HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

» »Unlabelled » Mawaziri wakabana koo ujumbe wa Nec

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ambaye ni Mke wa Rais Jakaya Kikwete, Mama Salma (kulia) akiwasikiliza wajumbe wenzake, Bernald Membe (kushoto) aliyekuwa akiteta na Mtoto wa Rais, Ridhiwani Kikwete walipohudhuria kikao cha halmashauri kuu kilichofanyika juzi usiku katika ukumbi wa White House, mjini Dodoma. Picha na Edwin Mjwahuzi  

MEMBE, MAKAMBA, LUKUVI, WASIRA
MANGULA AMRITHI MSEKWA UMAKAMU MWENYEKITI BARA, DK SHEIN ZANZIBAR

MATOKEO ya Uchaguzi wa Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec), kupitia kapu yaliwekwa kiporo hadi leo huku ikielezwa kwamba licha ya kuwepo kwa mchuano mkali, baadhi ya mawaziri wameibuka na ushindi.
Hatua hiyo imekuja huku Nec ikifanya mabadiliko makubwa katika uongozi wake wa juu baada ya kumpitisha Katibu Mkuu mstaafu, Philip Mangula kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara.
Tofauti na kawaida yake ya kutolaza matokeo katika chaguzi zake, jana Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete alitangaza kuahirisha mkutano huo hadi leo saa 3:00 asubuhi baada ya Mwakilishi wa Mpango wa Bara la Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM), John Shibuda kumaliza kutoa hotuba yake saa 2:30 usiku wakati huo wajumbe wakiwa wameshapiga kura za kuwachagua wajumbe hao.
Hata hivyo, habari zilizopatikana jana usiku zinasema kuwa baadhi ya mawaziri walikuwa wakiongoza hivyo kujihakikishia ushindi. Waliotajwa kuongoza ni Naibu Waziri Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano), Stephen Wassira, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, David Mathayo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Katibu wa CCM wa Uchumi na Fedha, Mwigulu Nchemba, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mjini, Jackson Msome na Mbunge wa Nkenge Asumpta Mshama.
Awali, Nec ilimteua Mangula kuwania nafasi hiyo kuchukua nafasi iliyokuwa inashikiliwa na kada mkongwe wa chama hicho, Pius Msekwa ambaye imeelezwa kuwa ameamua kustaafu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana asubuhi, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye alisema Nec iliyofanya kikao chake usiku wa kuamkia jana ilipitisha jina la Mangula kwa kishindo.
Akizungumzia uteuzi huo mjini Dodoma jana, Mangula alisema ameshtushwa na uamuzi huo wa chama, “…Nashukuru chama kuniamini lakini tusubiri uchaguzi kwani bado wanachama hawajapiga kura.”
Mbali ya kumpitisha Mangula, Nape alisema Nec pia ilimpitisha Mwenyekiti wa sasa wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete kutetea nafasi yake huku, Rais wa Serikali ya Zanzibar (SMZ), Dk Ali Mohamed Shein akiteuliwa kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti Zanzibar.
Nafasi ya Makamu Mwenyekiti Zanzibar, ilikuwa ikishikiliwa na Rais Mstaafu wa SMZ, Amani Karume ambaye alimaliza ngwe yake ya uongozi wa Serikali mwaka 2010.
Nape alisema majina hayo yatapelekwa katika mkutano mkuu wa chama hicho kesho kupigiwa kura ya ndiyo au hapana.
Dk Shein anachukua nafasi hiyo kutimiza utaratibu ndani ya chama wa Rais aliye madarakani kuwa pia na kofia ya uongozi wa juu ndani ya chama hicho.

Wachambua uteuzi
Uteuzi wa viongozi hao umetafsiriwa na wachambuzi wa masuala ya siasa nchini kwamba una lengo la kutibu majeraha yaliyotokana na makovu ya Uchaguzi Mkuu wa 2005 yaliyowagawa wanachama.
Katika uchaguzi wa mwaka huu ndani ya CCM, Mangula aliamua kugombea nafasi ya ujumbe wa Nec, lakini baadaye aliondoa jina lake ili kupisha wagombea wengine waliojitokeza kuomba nafasi hiyo.

Wasifu wa Mangula
Mangula ni kada mkongwe ambaye aliwahi pia kuwa mwalimu wa Chuo cha Chama Kivukoni kwa muda mrefu.
Pia amewahi kuwa Mjumbe wa Nec, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Tabora na Mwanza kabla ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM mwaka 1997 hadi 2006.
Mwaka 2007, aliamua kurejea katika uongozi wa chama kwa kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Mkoa wa Iringa, lakini akashindwa na Deo Sanga.
Baada ya hapo aliamua kurudi kijijini kwao, Imalinyi Wilaya ya Njombe kuendelea na shughuli za kilimo alizokuwa amezianza mara baada ya kumaliza muda wake wa utumishi ndani ya chama.

Wasifu wa Dk Shein
Dk Shein ambaye alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia Julai 13, 2001 hadi Oktoba 31, 2010 alizaliwa katika Kijiji cha Chokocho kilichopo Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba Machi 13, 1948.
Alisoma katika Shule ya Sekondari ya Lumumba iliyopo Unguja kati ya mwaka 1965 hadi 1964.
Baadaye alipata udhamini wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na kujiunga na Chuo Kikuu cha Vorenezh katika nchi iliyokuwa Muungano wa Jamhuri ya Kisoviet ya Kisoshalisti (USSR), kwa masomo ya maandalizi ya kusomea udaktari wa binadamu iliyochukua mwaka mmoja.
Dk Shein badaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Odessa, Urusi na kuhitimu Shahada ya uzamili ya tiba ya magonjwa ya binadamu (Medical Biochemistry) mwaka 1975.
Alirejea Zanzibar na kufanya kazi hiyo ya udaktari kwa miaka tisa hadi mwaka 1984, alipojiunga na masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Newcastle Upon Tyne, Uingereza alikotunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD) ya Clinical Biochemistry and Matabolic Medicine.
Aliteuliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Oktoba 29, 1995 na wiki mbili baadaye Novemba 13, aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Afya katika Serikali ya Awamu ya Tano. Kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Nchi (Ofisi ya Rais), Katiba na Utawala Bora.
Julai 13, 2001, Rais Benjamin Mkapa alimteua kuwa Makamu wa Rais baada ya kifo cha ghafla ya cha aliyekuwa akishika wadhifa huo, Dk Omar Ali Juma kilichotokea Julai 4, mwaka huo.

Minong’ono ya Sekretarieti

 
Habari zilizoenea katika maeneo mbalimbali ya Dodoma zinasema huenda Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete huenda akaingiza sura mpya katika Sekretarieti ya chama hicho.

Wanaotajwa kupewa nafasi ya katibu mkuu, Nnauye na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.
Wengine wanaotajwa kuingia katika Sekretarieti mpya ya chama hicho ni pamoja na Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja na Katibu Mkuu (UVCCM), Martine Shigela.

CHANZO: MWANANCHI

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments: