Watu 12 mbaroni kwa kuteka basi la Sumry

Watu 12 wanashikiliwa na  polisi wilayani Mpanda  mkoani Katavi  kwa tuhuma za  kuteka  basi la  la kampuni ya  Sumry  mwishoni mwa wiki.

Watuhumiwa  hao wanadaiwa  kuteka  basi lenye namba za usajili T 902 AZT Nissan Diesel ambalo lilikuwa likiendeshwa na  na Khalid Makamba  Oktoba 17  saa 6:23 usiku  katika eneo la Magamba lililopo katika Tarafa ya Nsimbo wilaya ya Mlele.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Joseph Myovela, alisema watekaji wakiwa na marungu,  mapanga na nondo waliweka mawe barabarani   na  kufanikiwa kuteka basi  hilo lilikuwa na abiria  wakitokea Sumbawanga  kuelekea wilayani Mpanda.
Majambazi hao walipora abiria simu, pesa na vitu mbalimbali ambavyo thamani yake bado  haijajulikana. 
Aliwataja watu hao kuwa ni Elias Zakaria  (45), mkazi Katumba na Mbuya Michael (25) na Moses Liberatus (24), wakazi wa mjini  Mpanda; Jackson Lucas (27), mkazi wa kijiji cha Katisunga wilayani Mlele; Mussa Nassor (17) na Ramadhani Hassan (17) ambao ni wakazi wa mtaa wa Majengo wilayani Mpanda.
Wengine ni wakazi wa Majengo Abdallah Hassani (19), Joseph Masesa (22), Sayo  Masunga (18), Christopher Kwebe  (20),  Elias George (24) na Shaban Loxagune (22), mkazi wa makazi ya wakimbizi ya Katumba Wilaya ya Mlele.
Alisema upelelezi utakapo kamilika watafikishwa mahakamani kujibu mashitaka.

CHANZO: NIPASHE

No comments

Powered by Blogger.