Viongozi
watatu wa ngazi ya juu wa Serikali ya Mkoa wa Katavi wametapeliwa na
watu wasiojulikana baada ya kuelezwa kuwa wameshinda promosheni ya
Airtel ya Shilingi milioni 50.
Waliotapeliwa
ni Mkuu wa Mkoa wa Katavi Dkt. Rajabu Rutengwe, Katibu Tawala wa Mkoa,
Emmanuel Kalobelo na Mganga Mkuu wa Mkoa, Yahaya Hussein.
Viongozi
hao walitapeliwa kwa nyakati tofauti na watu waliojitambulisha kwao kwa
simu kuwa ni watumishi wa Kampuni ya Simu ya Airtel.
Tukio
la kwanza lilikuwa ni la Mkuu wa Mkoa kuambiwa ameshinda zawadi ya Sh.
milioni 50 na aliombwa awatumie namba za simu za watu watano
aliozungumza nao mara ya mwisho na baada ya kufanya hivyo simu yake ya
mkononi ikafungwa na matapeli hao.
Akieleza
mkasa huo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Katavi Dkt. Yahaya alisema yeye baada
ya kupigiwa simu na matapeli hao hakuwa na shaka nao kutokana na kauli
yao ilivyokuwa ya ustaarabu. Alisema baada ya kuwapa majina ya watu
watano alizungumza nao mara ya mwisho kwenye simu yake na kuombwa
awatajie namba zake za siri za akaunti ya Benki ya NMB ili wamtumie
zawadi ya Sh. milioni 50. Baada ya kuombwa namba yake ya siri, Dkt.
Yahaya hakuwa na shaka yoyote na hivyo akawapatia namba hiyo ya siri.
Hata hivyo hakuweza kuibiwa fedha zozote kwa vile akaunti yake haikuwa
na salio la kutosha.
Meneja
wa Wawi la NMB Wilaya ya Mpanda, Erick Luhanda alisema amepokea
malalamiko kutoka kwa viongozi hao. Alisema kiongozi wa mwisho kumpa
taarifa alikuwa ni Katibu Tawala wa Mkoa, Kalobelo. Luanda alisema
tayari taratibu za kibenki zimefanyika hivyo hakutakuwa na hujuma kwenye
akaunti za viongozi hao.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari alithibitisha kutokea matukio hayo.



No comments:
Post a Comment