NANI amechafua hali ya hewa? Hii ni kauli inayoulizwa mara
kwa mara katika matukio yanayokutanisha jamii pamoja na sehemu za majumbani
ikiwa ni utaratibu wa kimaisha.
Lady Jay De
Katika suala muziki wa kizazi kipya, swali hili naweza
kuliuliza kila ninaposikia malalamiko ya wasanii dhidi ya watu Fulani, iwe ni
Kampuni, taasisi au kikundi cha watu wachache.
Ruge Mutahaba, Mkurugenzi wa Utafiti na Matukio wa Clouds Media Group
Sugu
na Ruge siku walipokutana kwa mara ya kwanza na kusawazisha mgogoro
wao. Kulia ni Tundu Lissu wakati kushoto ni aliyekuwa Waziri wa Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo sasa Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel
Nchimbi.
Kauli ambayo mara kadhaa pia najaribu kuifananisha na
hadithi ya mbwa mwenye mnofu mdomoni. Ngoja niiweke wazi kauli hii. Siku zote
mbwa mwenye mnofu hawezi kubweka.
Mkurugenzi Mtendaji wa Clouds Media, Joseph Kusaga
Ni mpole anayejilia vyake. Ila inapotokea mnyama huyo ambaye
kwa kawaida ameumbwa na kubarikiwa ukali mnofu wake unatolewa ndipo anapoanza
balaa.
Kwa wiki kadhaa sasa, msanii maarufu wa muziki wa Bongo
Fleva, Judhithi Wambura Lady Jay Dee amekuwa akiwatuhumu watu, hasa mabosi wa
Clouds Media Group kuwa wanawanyonya wasanii.
Ni kauli ambayo kwa kawaida imekuwa ikisemwa mara kadhaa na
watu ambao, ama katika suala hilo, wamekuwa wakisema bila kuangalia chimbuko
halisi la malumbano.
Kwa umri wangu mdogo niliokuwa nao, nimeweza kusikia
malumbano ya Clouds na baadhi ya wasanii na kujikuta nikibaki mdomo wazi.
Malumbano hayo yaliasisiwa na msanii wa Hip Hop ambaye kwa sasa ni Mbunge wa
Mbeya Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Joseph
Mbilinyi, maarufu kama Sugu.
Huyu kweli ni Sugu, maana umwamba wake ulionekana, ingawa
baadaye muafaka ulitangazwa kwa Sugu na wahusika wa Clouds, akiwapo Ruge
Mutahaba kumaliza matatizo yao.
Katika hilo, najaribu kufikiria kuwa kama watu hao walifikia
muafaka, ina maana zile tofauti zilizokuwapo awali, zimefikia tamati, huku
nikiamini kuwa matawi yote yalivunjwa pamoja na kuimarishwa ushirikiano kwa
ajili ya muziki nchini.
Ikumbukwe kuwa, kabla ya muafaka wa Sugu na wadau wa Clouds,
kulikuwa na matusi, kashfa nyingi zilizotengenezwa ili kufikisha kilio au
kuonyesha umwamba wao.
Tuliwahi kusikia au kuona hata kwenye mitandao kukiandaliwa
video za matusi kama njia za makombora ya vita hivyo. Hata hivyo, wakati ambapo
sasa hali imetulia, anaibuka tena Jay Dee kwa tuhuma zilizofanana na Sugu na
wadau wake.
Si lengo kuchochea moto huo, ila najiuliza swali, wakati
wote wa Sugu analalamikia vitendo alivyoita vya kidhalimu, huyu mwanadada
alikuwa wapi? Je, ni kweli kuwa wakati huo wa ukimya wake alikuwa na mnofu
mdomoni?
Je, ni kweli kuwa sasa mnofu huo haupo kinywani mwake na
kuona njia nzuri ni kuibuka kusipojulikana na kuanza kurusha matusi dhidi ya
watu anaowaita wanyonyaji wa haki za wasanii.
Nasema tena, katika suala zima la uchambuzi wa sakata hili,
kila mmoja yupo huru kuzungumza kila anachokiamini kwa faida ya sanaa na
wasanii wetu wa Tanzania.
Binafsi, nimeshangazwa na maneno ya Jay Dee na hakika
ameonyesha namna wasanii wasivyokuwa na mawazo endelevu kwa ajili ya kazi zao.
Badala yake, wamebakia kuwa watu wa kutoa lawama hata kwa vitu ambavyo
havistahili.
Kwa mfano, unaweza kujiuliza swali hili. Msanii analalamikaa
kuwa Clouds inambania kazi zake. Swali, hawa Clouds wanafanya kazi za kufanana
hadi na vituo vya Redio vya Radio One, TBC Taifa, TBC FM, Capital Redio, Uhuru
FM, Times FM na nyinginezo zote za jijini Dar es Salaam pamoja na mikoa yote
kulikozagaa vituo vya redio.
Kwa maana hiyo, kama msanii Mr Blue, Dogo Janja, Madee, Juma
Nature na wengineo wanalalamikia dhuluma au kubaniwa na Clouds, wana uwezo wa
kupekeleka nyimbo zao kwingine na bado maisha yao yakaenda kama kawaida.
Juu ya suala zima la kupunjwa kwenye shoo zinazoandaliwa na
Clouds, likiwapo Tamasha lao la Fiesta linalofanyika kila mwaka, pia si lazima
msanii alipwe fedha asizopenda.
Kama Profesa Jay, Fid Q, Linah Sanga, Mwasiti na wengineo
wanaona shoo zao hazilipi, wana wajibu wa kukataa na sio kufanya kwa shingo
upande au baadaye kuja kutoa maneno ya kashfa.
Labda wasanii hawajajua mbaya wao. Wasanii tatizo kubwa halipo
kwa Clouds na Ruge Mutahaba au Mkurugenzi wao Joseph Kusaga dhidi ya kashfa
wanazopewa kila kukicha.
Tatizo kubwa lipo kwa serikali kushindwa kuweka mifumo
mizuri kwa ajili ya jasho la wasanii. Tujiulize, hawa Clouds ndio wasambazaji
wa kazi zote za wasanii?
Jibu si kweli. Kumbe serikali pia inaweza kuweka mfumo mzuri
wa kuweka mtambo wa kudurufu kazi za wasanii, kuhakikisha kuwa kila kazi
inakuwa na stika kuonyesha uhalali.
Ndio wizi wa kazi upo, lakini si kweli kuwa kila msanii
anastahili kuwatukana watu wanapoingia kwenye migogoro ya kibiashara. Lady Jay
Dee aliwahi kuwa mfanyakazi wa Clouds FM kabla ya kuingia kwenye sanaa na
kupata mchango mkubwa wa wadau wake.
Hata kama leo Jay Dee akikataa, lakini Mungu anajua, ndio
maana bado nyimbo zake zinapigwa Clouds. Wasanii wa Tanzania ili wafanikiwe
kila mmoja ahakikishe kuwa anaacha fitina na kutenda kazi kama inavyotakiwa kwa
ajili ya kuinua kiwango cha sanaa.
Ajabu, wapo wanaoingia kwenye migogoro hii, huku ukiangalia
nyimbo zake, hazina ubora kuanzia audio hadi video. Sina shaka na uwezo wa Jay
Dee, ila wakati wote huo alikuwa wapi?
Kwanini wenye akili zao wasimcheke ujinga? Vipi wale
waliojitoa mhanga kwa ajili ya huo wizi unaotajwa kila kukicha? Hatuwezi kwenda
hivyo. Kuna mengi yapo chini ya pazia.
Na kama kila mmoja mwenye nafasi ya kusema akipewa nafasi
hiyo, utakuja kugundua kuwa kilichopo si kilio cha wasanii, bali
wafanyabiashara, ambao wamegundua ili kuendelea kunyonya damu za wasanii,
lazima wawagombanishe watu.
Kwa mfano, kama leo kuna mtu anagonga ‘copy’ za wasanii,
hakika ataendelea kuifanya kazi hiyo kwa kujiamini, maana wasanii wakubwa
wanaendekeza fitina na porojo zisizokuwa na mpango wowote kwa namna moja ama
nyingine.
Kuna kila sababu ya kujisahihisha kwa wasanii wetu. Waone
kuwa tatizo lao halipo kwa Clouds na wanaojaribu kupita njia za panya
kuwagombanisha au kujigombanisha wenyewe suala hilo likomeshwe kwa ajili ya
maisha ya sanaa na wasanii.
Naumizwa mno na tabia hii, hivyo kuna haki sasa wasanii
kuwekeza zaidi kwenye kazi zao kwa kutunga nyimbo nzuri, kufanya shoo za aina
yake na kujitanua Kimataifa, badala ya kuweka porojo matusi, zisizokuwa na
maana yoyote kwa sanaa na wasanii kwa ujumla.
Aidha ni wakati kwa wasanii wote Tanzania kuona hakuna haja
ya malumbano zaidi ya kushirikiana wao pamoja na wadau wa sanaa kwa ujumla,
wakiwapo Clouds FM, ndio maana kutokana na umuhimu wao kila mmoja anaona bila
wao hawaendi, ukizingatia kuwa hata Sugu, aliliona hilo na kufikia kukaa chini
na kumaliza tatizo kwa maslahi ya muziki.
Bila hivyo, tusubiri malalamiko makubwa zaidi, vilio
visivyokuwa na mashiko, maana siku zote nyumba yenye kelele malaika mzuri
haishi humo, jambo linaloweza kuwatafuna wasanii wenye mtazamo huo, waliokuzwa
na kulelewa vyema na kufikia umaarufu na kuona dawa ni kuanzisha matusi kwa
faida wanazojua wenyewe.
0712 053949
0753 80608
No comments:
Post a Comment