HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

» »Unlabelled » Tukio la watu kuzikwa hai lazua mambo

Mabaki ya nyumba za marehemu Ernest Mholela zilizobomolewa kabla ya kumzika akiwa hai kutokana na kutuhumiwa kuwa mchawi.  Picha na Stephano Simbeye 
Na Brandy Nelson, Mbeya   (email the author)
KUTOKANA na  tukio la watu wawili kuzikwa  wakiwa  hai  hivi karibuni Wilaya ya Mbozi, wazee  mkoani  Mbeya wameiomba  Serikali kuandaa utaratibu wa kutoa ulinzi hasa kwa watu   waliopo vijijini.
Wamesema matukio kama hayo yamewajengea  woga  na kusababisha kuishi kwa hofu hali inayosababisha kushindwa kufanya kazi zao za kila siku na kushiriki katika shuguli za kijamii vizuri.
Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili kwa niaba ya wazee  hao, Abel  Ambakisye  alisema tukio hilo limekuwa tishio kwa wazee hasa waishio vijijini na kuleta sifa mbaya ya Mkoa wa Mbeya  kuwa  ni eneo lenye matukio mabaya.
“Suala hili ni kubwa na baya kwa mkoa wetu, kwani linatutisha sisi wazee kuona watoto na vijana wetu wanatufanyia vitendo vya kinyama kama hiki kilichotokea hivi karibuni cha kuwazika watu wawili wakiwa  hai,” alisema.
Aliongeza kuwa “Huu ni unyama hivyo Serikali kupitia polisi inapaswa kuhakikisha wanafanya uchunguzi wa kina na kuandaa utaratibu maalumu wa kutupatia ulinzi ili tuweze kuishi kwa amani”.
Alisema huko nyuma Mkoa wa Mbeya ulisikika kwa kuwa na matukio ya uchunaji ngozi watu na upigaji nondo, kitendo ambacho kilisababisha watu wengi kutoka nje ya Mkoa wa Mbeya kuuogopa mkoa huu.
“Lakini Serikali kupitia polisi walikomesha vitendo hivyo, sasa  havipo tena, nguvu hizo sasa zielekezwe katika kupambana na matukio kama haya ya kuwazika watu wakiwa wazima”alisema.
“Tunaomba  Serikali ya kijiji pia ihusike katika kuvisaidia vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, kuhakikisha wazee wanakuwa na ulinzi ili waweze kuishi kwa amani na utulivu na kushiriki  katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya jamii bila kubughudhiwa,” alisema.
Aliongeza kuwa wazee wanatarajia kuonana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani kwa ajili ya kuwasilisha maombi yao na kujadiliana jinsi ya kukabiliana na tatizo hilo na kuangalia mbinu za kufanya ili kulikomesha.
Ambakisye  alisema wananchi wa  Mkoa  Mbeya  wanahitaji kufanya mikakati mbalimbali ya kuleta maendeleo, lakini vitendo kama hivi vinarudisha nyuma jitihada hizo.
“Kwani hata wawezekezaji wataogopa kuja hapa mkoani kwetu kuwekeza, kwa kuwa sifa kubwa inayotangazika mkoani kwetu ni vitendo vya kinyama na hivyo kujenga hofu miongoni mwa wawekezaji,” alisema.

MWANANCHI

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments: