Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa,
Bernard Membe
SERIKALI imesema kuwa itafanya
mazungumzo ya mwisho na Malawi kuhusu mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa,
kabla ya kulifikisha suala hilo katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki
(ICJ) ili kupatiwa ufumbuzi baada ya pande hizo mbili kushindwa
kukubaliana.
Imesisitiza kuwa Nyasa ni urithi wa nchi tatu,
yaani Tanzania, Malawi na Msumbiji na hivyo siyo sahihi upande wowote
kati ya nchi hizo kudai unamiliki sehemu kubwa ya ziwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mara baada
ya kukutana na mabalozi wa nchi za Umoja wa Ulaya nchini (EU) katika
Ukumbi wa Karimjee Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Bernard Membe alisema kuwa tayari ujumbe kutoka Malawi
umeshafika nchini kwa ajili ya mazungumzo hayo ambayo yamepangwa
kufanyika kesho.
Waziri Membe alikutana na mabalozi kutoka nchi za
Umoja wa Ulaya kuwapa taarifa juu ya mambo yanayoendelea nchini zikiwamo
vurugu za kidini zilizojitokeza hivi karibuni.
Katika mazungumzo hayo, Waziri Membe pia
aliwaeleza wanadiplomasia hao kuhusiana na hali ya uhuru wa vyombo vya
habari nchini, uamuzi wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
(Sadc) kujihusisha mzozo unaoendelea huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo (DRC), pamoja na mzozo wa mpaka wa Ziwa Nyasa.
“Lakini pia nilikutana na mabalozi hao kuwaelezea
hali ngumu ya uchumi wa nchi za ulaya na jinsi inavyoathiri maendeleo ya
nchi za Afrika, “ alisema Waziri Membe na kuongeza kuwa:
“Timu ya Malawi ipo nchini kwa mazungumzo na
keshokutwa (kesho) kutakuwa na mkutano wa mawaziri wa Mambo ya Nje wa
nchi hizi mbili kuzungumzia chanzo cha mgogoro huu wa Ziwa Nyasa. Katika
mkutano huo tutazungumzia tunakoelekea kwa kuwa tofauti zetu zipo
wazi,” alisema Membe.
Alisema watakaoalikwa katika mkutano huo ni
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Frederick Werema na Waziri wa Sheria,
Mathias Chikawe na kwamba lengo la kuwaalika viongozi hao ni kutaka
kulikabidhi suala hilo katika vyombo vya sheria.
“Baada ya mazungumzo tutasubiri baraka za Rais
Jakaya Kikwete ambaye pia atashauriana na Rais wa Malawi, Joyce Banda
ili kukubaliana suala hili liende ICJ,” alisema Membe.
Alisema kuwa kabla ya kuchukua hatua hizo ni lazima wakutane na ujumbe huo kutoka Malawi.
“Timu ya Tanzania ambayo ipo makini inajipanga
kwenda Umoja wa Ulaya, Uingereza na Ujerumani kwa ajili ya kupata
nyaraka zote za ushahidi na baada ya hapo utaanza mchakato wa kwenda
ICJ,” alisisitiza.
Alisema kuwa mabalozi hao wamefurahia jinsi Tanzania inavyotatua mgogoro huo na Malawi kwa kutumia njia za kidiplomasia zaidi.
CHANZO: MWANANCHI
“Ziwa hili ni urithi wa nchi tatu kama ilivyo kwa Ziwa Victoria,
haiwezekani atokee mtu na kusema kuwa ziwa hili lote ni mali yake,”
alisema Membe.
Alisema katika mkutano huo pia walijadili migogoro
ya kidini nchini na kwamba mabalozi hao walishtushwa baada ya kuibuka
kwa vurugu za kidini takriban mwezi mmoja uliopita.
“Tumewaambia kuwa Serikali inahakikisha kuwa suala
hili linatoweka kabisa na kuhakikisha kwamba hakuna tena mizizi ya
mvutano wa kidini, hiyo ndio Tanzania waliyokuwa wameizoea,” alisema
Membe na kuongeza:
“Viongozi wa Serikali kila tunapokutana na
viongozi wa dini tumekuwa tukisisitiza sana amani ya nchi, hata Rais
Kikwete amekuwa akikutana kimyakimya na viongozi wa dini na kuwasisitiza
kuhusu suala zima la amani.”
Katika hatua nyingine Membe alisema kuwa vyombo
vya habari vinatakiwa kuwa makini wakati wa kuripoti matukio ya kidini,
badala yake vitafute njia ya kusuluhisha kwa sababu wapo wanaotumia
migogoro hiyo ya kidini kuhatarisha amani ya nchi.
“Tumewaeleza msimamo wa serikali kwamba lazima
vyombo vya ulinzi na usalama kuvifuatilia vikundi vinavyozuka nchini na
ikibainika vilianziswha kwa ajili ya kuleta machafuko vyombo hivyo
lazima vichukue hatua,” alisema Membe.
Alisema katika mkutano huo wamekubaliana kwa
pamoja kushughulikia migogoro hiyo ya kidini, huku mabalozi hao
wakiahidi kuieleza Serikali ukweli kama wataona mambo hayaendi sawa.
CHANZO: MWANANCHI



No comments:
Post a Comment