Boti nyingine yazama Z’bar
Mwezi
mmoja tu tangu maafa ya kuzama kwa boti ya Mv Skagit iliyotokea Chumbe
Unguja Julai 18, watu wengine 10 kati ya 12 wamenusurika kufa kwenye
bahari kuu kati ya Pangani, Tanga na Mkoa wa Kaskazini Unguja baada ya
boti Mv Saluwat waliyokuwa wakisafiria kuzama.
Katika
ajali hiyo iliyotokea jana, watu wawili, Khalfan Saleh Ali ambaye ni
mmoja wa mabaharia wa chombo hicho na mwingine mwanamke, hajajulikana
jina, wanahofiwa kufa maji kwa kuwa hadi jioni walikuwa hawajapatikana.
Walionusurika
ni Athumani Makame Athumani (40) wa Mtoni Kidatu, nahodha Ali Idi Haji
(51) wa Pita na Zako, Shaame Ali Shaame (33) wa Mtoni Kidatu, Khamis
Juma Mtwana (33) wa Kibeni, Ahmada Haji Kombo (47) wa Shangani
Mkokotoni, Athumani Ali Shaame (50) wa Magogoni na Fundi Khalid (49) wa
Kizimbani Pita na Zako.
Raia wa kigeni walionusurika ni Banmin Luubih (30) na Jeenle Rog (29), Raia wa Wafaransa na Ruud Verhees (23) wa Uholanzi.
Watu
hao walikuwa katika boti hiyo iliyotoka bandari ya Pangani asubuhi juzi
ikienda bandari ndogo ya Mkokotoni ikiwa na abiria 12 na magunia ya
nazi.
Kati
ya watu waliookolewa kutokana na jitihada za wavuvi wa bandari ndogo ya
Shangani, Mkoa wa Kaskazini Unguja, walikuwemo raia watatu wa kigeni.
Fundi
mkuu wa boti hiyo, Khalid Haji Maulid, alisema iliondoka Pangani saa
2.30 asubuhi siku ya Jumapili na ikaanza kupata dhoruba na kuingiza maji
kwenye chombo majira ya saa 9 mchana.
Alisema walijitahidi kuyatoa maji kwa kutumia pampu, lakini mashine hiyo nayo ilipungua nguvu na kuharibika.
Fundi
Khalid alisema waliamua kurudi bandarini Pangani, lakini hawakufika
mbali kwani chombo kilizidi kuingiza maji na injini yake ikazimika.
“Abiria
wote tuliwapa life jacket kwa ajili ya kujiokoa. Wengine walikuwa
wakielea huku wameshika chombo na waliokuwa wakijua kuogelea,
walijirusha kwenye maji,” alisema fundi huyo ambaye alikuwa mmoja wa
wafanyakazi wa boti hiyo inayomilikiwa na Ahmad Haji Kombo, mkazi wa
Shangani, Mkokotoni.
Alisema
walilazimika kufanya kazi usiku kucha kuelekeza abiria wasikumbwe na
mawimbi kwa kushikilia sehemu ya juu ya chombo, lakini hatimaye chombo
kilizama kabisa usiku wa manane.
Fundi
Khalid alisema akiwa na nahodha wa chombo, Ali Idi Haji, walitoa ripoti
ya tukio hilo kwa vituo vya polisi wanamaji bandarini Pangani na Tanga
mjini, lakini hawakupata msaada wowote haraka.
“Tuliwafahamisha
tangu majira ya saa 9 mchana kuwa tupo eneo la Maziwe tunahitaji msaada
wa haraka, lakini bahati mbaya hadi kunakucha hatukuwaona,” alisema.
Fundi
Khalid alisema kutokana na kuchelewa kupata msaada wa polisi wanamaji,
waliwasiliana na wavuvi wanaowafahamu wanaoishi Shangani Mkokotoni.
Hata
hivyo, wavuvi hao walishindwa kutoka haraka kutokana na maji kuwa
yamejaa ambapo walisubiri hadi usiku wa manane yalipokupwa ndipo
wakaanza safari ya kuwatafuta ili kuwapa msaada.
Alisema watu wawili ambao hawajapatikana, mwanamke na mwanamume, walipotea alfajiri baada ya kuishiwa nguvu.
Chombo hicho kilisajiliwa na Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) kwa namba Z907 SV kikiwa na uwezo wa kuchukua abiria 50.
Mvuvi
aliyeongoza operesheni ya kuokoa watu hao, Rajabu Hamad Juma, aliiambia
NIPASHE kuwa alipokea taarifa majira ya saa 11 jioni juzi kutoka kwa
watu waliokuwa kwenye boti hiyo wakiomba msaada baada ya chombo kuzidiwa
na maji.
Alisema
walianza safari baada ya maji kupwa usiku wa manane wakitumia tochi na
taa za kandiri kwenda eneo la tukio la Maziwe walikoelekezwa.
Ilipofika
saa moja asubuhi jana ndipo walipowaona watu hao na walifanikiwa
kuwaokoa wakiwa salama na kuwapakia katika boti yao ya MV Tawakal.
“Laiti kungekuwa na vyombo vya kisasa watu hao wangeokolewa mapema zaidi,” alisema.
Kamanda
wa kikosi cha Polisi wanamaji Zanzibar, Martin Lissu alisema walipokea
taarifa za tukio mapema wakiwa kituoni kwao Malindi, lakini kulikuwa na
tatizo kubwa la mawasiliano kati yao na polisi wanamaji wa bandari ya
Tanga.
Kamanda
Lissu alisema polisi wenzao wa Bandari ya Tanga waliokuwa karibu zaidi
na eneo la tukio walikuwa wamewaeleza kuwa wamechukua hatua za kufika
eneo hilo, lakini hawakuwaona watu haraka.
Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa ZMA, Abdalla Hussein Kombo, alisema mamlaka yake
ambayo haikutoa msaada wowote kufika eneo la tukio, inakabiliwa na
tatizo kubwa la ukosefu wa vifaa vya mawasiliano na boti maalum.
Aliwasifu wavuvi wa Shangani Mkokotoni waliofanikiwa kutoa msaada na kuokoa abiria.
Baadhi ya walionusurika walipelekwa Hospitali ya Mkoa wa Kaskazini Unguja ya Kivunge kupatiwa huduma ya kwanza.
Tukio
hilo linakumbusha matukio mawili ya kuzama kwa Mv Spice Islander I
Septemba 10, 2011 na MV Skagit Julai 18 mwaka huu, ambazo ziliua mamia
ya watu na wengine kunusurika.
Ajali
hii inafanya ajali kubwa za boti kufikia tatu ndani ya mwaka mmoja
tangu Septemba 10, mwaka jana ambapo watu 1,529 walikufa na 941
kuokolewa baada ya meli ya MV Spice Islanders kupinduka na kuzama
katika mkondo wa bahari eneo la Nungwi Zanzibar.
Meli
hiyo ilizama kutokana na kuzidisha abiria na mizigo; kitendo
kilichopelekea viongozi kadhaa wakiwemo maofisa na vigogo wa Shirika la
Bandari na Mamlaka ya Usafiri Baharini kusimamishwa na kufunguliwa
mashitaka ya uzembe na kusababisha vifo.
Katika
ajali ya Mv Skagit iliyotokea karibu na kisiwa cha Chumbe ikiwa na
abiria 248, watoto 31 na mabaharia 9, watu 146 waliokolewa wakati 139
walikufa.
HABARI NA MWINYI SADALLAH
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment