watendaji nchi nzima kupeperusha bendera nusu mlingoti

Mashinji ametoa maelekezo hayo leo wakati akiongea na Waandishi wa Habari Makao Makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam na kusema bendera zinapaswa kupeperushwa nusu mlingoti hadi mwili wa kiongozi huyo utakapopumzishwa katika nyumba yake ya milele.

"Chama kitashiriki katika msiba huu kwa heshima zote kumuenzi mmoja wa waasisi wa siasa za mabadiliko ya kweli na Uhuru wa kweli nchini, msiba huu ni msiba wa CHADEMA, ni msiba wa Watanzania, ni msiba wa Taifa letu kutokana na mchango mkubwa wa Mzee wetu kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa nchi yetu, Mhe. Ndesamburo ndiye aliyekifadhili Chama kwa mara ya kwanza kwa kukipatia ofisi eneo la Kisutu jijini Dar es salaam" amesema Dkt. Mashinji