Chungu na tamu ya vigogo 2012
BAADHI ya vigogo wa kisiasa hawatasahau
yaliyowapata mwaka jana kutokana na mabadiliko makubwa yaliyoigusa
medani hiyo na kusababisha kuanguka ama kwa kura au kung’olewa katika
nafasi walizokuwa wakizishikilia.
Wakati baadhi wakiugulia kwa machungu hayo, kwa
upande mwingine lipo kundi la wale wanaosherehekea neema iliyowajia
mwaka huohuo, baada ya nyota zao kung’ara kisiasa na kujikuta wakikwaa
nafasi za uongozi, pengine ambazo hawakuzitarajia.
Miongoni mwa matukio yaliyowatikisa wanasiasa ni
hatua ya Rais Jakaya Kikwete kupangua Baraza la Mawaziri, kutenguliwa
kwa baadhi ya matokeo ya chaguzi za wabunge na uchaguzi wa ndani wa CCM
ambao uliwaweka kando baadhi ya vigogo wa chama hicho.
Kadhalika, yapo matukio yenye sura ya kipekee
ambayo yanawagusa wanasiasa kama Godbless Lema ambaye alianguka kisiasa
kwa ubunge wake kutenguliwa na Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha mwanzoni
mwa mwaka jana, lakini akaibuka tena shujaa baada ya kurejeshewa nafasi
hiyo na Mahakama ya Rufani, Desemba 2012.
Tukio kubwa ambalo lilitikisa siasa za Tanzania ni
lile la mabadiliko katika Baraza la Mawaziri ambayo yaliwaweka kando
mawaziri sita ambao walikuwa wakiziongoza wizara nyeti zinazosimamia
rasilimali za nchi na huduma za afya na uchukuzi.
Waliong’olewa ni Mustafa Mkulo (Fedha), William
Ngeleja (Nishati na Madini), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), Omari
Nundu (Uchukuzi), Dk Cyril Chami (Viwanda na Biashara) Dk Haji Mponda
(Afya na Ustawi wa Jamii). Pia panga hilo liliwakumba waliokuwa Naibu
Mawaziri, Dk Lucy Nkya (Afya na Ustawi wa Jamii) na Dk Athuman
Mfutakamba (Uchukuzi).
Kuanguka kwa Mkulo, Ngeleja na Maige kulitokana na
taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
iliyozihusisha wizara zao na ufisadi. Dk Mponda na Dk Nkya, waling’olewa
kutokana shinikizo la madaktari ambao walifanya mgomo uliotikisa sekta
ya afya nchini.
Kwa upande wake, Nundu naibu wake, Dk Mfutakamba
waling’olewa kutokana na kashfa ya ujenzi wa gati bandarini ambao
uliwagawa kiasi cha kutofautiana bungeni, wakati Dk Chami naye aliponzwa
na ugomvi na aliyekuwa naibu wake, Lazaro Nyalandu. Hata hivyo Nyalandu
alipona baada ya kuhamishiwa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Walioula
Mabadiliko hayo yalikuwa neema kwa wateule wapya
wakiwamo wale ambao hawakuwahi kuwa wanasiasa kama ilivyo kwa Profesa
Sospeter Muhongo ambaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Nishati na Madini.
Profesa Muhongo alipewa naibu wawili; George Simbachawene (Nishati) na Stephen Masele (Madini) ambao walikuwa wabunge.
Wabunge wengine walioula ni Dk William Ngimwa
ambaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha na kupewa naibu wawili ambao nao
hawakuwa katika duru za kisiasa; Saada Mkuya Salum na Janeth Mbene. Ni
wakati huohuo ambao Mwenyekiti wa NCCR -Mageuzi, James Mbatia aliteuliwa
na Rais kuwa mbunge.
MWANANCHI
Mbunge wa Handeni, Dk Abdallah Kigoda naye aliteuliwa kuwa
Waziri wa Viwanda na Biashara, katika mabadiliko ambayo pia yalishuhudia
baadhi ya waliokuwa naibu mawaziri wakipanda vyeo na kuwa mawaziri
kamili.
Hao ni Dk Harrison Mwakyembe aliyeteuliwa kuongoza
Wizara ya Uchukuzi, Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki,
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara na
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza.
Kabla ya uteuzi huo, Dk Mwakyembe alikuwa naibu
katika Wizara ya Ujenzi, Kagasheki katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya
Nchi na Chiza alikuwa naibu katika wizara hiyohiyo kama ilivyokuwa kwa
Dk Mukangara aliyekuwa Habari na kupandishwa kuchukua nafasi ya Dk
Emmanuel Nchimbi ambaye alihamishiwa Mambo ya Ndani, kuchukua nafasi ya
Shamsi Vuai Nahodha aliyehamishiwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa.
Nahodha alichukua nafasi ya Dk Hussein Mwinyi ambaye alihamishiwa Afya.
Katika mabadiliko hayo wabunge wengine waliteuliwa
kuwa naibu mawaziri ambao ni Angela Kairuki (Katiba na Sheria), Januari
Makamba (Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia), Dk Seif Selemani Rashid
(Afya na Ustawi wa Jamii), Dk Binilith Mahenge (Maji), Dk Charles Tzeba
(Uchukuzi) na Amos Makala (Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo).
Mawaziri wengine waliohamishwa ni George Mkuchika,
Profesa Jumanne Maghembe, Profesa Mark Mwandosya, Hawa Ghasia, Celina
Kombani na Sofia Simba.
Naibu mawaziri waliohamishwa ni Gregory Teu, Pereira Ame Silima, Adam Malima, Charles Kitwanga na Gerson Lwenge.
Uchaguzi CCM
Uchaguzi wa ndani wa CCM nao ulisababisha
mtikisiko kwa baadhi ya vigogo wa kisiasa akiwamo, aliyekuwa Katibu
Mkuu, Wilson Mukama ambaye aling’olewa katika mabadiliko ya sekretarieti
yaliyofanywa baada ya uchaguzi huo.
Tukio kubwa katika uchaguzi huo lilikuwa kurejea
katika siasa za CCM kwa aliyepata kuwa Katibu Mkuu wake, Philip Mangula
ambaye alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti (Bara), kuchukua nafasi ya
Pius Msekwa ambaye tayari alikuwa ameomba kutoendelea na wadhifa wake.
Kadhalika Abdulrahman Kinana aliteuliwa kuwa
Katibu Mkuu wa CCM huku aliyekuwa Mtunzahazina wa chama hicho, Lameck
Mwigulu Nchemba akipanda cheo na kuwa Naibu Katibu Mkuu (Tanzania Bara).
Katika mabadiliko ya Sekretarieti, pia Zakia
Meghji aliteuliwa kuwa Mtunzahazina wakati aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu
wa Umoja wa Mataifa, Dk Asha-Rose Migiro aliteuliwa kuwa Katibu wa Siasa
na Uhusiano wa Kimataifa wa chama hicho.
Katika ngazi za mikoa na jumuiya za chama hicho, aliyekuwa
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita aliangushwa huku
Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Makongoro Mahanga naye akiangushwa
katika kuwania ujumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) kupitia Wilaya ya Ilala.
Matukio mengine
Mwaka jana, Bunge lilipoteza wabunge wawili ambao
ni aliyekuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki (CCM), Jeremiah Sumari na
aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Regia Mtema.
Kifo cha Sumari kilisababisha kufanyika kwa
uchaguzi mdogo mwanzoni mwa Aprili ambao ulimwingiza bungeni, aliyekuwa
mgombea wa Chadema, Joshua Nassari baada ya kumshinda Sioi Sumari wa CCM
kwa kura zaidi ya 6,000.
Cecilia Pareso wa Chadema, aliingia bungeni kuchukua nafasi ya Mtema.
Hata hivyo, wabunge wawili wa CCM; Aeshi Hilal
(Sumbawanga Mjini) na Dk Dalaly Kafumu (Igunga) wameingia mwaka mpya
wakiwa nje ya Bunge baada ya matokeo yaliyowapa ushindi kutenguliwa na
Mahakama Kuu, uamuzi ambao wameupinga katika Mahakama ya Rufani.
Post a Comment