Dk Mwakyembe, Serukamba vitani

Waziri wa Uchukuzi Dk Harrison Mwakyembe 



Dodoma. Waziri wa Uchukuzi Dk Harrison Mwakyembe ameingia katika msuguano wa chinichini na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Peter Serukamba ambaye alidaiwa kuongeza maneno kwenye hotuba ya kamati yake yaliyokuwa yakimlenga waziri huyo binafsi.
Kutokana na hali hiyo, hotuba iliyokuwa isomwe na Serukamba kama maoni ya kamati baada ya Dk Mwakyembe kuwasilisha hotuba yake, ilibadilishwa dakika za mwisho na kusainiwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Profesa Juma Kapuya.
Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo (ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe) alisema waliamua kuunda kamati ndogo ya wabunge wanne kusahihisha lugha iliyotumika katika kuandaa maoni ya kamati hiyo kuhusu Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi kwa Mwaka wa Fedha wa 2013/2014.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, wajumbe waligundua kuwa lugha iliyotumika ililenga kushambulia moja kwa moja Dk Mwakyembe ndani ya Bunge jambo ambalo lilkuwa kinyume cha makubaliano ya kamati.
Hata hivyo, Serukamba akizungumza na gazeti hili alikana kubadili hotuba hiyo na kuongeza kuwa; “Mimi nimerudi jana, kwa kawaida kamati ikishajadili suala la hotuba kuandikwa tunamwachia Katibu na akimaliza anairudisha kwetu wabunge. Hivyo nilichokisoma ndicho tulichokubalina na wajumbe wa kamati hiyo.”
Aliongeza: “Msitake kunigombanisha na mheshimiwa Waziri, mimi ndiyo kwanza nimeingia asubuhi hii hakuna kilichobadilika katika hotuba hiyo.”
Gazeti hili lilifanikiwa kuona nakala mbili za hotuba za kamati, moja ikiwa na saini ya Serukamba na nyingine ikiwa imesainiwa na Profesa Kapuya na zote zina tarehe inayofanana ambayo ni Mei 16, 2013.
Kwa upande wake Kapuya katika majibu ya maandishi kwa gazeti hili alisema si kweli kwamba ziliandikwa hotuba mbili. “Habari hizo hazina ukweli, kamati yangu ina utaratibu wa kuandaa hotuba yetu na ikishakamilika tunateua kamati ndogo ambayo inapitia hotuba hiyo kabla ya kuisoma,”alisisitiza Profesa Kapuya.
Majibu ya Serukamba na Kapuya yanatofautiana na kauli ya Dk Mwakyembe ambaye aliliambia gazeti hili kwamba pia alipata taarifa za kuwapo kwa mpango huo kutoka kwa “watu wanaojua na kuthamini kazi yake.”
“Siyo kila mtu anaweza kukuchukia huwezi kunyimwa maneno, watu wenye imani na mimi walikuja kunipa taarifa na wakanipatia ile aliyokuwa ameandika yeye…. ana bahati sana nilikuwa namsubiri kwa hamu aisome hiyo hotuba yake nilipanga kumchanachana pale pale asingeamini,”alisisitiza Dk Mwakyembe.
Alipoulizwa kwa nini anafikiri mwenyekiti huyo ameamua kumfanyia hivyo, Dk Mwakyembe alisema; “Siwezi kujua lakini naamini hizi ni mbio tu za mwaka 2015.”
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema hafahamu kuhusu suala hilo. “Ninachofahamu ni kwamba Serukamba alikuwa amesafiri kwenda China na mimi nilimwona siku hiyo akisoma maoni ya kamati yake, kama kulikuwa na tatizo hilo pengine litakuja baadaye ofisini kwetu,”alisema Ndugai kwa simu.
Ilikuwaje?
Habari zinasema licha ya kwamba Serukamba alikuwa nje ya nchi, alihusika katika kuandaa rasimu ya awali ya taarifa ya kamati ambayo yeye alisaini.
Hata hivyo wakati akiwa bado hajarejea nchini, wajumbe wa kamati yake walibaini kwamba katika hotuba hiyo kulikuwa na lugha ya kumuhoji zaidi waziri pamoja na Serikali badala ya kushauri, huku baadhi ya kauli zikionyesha kumlenga Dk Mwakyembe binafsi.
Wajumbe hao walilalamika kwamba maneno hayo yaliyokuwa yakimshambulia waziri ni kinyume na walivyokubaliana hivyo waliamua kuunda kamati ya watu watatu ambao ni wajumbe wa kamati hiyo ili kufanya marekebisho.
“Hatua ya kuunda kamati hiyo ndogo ilifikiwa Jumatatu wiki hii, maana tulibaini kwamba lugha iliyotumiwa haikuwa sahihi, sisi kazi yetu ni kuishauri Serikali na si kuhoji maswali, maswali unaweza kuhoji wakati wa kuchangia mbunge mwenyewe lakini si kwa kuandika katika maoni ya kamati, “kilieleza chanzo hicho.
Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge toleo la 2007 ya 114(18), Kamati ya Kudumu ya Bunge inaweza kuunda kamati ndogo kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli zake, kadri itakavyoona inafaa na kila kamati ndogo itapangiwa kazi zake na kamati ya kudumu husika.
Wajumbe hao ni Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Ramo Makani na Wabunge wa Viti Maalumu, Rita Kabati na Zarina Madabida wote wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Hotuba hiyo baada ya kukamilika ilisainiwa na Profesa Kapuya na hiyo ndiyo iliyosomwa bungeni.


MWANANCHI

No comments

Powered by Blogger.