
Dodoma/Dar. Mkutano wa ndani baina ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete na wabunge wa chama hicho uliofanyika Jumapili iliyopita mjini Dodoma, ni kama umeamsha upya makundi ya kuwania urais wa 2015, Mwananchi limebaini.
Kutokana na hali hiyo, jana chama hicho
kililazimika kutumia nguvu kubwa kudhibiti taarifa zinazohusu kauli
iliyodaiwa kuwa ilitolewa na Rais Kikwete, kwamba “Wanaoutaka urais
kupitia CCM waanze kujipitisha ilimradi wasiwagawe wanachama kwa misingi
ya makundi.”
Taarifa kuhusu ruksa hiyo inayodaiwa kutolewa na
Rais, ndizo zilizotikisa vichwa vya habari katika magazeti ya juzi na
jana lakini Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye anasema siyo
za kweli na kwamba Rais alilishwa maneno.
Nape jana katika mkutano na Waandishi wa Habari
jijini Dar es Salaam alisema: “Wamemlisha maneno mwenyekiti
wetu...inaelekea kuna kikundi cha watu wana mgombea wao wa kuchonga
ambaye bila shaka anapungukiwa na sifa, hivyo wanajaribu kumwongezea
sifa kwa kumlisha mwenyekiti maneno na kuwapa baadhi ya waandishi, uhuni
huo haukubaliki.”
Wakati Nape akitoa kauli hiyo, Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira akizungumza bungeni
jana pia alisema taarifa kuhusu mkutano wa Rais Kikwete na wabunge
zilipotoshwa, huku akitaka suala hilo lifafanuliwe na watendaji wa CCM.
JK na wabunge
Nape alisisitiza katika mkutano huo Rais Kikwete
alisema ni marufuku kwa mwanachama anayetaka kugombea kwenye uchaguzi wa
dola kujipitishapitisha na kufanya kampeni kabla ya wakati.
Habari kutoka ndani ya mkutano huo zinasema
chimbuko la hoja ya watu wanaotaka kujinadi kwa ajili ya uongozi
iliibuliwa na Mbunge wa Same Mashariki, Anna Killango Malecela na Mbunge
wa Lupa, Victor Mwambalaswa ambao walihoji juu vikao vinavyofanywa na
watu wanaosaka urais kupitia CCM kwa kuwashirikisha watendaji wa chama
na Serikali.
Majibu ya Kikwete
Baadhi ya wabunge wameliambia gazeti hili kuwa
Rais Kikwete katika mkutano huo alieleza kusikitishwa na kampeni za
urais ambazo alisema zinakigawa chama.
“Sisi tunashangazwa na taarifa ambazo magazeti
mmeziandika, ukweli ni kwamba mheshimiwa Rais alituasa kwamba tusikigawe
chama na kwamba asingependa tuwe na mgombea mwenye makovu ifikapo
2015,” alisema mmoja wa wabunge.
Vyanzo vyetu hivyo vilimnukuu Rais Kikwete
akisema: “Mnaumizanaa wee, sasa inaweza kufika hiyo 2015 tutajikuta
tukiwa na wagombea wenye plasta, sasa ikifikia hapo sijui tutaanza
kumuuza mgombea wetu au kutibu majereha kwanza?”
Sitta aja juu
Sitta aja juu
Wakati hayo yakielezwa, Mbunge wa Urambo
Mashariki, Samuel Sitta ameibuka na kusema kuwa kitendo cha kuruhusu
wagombea wa urais kujitangaza sasa ni hatua ambayo inaweza kuwagawa
Watanzania.
“Mimi sikuelewa hivyo, ni tafsiri fulani hivi tu
za watu wachache wenye masilahi yao, na wanaoishabikia hiyo ni wenye
mapesa mengi wanaoweza kufanya kampeni kwa muda mrefu,” alisema Sitta.
“Nimempigia Katibu Mkuu wetu atupe mwongozo katika
hili, ikiwezekana kwa maandishi ili ijulikane wazi nini kinapaswa
kufanyika na nini hakipaswi.”
MWANANCHI
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment