HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

» »Unlabelled » Makinda: Kuna siku Tanzania itaongozwa na mwanamke



Ibrahim Yamola
SPIKA wa Bunge, Anne Makinda, amefunga na kutabiri  kuwa kuna siku Serikali ya Tanzania itaongozwa na mwanamke.

Amesema tayari ameona mwanga wa wanawake kushika hatamu ya uongozi katika miaka kadhaa ijayo na kuwataka wanawake waendeleo na moyo wa kujituma ili kufikia malengo hayo.

“Naona mwanga wa mafanikio kwa watoto wa kike na hii inaonyesha kuwa miaka kadhaa ijayo, wanawake wataiongoza Serikali kutokana na juhudi zao,” alisema Makinda.

Alisema  katika  miaka kumi ijayo kuanzia  sasa, kutakuwa na wimbi kubwa la mabadiliko yatakayotokana nan tatizo la wanaume kuchagua kazi.

“Huko tunakoelekea wanaume watakuwa maskini kwa kuwa wanachagua kazi za kufanya lakini wanawake wanaonyesha jitihada katika kazi mbalimbali za kijamii hii ni changamoto kwa wanaume,” alisema.

Spika Makinda aliyasema hayo juzi,  alipokuwa akizungumza katika sherehe za miaka 100 ya Mama Barbro Johansson  na mahafali ya kumi ya kidato cha nne na ya saba ya kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Barbro Johansson, iliyopo nje kidogo ya  jijini Dar es Salaam.

Alisifu jitihada kubwa zinazofanywa na wanawake wanaojishughulisha katika nyanja  mbalimbali ya maendeleo huku wakiibua kwa kasi katika eneo la kisiasa.

Alisema hali hiyo ndiyo inayoashiria  picha kwamba dhana ya mapinduzi kwa ajili ya ukombozi kwa wanawake, sasa  ni jambo lisilokwepeka.

Alisema kitendo cha wanawake kufanya biashara bila kuchagua, kinaashiria kwamba kuna siku wanaume watakuwa tegemezi kwa wanawake.

“Wanawake wa kipindi hiki hawachagui kazi wala biashara za kufanya, kitu ambacho kitaleta mafanikio kwa haraka,”alisema.

Makinda ambaye ndiye mwanamke wa kwanza katika historia ya siasa za Tanzania kushika wadhifa wa Uspika, aliwahimiza wanafunzi hao kujishughulisha zaidi na masuala ya elimu na kuweka kando mambo mengine yanayoweza kuvuruga mfumo wao wa kielimu.

 “Wanaume wa siku hizi wanatumia fedha kuwarubuni na baadaye kuwaacha na wakati mwingine fedha wanazotumia kuwaonyesha sio zao ni za wizi hivyo waepukeni” alisema  Makinda.

Kauli ya Makinda inakuja katika wakati ambapo vugu vugu la mabadiliko likizidi kushika kasi kwa nchi za Afrika, ambazo kwa miaka mingi zimelalamikiwa kwa  kuendelea kukumbatia mfumo dume unaokandamiza ustawi wa wanawake.

Mabadiliko ya kisiasa yaliyojitokeza hivi karibuni nchini Malawi kwa mwanasiasa Joyce Banda kuwa Rais wa kwanza mwanamke wa taifa hilo na historia iliyowekwa na kiongozi wa Liberia Johnson Sirleaf kuwa mwanamke wa kwanza barani Afrika kuwa Rais, ni baadhi ya matukio yanayochagiza vugu vugu la mabadiliko ya kisiasa kwa nchi za Afrika.

Katika hotuba yake ya kumkaribisha Spika Anne Makinda, Mwenyekiti Mwanzilishi wa Mfuko wa Joha Trust, Profesa Anna Tibaijuka alisema shule hiyo ilianzishwa na kupewa jina la muasisi wake Mama Barbro Johansson ikiwa ni sehemu ya kuenzi mchango wake kwa kuthamini juhudi za wasichana.

Profesa Tibaijuka ambaye pia ni Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema mwaka huu Mama Barbro anatimiza miaka 100 tangu azaliwe.

Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz/habari







«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments: