Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo Februari 24, 2013 ameungana na Wakuu wenzake wa Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu kutia saini Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Amani, Usalama na Ushirikiano katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Mhe. Rais Kikwete alisema mara baada ya utiwaji saini wa Mpango huo kwamba: “Hii ni siku kubwa na ya kihistoria kwa watu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, jirani zake na Ukanda wote wa Maziwa Makuu. Ni siku ya kukumbukwa kwa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), Afrika, Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa na Jumuiya yote ya Kimataifa. “Watu wa Kongo wameteseka kwa muda mrefu sana. Wanastahili kupumua sasa. Wanastahili kuishi maisha
bora; maisha ambayo usalama wao umehakikishiwa na kuthibitishwa; maisha
ambayo yatawafanya waendeshe maisha yao kwa kufanya mambo ya maana
zaidi katika kuboresha maisha yao ya kila siku.
“Saini
tulizotia kwa Mpango huo leo ni kielelezo cha dhati na ahadi ya
utekelezwaji wa yale yanayotarajiwa na watu wa Kongo na Ukanda wa
Maziwa Makuu kwa ajili ya Amani, Usalama na Ushirikiano.
“Kwa
niaba ya Serikali na Watu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania naahidi
kwamba sisi tutatekeleza kwa dhati yale yote yanayotarajiwa kwa upande
wetu”, alisema.
Mpango
huo umetiwa saini na viongozi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
(DRC), Jamhuri ya Uganda, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Angola,
Jamhuri ya Burundi, Jamhuri ya Kongo (Brazaville), Jamhuri ya Zambia,
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Jamhuri ya Afrika Kusini.
Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mhe. Ban Ki-moon, Mwenyekiti wa Kamisheni ya
Umoja wa Mataifa, Dkt. Nkosazana Dlamini-Zuma, pamoja na wenyeviti wa
Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Ukanda wa Maziwa
Makuu (ICGLR) wametia saini Mpango huo kama mashahidi na wadhamini.
Mpango
huo una nia ya kuchangia juhudi ambazo zimefanywa na ICGLR na SADC
katika kutafuta amani Mashariki ya Kongo na ukanda wote wa Maziwa Makuu
kwa ujumla.
Mpango
huo pia umetilia maanani mapendekezo muhimu yaliyokubalika baada ya
mashauriano kati ya wakuu wa nchi za ICGLR na SADCna Katibu Mkuu wa
Umoja wa Mataifa.
Mapendekezo
ya mpango huo ni pamoja na kuboresha sekta ya Ulinzi na usalama,
hususan jeshi la polisi, Kuimarisha mamlaka ya nchi hasa mashariki ya
Kongo; na kuendeleza ajenda kuhusu maelewano, kuvumiliana na kudumisha
demokrasia nchini humo.
Vile
vile, nchi za Kanda zimetakiwa kutoingilia mambo ya ndani ya nchi
jirani, kututoa msaada wowote wa vikundi vya waasi, kuheshimu utawala na
maeneo ya nchi jirani na kuimarisha mahusiano ya Kanda.
Hali
kadhalika, Jumuiya ya Kimataifa imetakiwa kuisaidia DRC na Kanda yote
ya Maziwa Makuu kwa ujumla katika utekelezaji wa miradi muhimu pamoja na
mkataba wa Amani, Usalama na Maendeleo katika Ukanda wa Maziwa Makuu.
Aidha,
Mpango huo unapendekeza kuwepo kwa chombo cha usimamizi (Oversight
Mechanism) ambacho kitaundwa na viongozi wote wa nchi 11 pamoja na Umoja
wa Mataifa, SADC na ICGLR.
“Mwisho”
Imetolewa na:
Muhidin Issa Michuzi,
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi,
Addis Ababa,
ETHIOPIA.
24 Februari, 2013
Post a Comment