WAZIRI
Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika, amemtaka Spika wa Bunge, Anna
Makinda, kutumia madaraka na mamlaka yake kutangaza kwa umma kamati
nyingine ya kudumu ya Bunge itakayoshughulikia masuala ya gesi asili
kabla na wakati wa mkutano wa Bunge ujao mwishoni mwa mwezi huu.
Mnyika
ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo kupitia CHADEMA, alisema hatua hiyo ni
kutokana na hali tete na tata kuhusu sekta ndogo ya gesi asilia nchini
na kwa kuzingatia umuhimu na unyeti wa sekta hiyo katika uchumi wa nchi
na maisha ya wananchi.
Katika
taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Mnyika alisema pamoja na mambo
mengine, Spika Makinda aelekeze kamati hiyo kupokea na kujadili taarifa
ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge ya mwaka 2011 kuhusu sekta ndogo ya
gesi asili ikiwemo juu ya hatua iliyofikiwa katika kushughulikia tuhuma
za ufisadi.
Madai
mengine ni ya mapunjo ya fedha za mauzo ya gesi asili na hatua
iliyofikiwa katika maandalizi ya sera, mpango mkakati na sheria ya gesi
asili.
“Hatua hii
ni muhimu kufuatia ukimya wa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter
Muhongo kuhusu kauli yangu ya Oktoba 4, 2012 ya kutaka taarifa ya
ufafanuzi kuhusu utafutaji wa mafuta na gesi asili nchini iliyotolewa na
wizara hiyo Septemba 21 mwaka huu ifutwe,” alisema.
Alisema kuwa
taarifa hiyo ya wizara ilieleza kuwa maandalizi ya sera ya gesi asili
yapo katika hatua za mwisho wakati ambapo kamati mbalimbali za kudumu za
Bunge hazijahusishwa katika mchakato huo muhimu pamoja na kuwa mamlaka
ya kutunga sera kwa mfumo wa sasa ni ya Baraza la Mawaziri.
“Kwa unyeti
na upekee wake sera ya gesi, Spika wa Bunge anapaswa kuwezesha Kamati za
Kudumu za Bunge zihusishwe ili pawepo mashauriano na maridhiano kwa
mapana na marefu,” alisema.
Mnyika
alisema izingatiwe kwamba katika mkutano wa nane wa Bunge, Spika
alitangaza kuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imevunjwa
na kwamba majukumu iliyokuwa ikishughulikiwa yatashughulikiwa na kamati
nyingine kwa mujibu wa madaraka na mamlaka ya spika.
CHANZO: Tanzania Daima




No comments:
Post a Comment