Mwanafunzi
wa kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Alfa iliyopo Manispaa ya
Morogoro, Jesca Kiliani akifanya mtihani wa taifa wa kidato hicho akiwa
wodini katika Hospitali ya Rufaa ya mkoani Morogoro, jana, alikolazwa
kwa ajili ya matibabu baada ya kufanyiwa oparesheni. Wanafunzi wa kidato
cha nne nchini waameanza mitihani ya kuitimu kidato hicho.
MWANAFUNZI
wa kidato cha nne katika Sekondari ya Alfa Germ, Morogoro, Jessica
Kiliani (17), amelazimika kufanya mtihani wake wa kuhitimu elimu hiyo
akiwa wodini baada ya kufanyiwa upasuaji.
Hatua hiyo
ilifikiwa baada ya mwanafunzi huyo, kuomba aruhusiwe kufanya mtihani huo
licha ya kuwa wodini akiugulia maumivu ya upasuaji aliofanyiwa na
madaktari wa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa zaidi saa ya mbili na
kulazwa katika wodi ya wazazi namba 7B.
Mama mzazi
wa mwanafunzi huyo, Anna Ngapemba alisema alipigiwa simu na mkuu wa
shule hiyo 6:00 usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili iliyopita akimjulisha
kuwa binti yake anasumbuliwa na tumbo na anahitaji msaada wa haraka.
Ngapemba
alisema alilazimika kwenda shuleni hapo usiku huohuo na kukutana na mama
mlezi (matron) wa hosteli za shule hiyo na kujulishwa juu ya hali ya
binti yake na kwa kushirikiana na uongozi wa shule hiyo, walimpeleka
katika Hospitali ya Mkoa.
Alisema
wauguzi waliokuwa zamu usiku huo walilazimika kumpigia simu daktari
bingwa wa magonjwa ya wanawake, Christopher Manumbu ambaye alifika na
kumfanyia upasuaji kutokana na hali aliyokuwa nayo.
Mama huyo alisema binti yake aliwahi kulalamika kuwa na maumivu ya tumbo
akiwa kidato cha pili mwaka 2010 lakini baada ya kupatiwa matibabu,
hali hiyo haikumtokea tena hadi Jumamosi iliyopita.
Baada ya upasuaji huo, Dk Manumbu alisema binti huyo alihitaji upasuaji wa haraka ili kutokana na hali yake kuwa mbaya.
Akiwa chini
ya msimamizi wa mitihani na polisi, Jessica licha ya kuwa katika hali ya
maumivu alifanya mitihani miwili kama wenzake wa kidato hicho. Mitihani
hiyo ni Uraia na Kiingereza.
Mwanafunzi
huyo alisema hakuwa tayari kuikosa mitihani hiyo na ndiyo maana
alimwomba mama yake kuwasiliana na uongozi wa shule yake ili umwandalie
mazingira mazuri ya kufanya mtihani akiwa wodini.
Alifanya mitihani yote miwili akiwa katika Wodi ya Wazazi namba 7B, katika chumba cha pekee.
Watahiniwa Jitegemee chupuchupu
Zaidi ya wanafunzi 30 wa Shule ya Sekondari Jitegemee, Dar es Salaam
nusura wasifanye mtihani wao wa kidato cha nne kutokana na kutokuwa na
vitambulisho vinavyowaruhusu kuingia katika chumba cha mtihani.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Luteni Kanali Martin Mkisi alisema jana kuwa
wanafunzi hao walisahau vitambulisho hivyo lakini waliombewa kwa
msimamizi mkuu wa mitihani hiyo.
“Changamoto
huwa hazikosekani licha ya kuwaandaa vizuri wanafunzi, lakini wamesahau
vitambulisho, kama mkuu wa shule nilichukua jitihada ya kuwaandikia
ujumbe mfupi wa utambulisho ili waweze kufanya mtihani,” alisema Mkisi.
Akizungumzia
mtihani huo, mmoja wa watahiniwa katika shule hiyo, Hafsa Ramadhani
alisema ulikuwa mzuri kutokana na maandalizi aliyofanya.
Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne Tanzania Bara ulianza jana na unatarajiwa kumalizika Oktoba 25, mwaka huu.
Habari na Venance George na Juma Mtanda, Morogoro; Magreth Munisi, Deborah Ngajilo na Aisha Ngoma
Picha na Juma Mtanda
Chanzo - Mwananchi



No comments:
Post a Comment