HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

» »Unlabelled » Serikali imekalia bomu Mifuko ya Hifadhi ya Jamii

INAWEZEKANA kabisa kwamba Serikali mpaka sasa haijang’amua kwamba wafanyakazi wote nchini wanalichukulia suala la mafao yao katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kama suala la kufa na kupona. Serikali haionyeshi dalili zozote kuwa, inatambua kwamba wafanyakazi wamejaa hasira kuhusu namna mafao yao yamekuwa yakisimamiwa na mifuko hiyo.

Wala haionyeshi kutambua ukweli kwamba sasa wafanyakazi wamezinduka kutoka katika usingizi wa pono uliowapumbaza kwa miaka mingi. Pia haijahisi kwamba wafanyakazi nchi nzima, kwa umoja na mshikamano wao wameapa kutorudi nyuma hadi sheria na mifumo inayosimamia mifuko hiyo zifanyiwe marekebisho siyo tu ili haki itendeke, bali pia ionekane pasipo shaka yoyote  kwamba haki kweli inatendeka.
Tunasema hivyo kwa sababu ingekuwa imetambua yote hayo isingekuwa inashughulikia matakwa ya wafanyakazi hao kisanii, wala isingeonyesha undumila kuwili kwa leo kusema hivi na kesho kusema kinyume chake kabisa. Ingekuwa imeng’amua kwamba wafanyakazi sasa wametambua kwamba mifuko hiyo inatumia mafao yao katika namna ambayo hawanufaiki nayo  isingekuwa inapiga chenga kama inavyofanya hivi sasa inapopaswa kuwa tayari imeandaa muswada maridhawa wa kuwasilisha bungeni mwezi ujao kuhusu mifuko hiyo kuwa na vipengele vya fao la kujitoa kwa wanachama wake.
 Sasa tunaambiwa kwamba Muswada wa Marekebisho ya sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambao kama tulivyosema hapo juu unatarajiwa kuwasilishwa bungeni mwezi ujao, umewaacha solemba wanachama wa mifuko mingine baada ya marekebisho hayo kurejesha fao la kujitoa kwa mfuko mmoja tu. Itakumbukwa kwamba Sheria ya mafao ilipitishwa katika kikao cha Bunge cha Aprili mwaka huu na kuwazuia wanachama wa mifuko hiyo kuchukua mafao yao kabla ya umri wa kustaafu wa  miaka 55 hadi 60.
   Itakumbukwa pia kuwa, baada ya wanachama wa mifuko hiyo na wadau wengi kuipinga sheria hiyo, Serikali iliahidi kwamba ingeifanyia marekebisho sheria hiyo na kuwasilisha muswada wa marekebisho hayo bungeni kwa hati ya dharura mwezi ujao. Sasa tunaambiwa kwamba tayari Serikali imewasilisha muswada huo kwa uongozi wa Bunge.
   Hata hivyo, ni jambo la kushangaza kwamba muswada huo unapendekeza marekebisho kwenye Sheria ya Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF) tu kwa kuongeza kifungu kipya cha fao la kujitoa kwa wanachama wake. Kwa maneno mengine, wanachama wa mifuko mingine hawataruhusiwa kujitoa kabla ya kutimiza miaka ya kustaafu tuliyobainisha hapo juu.
   Sasa nini yatakuwa matokeo ya hali hiyo ya kushangaza? Hakuna asiyetambua athari zitakazotokana na hatua hiyo ya Serikali. Tutegemee kutokea hali ya sintofahamu ya migogoro, vurugu, migomo ya wafanyakazi isiyokwisha na kuporomoka kwa uchumi wa nchi kwa kiwango cha kutisha, kwani wafanyakazi wa migodini na kwingineko wataweka vitendea kazi chini na kuondoka kwa ghadhabu kubwa.
   Serikali inaonekana kusahau kwamba hoja ya msingi ya wafanyakazi ni kuwa, hali ya maisha katika miaka tuliyomo hayana uhakika wa mtu kuishi hadi miaka ya kustaafu, mbali na kwamba waajiri wengi wanawapa wafanyakazi wao mikataba ya muda tu badala ya mikataba ya kudumu. Kwa maana hiyo, baada ya mikataba yao kuisha itawabidi wajitoe katika mifuko hiyo na kuchukua mafao yao ili yawasaidie maishani.
   Yanasemwa mengi kuhusu lengo la hatua hiyo ya Serikali kwamba inalenga kuinusuru mifuko ya hifadhi kadhaa ambayo inasemekana tayari imefilisika. Ni siri iliyo wazi kwamba Serikali inajikuta katika hali ngumu na ya aibu kutokana na ukweli kwamba nayo imekuwa sehemu ya tatizo kwa kukopa mabilioni ya fedha katika  mifuko hiyo na kushindwa kuzirejesha.
   Kwa mfano, NSSF imesema inaidai Serikali zaidi ya Sh366 bilioni ilizokopa kujenga Chuo Kikuu cha Dodoma, nyumba za polisi Kurasini na Machinga Complex zote za jijini Dar es Salaam. Hakuna asiyejua kwamba Serikali ilikopa fedha hizo kwa malengo ya kisiasa. Leo hii tunashuhudia wafanyakazi wakifanywa kafara kwa makosa ya wanasiasa.
 
CHANZO: MWANANCHI

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments: