Rajabu Maranda (Fulana ya Blue) na Farijala Hussein
Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imewahukumu kutumikia
kifungo jela miaka tisa wafanyabiashara watatu; Farijala Hussein, Rajabu
Maranda na Ajai Somani na kuwaamuru wafanyakazi watatu wa Benki Kuu ya
Tanzania (BoT), kulipa fidia ya Sh. milioni 15 baada ya kupatikana na
hatia ya wizi wa fedha kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (Epa) ndani ya
BoT na kuisababishia benki hiyo hasara.
Pia imewaamuru wafanyabiashara hao
kurejesha Sh. 1,099,400,000.10 na wakishindwa mali zao zitaifishwe, huku
wafanyakazi hao wa BoT wakihukumiwa kwenda jela miaka mitatu kila mmoja
iwapo watashindwa kulipa faini ya Sh. milioni 5 kila mmoja baada ya
kupatiakana na hatia ya kosa la sita la kuisababishia BoT hasara.
Watumishi wa BoT waliohukumiwa hukumu hiyo, ni Imani Mwakosya, Ester Komu na Sofia Lalika.
Hukumu hiyo ilisomwa jana na jopo la
mahakimu watatu wakiongozwa na Mwenyekiti, Samwel Karua, Beatrice
Mutungi na Illivin Mgeta waliosikiliza kesi hiyo.
Akisoma hukumu hiyo kwa niaba ya jopo
hilo, Hakimu Mgeta alisema mshtakiwa wa kwanza, Farijala atatumikia
kifungo cha miaka mitatu kwa kosa la pili, miaka miwili kwa kosa la
tatu.
Pia alisema Fariajala, Maranda na Somani watatumikia kifungo cha miaka miwili kwa kosa la nne.
Hakimu Mgeta alisema mbali na kifungo
hicho, Farijala anaamriwa kurejesha Sh. 82,956,400, ambazo ushahidi
umethibitisha kuwa aliiba.
“Pia mshtakiwa wa pili Maranda anaamriwa
kurejesha Sh. milioni 616.4 na mshtakiwa wa tatu Somani Sh. milioni 400,
ambazo ushahidi wa Jamhuri umethibitisha kuwa waliiba fedha hizo …
endapo washtakiwa wote watatu wakishindwa kurejesha fedha hizo mali zao
zitaifishwe,” alisema.
Alisema mahakama imekubaliana na hoja za
wakili wa utetezi Majura Magafu, kwamba, mshtakiwa wa nne Mwakosya, wa
tano Komu na wa sita Lalika waliamini kazi waliyoifanya ilikuwa sahihi,
hivyo walikuwa wakitekeleza majukumu yao wasiamriwe kurejesha fedha
zinazodaiwa kuchotwa BoT.
Washatkiwa hao walifikishwa mahakamani
hapo Novemba 4, 2008, wakikabiliwa na mashtaka sita, likiwamo la
kughushi na wizi wa Sh. bilioni 3.8.
Hata hivyo, upande wa Jamhuri umeweza
kutoa ushahidi wa kuwatia hatiani washtakiwa katika shtaka la pili la
kughushi, hati za kuhamisha mali kwa jina la Kampuni ya Mwibare Farm ya
Tanzania na Lakshmi Textile Mills Ltd ya Mumbai.
Katika shtaka la tatu na la nne, walidaiwa kuiba Sh. bilioni 3, 868, 805, 737. 13, mali ya BoT.
Katika shtaka la sita, walidaiwa kuwa
Desemba 7, 2005 wakiwa waajiriwa wa BoT, kupitia nyadhifa zao,
walizembea kazini na kuisababishia serikali hasara ya kiasi hicho cha
fedha.
CHANZO:
NIPASHE



No comments:
Post a Comment