HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

» »Unlabelled » Ni vita CCM Dodoma

Hussein Bashe 

BASHE ASEMA MEMBE ANAKIGAWA CHAMA, WAZEE WAJA JUU WASEMA HAKUNA KUGAWA MADARAKA, KAMPENI ZAPAMBA  MOTO


VITA ya maneno ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inazidi kupamba moto, baada ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu taifa, Hussein Bashe kumtuhumu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe akisema ndiye anakivuruga chama  hicho.
Mapambano hayo yanatokea wakati wanaCCM wanakutana mjini Dodoma kwa siku tatu katika mkutano wake mkuu, ambao utachagua viongozi wa kitaifa watakaokiongoza chama hicho pamoja na wajumbe wa Nec 10 kutoka Tanzania Bara na wengine kumi kutoka Zanzibar.
Bashe pia alimtuhumu Membe kuwa anawatumia vijana wawili ndani ya chama hicho kusambaza vipeperushi vya kumhujumu mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete na kumsingizia yeye na wenzake.
Kauli ya Bashe inakuja siku moja baada ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa chama hicho kutoka Mkoa wa Morogoro, Augustino Matefu kumtaja Bashe, Makamu Mwenyekiti wa UVCCM taifa, Beno Malisa na kada wa chama hicho, Fredrick Lowassa, kuwa wanahusika kutawanya vipeperushi hivyo.
Vipeperushi hivyo, ambavyo vilitawanywa katika maeneo mbalimbali ya mji wa Dodoma vilikuwa na ujumbe unaosomeka: “CCM inayumba,  kwa pamoja tumpunguzie mzigo mheshimiwa Rais kwa kumvua  kofia moja ya uenyekiti, nina imani kwa pamoja tutashinda, piga kura ya hapana kwake, CCM oyeeee.”
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Dodoma, Bashe alikanusha taarifa hizo akisema kuwa hajawahi kufikiria kumpinga Rais Kikwete na kwamba maneno hayo ni uzushi juu yake.

“Lazima niwaambie kuwa hayo ni makundi yanayotengenezwa na baadhi ya watu, ili kunichafulia jina langu. Mwaka jana nilisema kuwa nitakuja kumtaja mtu huyo na leo namtaja kuwa ni Benard Membe, ndiye anayenisakama kupitia vijana wake,” alisema Bashe.

Alisema kuwa Membe kupitia kwa vijana wawili aliowataja kuwa ni Makonda na Matefu, alianza kumsakama tangu Aprili mwaka uliopita baada ya yeye (Bashe), kuteuliwa na UVCCM kuongoza kamati ya kutafuta maoni ya kuihuisha jumuiya hiyo.

“Kwanza lazima Watanzania wafahamu kuwa, Membe ni mwongo, asiyekuwa na msimamo wakati wote. Nilisema na leo nataka ujumbe umfikie na tayari nimeandika barua kwa Katibu Mkuu wa CCM kumjulisha hilo,” alisema Bashe.
Pia alimtuhumu waziri huyo kuwa amekuwa akiishi kwa kubebwa wakati wote akitoa mfano kuwa, mwaka 2005 alibebwa na Rostam Aziz kwa kumpatia gari lililomwezesha kwenda kuomba kura za ubunge na akapata.

Bashe pia alimtuhumu Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu kuwa ni mshirika wa Membe katika harakati hizo za kukichafua Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Nyalandu
Hata hivyo, Nyalandu alipotakiwa kuzungumzia tuhuma hizo jana, alisema: “Waongo sehemu yao ni katika ziwa liwakalo moto kwa kibiriti.”
Membe
Alhamisi wiki hii, Membe alikaririwa na gazeti hili akisema kuwa kuna kundi la watu ndani ya chama hicho, linalofanya kampeni chafu dhidi yake, lakini akasema kwamba hujuma hiyo haitafanikiwa, badala yake atashinda kwa kishindo katika uchaguzi wa Nec.
''Nakubaliana kabisa kwamba ziko njama za kunihujumu, ambazo hata mimi nazijua. Lakini wabaya wangu hao, wanafanya jambo ambalo hawalijui, kama wangejua wasingepoteza muda huo,'' alisema Membe.
Alijifananisha na mwembe, ambao hutupiwa mawe wakati wote kuliko mchongoma wenye miiba aliosema hauwezi kutupiwa mawe kwani hauna kitu cha kuchukua juu yake.

Wazee wanena

 
Baraza la Wazee wa CCM, Wilaya ya Dodoma Mjini jana walipinga kauli zinazotolewa na baadhi ya watu kutaka madaraka ya Mwenyekiti wa chama hicho taifa yatenganishwe.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Mwenyekiti wa Baraza hilo, Balozi Job Lusinde, alisema kuwa siyo jambo la busara hata kidogo kutenganisha nafasi hizo.
Lusinde alisema kwamba ni vyema Rais akaachwa kuendelea na shughuli zake pamoja na kofia zote mbili kwa kuwa ndiyo msingi na kanuni za chama.
 

