HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

SERIKALI YAAGIZA NBAA KUHARAKISHA MABORESHO YA MITAALA KUKIDHI KASI YA TEKNOLOJIA


Serikali imeitaka Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) kuharakisha maboresho ya mitaala na mafunzo ya Uhasibu ili yaendane na kasi ya maendeleo ya teknolojia, hususan matumizi ya akili unde (AI), ambayo yanaendelea kubadili namna kazi mbalimbali zinavyofanyika duniani.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), wakati akihutubia katika Mahafali ya 49 ya NBAA yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha APC-Mbweni, jijini Dar es Salaam.

Mhe. Luswetula alisema dunia inaelekea kwa kasi katika matumizi ya akili unde na kwamba taaluma ya uhasibu haiwezi kubaki nyuma katika mabadiliko hayo, kwa kuwa teknolojia hiyo inaendelea kubadili namna kazi mbalimbali zinavyotekelezwa.

Alisema ni muhimu wataalamu wa uhasibu kuandaliwa mapema ili waweze kutumia teknolojia hiyo kuongeza ufanisi na tija katika utendaji wao, badala ya taaluma hiyo kuachwa nyuma na mabadiliko ya kiteknolojia.

«“Dunia yote inaelekea kwenye matumizi ya akili unde, na NBAA pamoja na wadau wengine muangalie mmejipangaje kukabiliana na mapinduzi haya, hasa kuhakikisha mitaala yetu ya mafunzo imesharekebishwa ili kuendana na mwelekeo wa dunia ya sasa,” alisema Mhe. Luswetula.»

Aidha, Mhe. Luswetula alisisitiza umuhimu wa kuongeza idadi ya wataalamu wa uhasibu na ukaguzi wa hesabu nchini, huku akisisitiza kuwa ongezeko hilo linapaswa kuzingatia ubora, weledi, uaminifu na uadilifu ambao ni misingi muhimu ya taaluma hiyo.

Alisema idadi ya wataalamu wenye sifa katika fani ya uhasibu na ukaguzi wa hesabu bado haitoshelezi mahitaji yaliyopo katika sekta ya umma na binafsi.

Mhe. Luswetula alisema wahasibu na wakaguzi wa hesabu wana nafasi muhimu katika kulinda na kusimamia rasilimali za Taifa, kwa kuwa taaluma hizo ni miongoni mwa nguzo muhimu za uchumi.

Kwa hiyo, alisema wataalamu hao wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia viwango vya juu vya uadilifu, weledi na uaminifu.

“Naitaka NBAA kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kutafuta suluhisho la changamoto ya ukosefu wa mafunzo kwa vitendo kwa wahitimu wa uhasibu, kwa sababu wahitimu wengi wanapata elimu ya nadharia darasani zaidi lakini wanakutana na changamoto wanapoingia katika mazingira halisi ya kazi kutokana na kukosa fursa za kutosha za kujifunza kwa vitendo,” alisema Mhe. Luswetula.

Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na NBAA, ikiwemo kuhakikisha Bodi hiyo inakuwa na watumishi wa kutosha wenye weledi unaohitajika.

Mhe. Luswetula pia aliwapongeza wahitimu wa programu mbalimbali za NBAA, zikiwemo Taaluma ya Juu ya Uhasibu (CPA), Cheti cha Uhasibu (ATEC), CPA Equivalent, Stashahada ya Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu wa Sekta ya Umma (IPSAS), Stashahada ya Kitaalamu katika Ukaguzi wa Ndani (Professional Diploma in Internal Auditing), pamoja na Stashahada ya Kitaalamu katika Utoaji wa Taarifa za Uendelevu (Professional Diploma in Sustainability Reporting).

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NBAA, CPA Prof. Sylvia Temu, alisema Bodi hiyo imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo mbalimbali, huku ikitekeleza Mpango Mkakati wa Miaka Mitano unaoendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Alisema kupitia mpango huo, NBAA inalenga kuhakikisha Tanzania inakuwa na wataalamu wa uhasibu waliobobea wasiopungua 90,000 ifikapo mwaka 2050, sambamba na kuimarisha viwango vya taaluma hiyo kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.

“Kipindi cha mwaka 2025/26, NBAA iliendelea kusimamia mitihani ya kitaaluma, uadilifu wa makampuni yanayofanya shughuli za kihasibu na ukaguzi wa hesabu, pamoja na kutoa mafunzo endelevu kwa wahasibu, wakaguzi, watahiniwa, walimu na wadau wengine,” alisema CPA Prof. Temu.

Alisema NBAA pia imeendelea kuendana na mabadiliko ya mazingira ya biashara na uchumi kwa kuwekeza katika maeneo mapya ya taaluma, ikiwemo masuala ya mazingira, jamii na utawala bora (ESG).

CPA Prof. Temu aliongeza kuwa NBAA imeendelea kushiriki katika taasisi na majukwaa ya kikanda na kimataifa ya taaluma ya uhasibu, ikiwemo International Federation of Accountants (IFAC), Pan Africa Federation of Accountants (PAFA) na Jumuiya ya Professional Accounting Bodies Afrika Mashariki.

Alisema ushiriki huo unalenga kuongeza ushindani wa wataalamu wa Tanzania katika soko la huduma za kitaaluma ndani na nje ya Afrika.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA Prof. Siasa Mzenzi, alisema tangu mwaka 2022, Bodi hiyo imekuwa ikiendesha mahafali mara mbili kwa mwaka kwa lengo la kuwawezesha wahitimu kupata vyeti vyao kwa wakati.

Alisema hatua hiyo inawawezesha wahitimu kutumia sifa walizopata katika kutafuta ajira au kuwasilisha vyeti kwa waajiri wao kwa ajili ya kupandishwa madaraja.

CPA Prof. Mzenzi aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Fedha kwa ushirikiano unaoiwezesha NBAA kutekeleza majukumu yake ya kuimarisha taaluma ya uhasibu na ukaguzi wa hesabu nchini.

“Natoa wito kwa waajiri wa sekta ya umma na binafsi kutumia wataalamu hawa waliohitimu, na tutaendelea kujenga uwezo katika maeneo mapya kama alivyoainisha Mgeni Rasmi ili kuongeza idadi ya wataalamu wa maeneo hayo, hususan Sustainability Reporting,” alisema CPA Prof. Mzenzi.

Mahafali hayo ya 49 yalihusisha jumla ya wahitimu 681 kutoka katika ngazi saba za taaluma, wakiwemo wahitimu wa Cheti cha Waandishi na Utunzaji wa Vitabu vya Hesabu (Accounting Technicians), Taaluma ya Juu ya Uhasibu (CPA), CPA Equivalent, Cheti cha Kitaaluma katika Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu wa Sekta ya Umma (Professional Certificate in IPSAS), Stashahada ya Kitaaluma katika Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu wa Sekta ya Umma (Professional Diploma in IPSAS), Stashahada ya Kitaaluma katika Ukaguzi wa Ndani (Professional Diploma in Internal Auditing), pamoja na Stashahada ya Kitaaluma katika Utoaji wa Taarifa za Uendelevu (Professional Diploma in Sustainability Reporting).
Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb) akisoma hotuba yake kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) kwenye mahafali ya 49 ya NBAA yaliyofanyika katika hoteli ya APC Bunju mkoani Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA. Prof. Sylvia S. Temu akizungumza kuhusu namna Bodi hiyo ilivyofanikisha kuongeza idadi ya wahitimu kwa mwaka huu wakati wa mahafali ya 49 ya NBAA.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA Prof. Siasa Issa Mzenzi akitoa ufafanuzi kuhusu Bodi hiyo inavyofanya kazi zake wakati wa mahafali ya 49 ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA).
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), CPA Adv. Charles E. Kichere akizungumza jambo wakati wa mahafali ya 49 ya NBAA.
Mkurugenzi Mtendaji Mtaafu wa NBAA, CPA Pius A. Maneno akisoma hotuba yake kuhusu mafanikio yaliyopatikana kwenye kipindi chake cha uongoziwake wakati wa mahafali ya 49 ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA).
Baadhi ya Wahitimu pamoja na wageni waalikwa wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb) kwenye mahafali ya 49 ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA).
Wahitimu wa ngazi ya CPA wakisoma viapo vyao wakati wa mahafali ya 49 ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA).
Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb) akiwatunuku wahitimu kwenye mahafali ya 49 ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA).
Wahitimu wakishangilia mara baada ya kutunukiwa CPA wakati wa mahafali ya 49 ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA)
Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb) akitoa vyeti kwa wahitimu waliofanya vizuri kwenye mitihani ya Bodi wakati wa mahafali ya 49.
Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) wakati wa mahafali ya 49 ya Bodi hiyo.



Wahitimu wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) wakiwa kwenye maadamano ya kitaaluma wakati wa mahafali ya 49 ya Bodi hiyo yaliyofanyika katika hoteli ya APC Bunju, Dar es Salaam.



NBAA YAENDESHA WARSHA YA IPSAS MOROGORO



Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), Septemba 8, 2026, imeendesha Warsha ya Mafunzo kuhusu Uandaaji wa Hesabu kwa kuzingatia Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu kwa Sekta ya Umma (IPSAS), mkoani Morogoro.

‎Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Prof. Siasa I. Mzenzi, amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa IPSAS, hatua ambayo imeiwezesha nchi kujenga uwezo na kupata uzoefu unaoweza kuwa mfano kwa mataifa mengine.

CPA ‎Prof. Siasa amesema Tanzania kwa sasa imevuka hatua ya msingi ya kujenga uwezo katika eneo la IPSAS, tofauti na baadhi ya nchi ambazo bado zinaendelea kutafuta namna ya kuimarisha uwezo wa wataalamu wao katika utekelezaji wa viwango hivyo. Amesema mafanikio hayo yameifanya Tanzania kuwa na nafasi ya kushirikisha uzoefu wake na nchi nyingine.

‎“Tumefanikiwa sana kwenye IPSAS, mkazo huo kwa sasa tunauelekeza pia kwenye Sustainability Reporting na tayari tumeshatoa Technical Pronouncement No. 1 ya mwaka 2024 ambayo inazitaka taasisi kuanza kutoa taarifa za Sustainability.

CPA ‎Prof. Siasa amesisitiza umuhimu wa Taasisi za Umma kutumia mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa IPSAS kama msingi wa kuimarisha utoaji wa taarifa za uendelevu, akieleza kuwa maeneo hayo yanapaswa kwenda sambamba katika kukuza uwazi, uwajibikaji na uendelevu wa taasisi za umma.

‎Katika hatua nyingine, amewahamasisha washiriki wa warsha hiyo kuweka kipaumbele katika uandaaji na uwasilishaji bora wa vitabu vya hesabu kwa ajili ya "Best Presented Financial Statements Awards", akieleza kuwa idadi ya washindi itaongezwa kutoka watatu hadi watano.

‎Warsha hii ya IPSAS inalenga kuwawezesha washiriki kuongeza uelewa na ujuzi kuhusu matumizi sahihi ya IPSAS katika uandaaji wa taarifa za fedha za sekta ya umma, pamoja na kuimarisha weledi wa wataalamu katika eneo la Uhasibu na Ukaguzi wa hesabu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) CPA Prof. Siasa I. Mzenzi akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha ya Mafunzo kuhusu Uandaaji wa Hesabu kwa kuzingatia Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu kwa Sekta ya Umma (IPSAS), mkoani Morogoro.
Mkurugenzi wa Huduma za Viwango vya Kiuhasibu, Utafiti na Huduma za Ufundi wa NBAA, Angyelile Tende akizungumza kwenye warsha ya Mafunzo kuhusu Uandaaji wa Hesabu kwa kuzingatia Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu kwa Sekta ya Umma (IPSAS), mkoani Morogoro.
Baadhi ya washiriki pamoja na watumishi wa NBAA wakifuatlia ufunguzi wa warsha ya Mafunzo kuhusu Uandaaji wa Hesabu kwa kuzingatia Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu kwa Sekta ya Umma (IPSAS), mkoani Morogoro.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) CPA Prof. Siasa I. Mzenzi  katikati waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya washiriki pamoja na watumishi wa NBAA kwenye warsha ya Mafunzo kuhusu Uandaaji wa Hesabu kwa kuzingatia Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu kwa Sekta ya Umma (IPSAS)