Yule mtu aliyedaiwa kuwa ni mwanajeshi wa JWTZ wa kikosi cha
Monduli ametiwa mbaroni leo kwa ushirikiano wa jeshi la wananchi na
Police.
Uchunguzi wa awali umebaini kuwa kijana huyu hakuwa mwanajeshi wa JWTZ
kama alivyojitambulisha kwa waandishi wa habari ila aliwahi kuwa JKT na
akaacha, ila amekuwa akivaa ngua hizo za jeshi kwa miaka mingi na
wananchi wa Mererani wanamtambua kama mwanajeshi.
Maswali ya kujiuliza
Inakuwaje raia anavaa nguo za jeshi kwa miaka mingi bila kuchukuliwa hatua, hayo mavazi kayapata wapi?
Je, Lema asingepiga picha naye angejulikanaje kuwa ni raia anavaa nguo za jeshi na kujitambulisha kama mwanajeshi?
KIJANA aliyepiga picha na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless
Lema, akiwa amevalia sare za Jeshi la Wananchi (JWTZ) katika mkutano wa
mbunge huyo uliofanyika Mererani mkoani Manyara na kujitambulisha kuwa
anatoka kikosi cha Monduli, amekamatwa na Jeshi la Polisi mkoani
Kilimanjaro juzi baada ya kusakwa kwa siku kadhaa.
Kijana huyo alionekana pichani akiwa amenyoosha vidole viwili kama
ishara ya alama inayotumiwa na CHADEMA, na hivyo uongozi wa JWTZ makao
makuu kutangaza kumsaka na kumhoji ili kujiridhisha kama ni askari wao,
waweze kumchukulia hatua kutokana na kushabikia siasa akiwa amevalia
sare za jeshi.
Pia JWTZ walieleza kutilia shaka sare zake wakidai kuwa walishaacha
kuzitumia kwa muda mrefu na kwamba kikosi cha Monduli
alichojitambulisha kuwa anatoka hakikutajwa jina.
Taarifa zilizoifikia Tanzania Daima, zilieleza kuwa kijana huyo
ambaye jina lake bado halijafahamika, alitiwa mbaroni eneo la Boma
Ng’ombe na kuhifadhiwa katika kituo cha polisi mjini hapo wilayani Hai.
Hata hivyo, licha ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Akili Mpwapwa
na Msemaji wa JWTZ, Kanali Kampambala Mgawe, kukiri kukamatwa kwa
kijana huyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, alikana
akisema hana taarifa za kukamatwa kwake.
Licha ya Kamanda Boaz kukwepa kulielezea tukio hilo, taarifa
zilizoenea kwenye mitandao ya kijamii na kwa baadhi ya wananchi mkoani
humo, zilisema kijana huyo alikamatwa na alikuwa akihojiwa na maofisa wa
JWTZ kutoka makao makuu.
“Mimi nipo kwenye mkutano na nimefanya heshima kukupokelea simu yako,
hizo taarifa za kukamatwa huyo kijana unazosema zimetokea jana mimi
siwezi kujua kwani tokea juzi sina taarifa ya kilichotokea,” alisema
Boaz.
Taarifa za awali zilisema kuwa kijana huyo si askari wa JWTZ kama
alivyokuwa akijitambulisha kwa watu na kuvalia sare za jeshi hilo, bali
alikuwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), ambapo hata hivyo alishaacha kazi
hiyo.
Akizungumzia kukamatwa kijana huyo, Mbunge wa Arusha Mjini, Lema,
alisema kama suala hilo ni kweli basi Watanzania wapo katika hatari
kubwa na aibu kwa serikali nzima.
Aliongeza kuwa, ikiwa kijana huyo si askari, ni dhahiri kwa sasa kuna
watu wengi wenye kuvaa mavazi ya majeshi tofauti ya Tanzania na
kufanya kazi zinazofanywa na askari pasipo kutambuliwa na vyombo vya
ulinzi na usalama.
“Kama mtu anaweza kuvaa nguo ya jeshi mbele ya hadhara na akakaa na
polisi wetu pasipo kujulikana, unafikiri Watanzania wataendelea kuwa
salama?” alihoji Lema.
TANZANIA DAIMA



No comments:
Post a Comment