Nec Vijana
 
Kwa upande wao wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM kupitia kundi la vijana, walisema kuwa watamlinda kwa gharama yoyote Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete pamoja na kuhakikisha kuwa anapata kura zote za ‘ndiyo.’
Mbali na hilo, vijana hao walisema kuwa watafanya kila njia kumsaka mtu aliyetengeneza vipeperushi hivyo vinavyosambazwa dhidi ya mwenyekiti wao,  Rais Jakaya Kikwete.
Wajumbe hao saba kati ya kumi waliitisha mkutano na waandishi wa habari katika Ofisi za CCM Mkoa wa Dodoma na kutoa tamko hilo, huku wakieleza kuwa hawatalala hadi watakapoona mwenyekiti wao akiibuka na ushindi wa kishindo.
“Sisi ndiyo jeshi la chama. Itakuwa ni aibu kama mwenyekiti wetu atakuwa akidhalilishwa kwa kupata kura chache, ilhali nasi tupo. Lazima kuwaaibisha watu wa aina hiyo na kuwasaka popote walipo. Tunaomba vijana wenzetu watuamini kuwa tuko Dodoma kufanya kazi hiyo,” alisema Jery Silaa kwa niaba ya wenzake.

CCM Kagera
Naye Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Kagera,  Hamimu Omary,  amekanusha uvumi uliozagaa kuwa Mkoa wa Kagera ni mmoja ya mikoa inayounga mkono mkakati wa kumhujumu Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete.

Alisema kitendo cha kupiga kura za hapana kwa Rais Kikwete hakimdhalilishi mwenyekiti huyo peke yake, bali kinawadhalilisha viongozi wote ndani ya chama hicho.
Alitaka watakaobainika kushiriki katika mpango huo wachukuliwe hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kufukuzwa uanachama.
Omary alisema kuwa wajumbe wa mkutano mkuu wamefika katika mkutano huo wa uchaguzi kwa ajili ya kujipanga katika kukiimarisha chama na siyo kuchafuana.
Mkoa wa Shinyanga

Akizungumza kuhusu tuhuma hizo za kutaka kumchafua Kikwete, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa Shinyanga John Mgeja, alipasua jibu akimtaja waziri mmoja wa wizara nyeti nchini kuwa ndiye anahusika katika kuandaa mpango huo.

Mgeja alisema kuwa, amepata majina ya watu wote waliohusika kuandaa mchezo huo mchafu dhidi ya Rais Kikwete na kwamba wanaongozwa na waziri huyo anayedaiwa kushirikiana na kigogo mkubwa ndani ya CCM ambaye ni mjumbe wa Sekretarieti ya chama hicho.

Vita
Katika uchaguzi wa chama hicho tawala vita ni kubwa katika kuwania nafasi 10 za ujumbe wa Nec, ambapo mawaziri sita ni miongoni mwa wanachama 31 upande wa Bara watakaopambana kuwania nafasi hizo.

Kwa upande wa Zanzibar vita hiyo inawakutanisha wanachama 28 wanaowania nafasi 10 za Nec wakiwamo mawaziri wanne.

Mbali na mawaziri sita, nafasi 10 za Tanzania Bara pia zinawaniwa na wabunge watatu, mkuu wa wilaya mmoja na vigogo wawili wa Kamati Kuu ya chama hicho.

Kwa upande wa Zanzibar pamoja na mawaziri wanne yumo pia Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi.


Kampeni za lala salama
 
Mji wa Dodoma na vitongoji vyake umefurika wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM, huku wagombea wa ujumbe wa Nec wakifanya kampeni zao za mwisho.
Kampeni zinafanyika usiku na mchana kwa wapambe wa wagombea kupita kila kona walipo wajumbe wa mkutano mkuu wakiomba kura.
Baadhi ya wagombea wamebuni mbinu mpya ya kufanya kampeni kwa kubandika migongoni karatasi zenye picha za wapambe wao zinazoelezea wasifu wao ili kuwafanya watu wanaokutana nao kuona kwa urahisi.
Waandishi wa gazeti hili jana walishuhudia vijana wengi wakirandaranda katika uwanja wa majengo ya Makao Makuu ya chama hicho wakiwa wamebandika karatasi za wasifu wa wagombea wao migongoni.
Jana, takriban wagombea wote wa Nec, walikuwa wakipita kwa baadhi ya wajumbe waliokuwa katika viwanja vya majengo ya makao makuu wakiwasalimia na kuomba kura.


CHANZO: MWANANCHI

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments: