HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

ALIYEKUWA MKURUGENZI MKUU (NIDA) AKOSA DHAMANA ARUDISHWA RUMANDE

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


MAHAKAMA Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, imetoa masharti ya dhamana kwa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dickson Maimu na wenzake watano, wanaokabiliwa na mashitaka ya kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 1.2.
Jaji Eliezer Feleshi, alitoa masharti hayo juzi baada ya kukubali hoja za maombi yaliyowasilishwa na washtakiwa hao. Hata hivyo baada ya kutolewa kwa masharti hayo, washtakiwa walirudishwa rumande baada ya kushindwa kuyatimiza.
Mbali na Maimu, washtakiwa wengine waliopewa masharti ya dhamana ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Joseph Makani, aliyekuwa Ofisa Usafirishaji, George Ntalima, na aliyekuwa Mkurugenzi wa Sheria, Sabina Raymond.
Wengine ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Bima ya Aste Insurance Brokers Company, Astery Mwita Ndege, aliyeingia mkataba na Nida wa kutoa huduma za bima na Xavery Silverius Kayombo, ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Gotham Internatianal Limited.
Akitoa masharti hayo, Jaji Feleshi alisema, Maimu alitakiwa kutoa dhamana ya Sh milioni 315.9, mshtakiwa wa pili Sh milioni 105.8, wa tatu Sh milioni 6.9, wa nne na watano kila mmoja Sh milioni 22.05.
Aidha, kila mshtakiwa anatakiwa kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika, wanaotakiwa kusaini hati ya dhamana ya nusu ya fedha zilizotajwa na Mahakama.
Aliongeza kuwa, washtakiwa hawaruhusiwi kusafiri nje ya Dar es Salaam bila kibali cha Mahakama pia wawasilishe hati za kusafiria kwenye ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na kila mmoja anatakiwa kufika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa muda na tarehe kesi itakapopangwa.
Awali washtakiwa hao, waliwasilisha maombi hayo na Mahakama iliyatupilia mbali, hata hivyo waliwasilisha tena maombi hayo. Washtakiwa hao wanadaiwa kutumia vibaya madaraka yao wakati wakitekeleza majukumu yao, kutumia nyaraka za uongo na kuisababishia mamlaka hiyo hasara ya Sh bilioni 1.2.

ALIYEKUWA MKURUGENZI WA MAMLAKA YA VITAMBULISHO VYA TAIFA NA WENZAKE WAFIKISHWA MAHAKAMANI LEO

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.



ALIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu na maofisa wengine saba waandamizi, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka 27 yakiwamo ya matumizi mabaya ya ofisi na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh bilioni 1.2.
Washitakiwa wengine ni Mkurugenzi wa Huduma za Kibiashara, Avelin Momburi, Meneja wa Fedha na Uhasibu, Benamini Mwakatumbula, Meneja wa Bajeti na Milki, Joseph Makani, Ofisa Usafirishaji, George Ntalima na Mkurugenzi wa Sheria, Sabina Raymond.
Wengine ni Xavery Kayombo ambaye wadhifa wake haukutajwa, na Astery Ndefe ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Brokers Company Limited. Washitakiwa hao pia wanakabiliwa na mashitaka yanayohusu kutumia nyaraka zenye kusudio la kudanganya na kula njama za kutenda kosa.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicious Mwijage, washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote dhidi ya mashitaka hayo kwa sababu wanashitakiwa chini ya Sheria ya Uhujumu Uchumi. Wote waliamuriwa kurejeshwa mahabusu hadi Agosti 31, mwaka huu kesi yao itakapotajwa tena.
Uchunguzi wa kesi hiyo kwa mujibu wa waendesha mashitaka, wanaoongozwa na Mwanasheria Mwandamizi wa Serikali, Awamu Mbangwa haujakamilika. Hakimu alisema kwamba suala la dhamana litaamuriwa na Mahakama Kuu, kwa kuwa kiwango cha fedha katika kesi hiyo kinazidi Sh milioni 10.
Lakini alisema atatoa uamuzi kuhusu dhamana kwa washitakiwa Mobuli na Makani kesho kwa sababu ya hoja kwamba wawili hao hawakabiliwi na mashitaka ya uhujumu uchumi, kama washitakiwa wengine. Jopo la waendesha mashitaka linawajumuisha pia Leonard Swai, Janeth Machuria, Joseph Kiula na Fatma Waziri.
Waendesha mashitaka walidai kuwa katika tarehe tofauti kati ya mwaka 2010 na 2015, wakiwa watumishi wa umma, Maimu na Mwakatumbula walitumia vibaya madaraka yao kwa kuidhinisha kwa Kampuni ya Gotham International Limited malipo ya Dola za Marekani milioni 5.175 pamoja na Sh milioni sita.