Dodoma. Wabunge wa CCM wamekuja juu na kumtaka
Rais Jakaya Kikwete kuwafukuza kazi vigogo wa Serikali mkoani Mtwara,
wakiwamo Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya kutokana na kile walichoeleza ni
uzembe uliochangia vurugu zinazoendelea za wananchi kugomea gesi kutoka
nje ya mkoa huo.
Wengine waliopendekezwa kuchukuliwa hatua ni
kamati nzima ya ulinzi na usalama ya ngazi ya mkoa na wilaya ya Mtwara
mjini, wakiwamo makamanda wa polisi.
Kutokana na hali hiyo, vigogo kadhaa mkoani humo
wako hatarini kukumbwa na ghadhabu hiyo akiwamo Mkuu wa vikosi vya Jeshi
la Wananchi Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Mkuu wa
mgambo na Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Wabunge hao walikuwa wakitoa mapendekezo hayo
kwenye kikao cha Kamati ya Wabunge wa CCM iliyofanya kikao cha dharura
juzi usiku, mjini hapa.
Kikao hicho kiliongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda, huku Spika wa Bunge, Anne Makinda ambaye wakati huo alikuwa
kwenye kikao cha Kamati ya Uongozi wa Bunge, aliwakilishwa na Mwenyekiti
wa Bunge, Jenista Mhagama.
Katika kikao hicho maalumu kilichokusudia kutoa
ushauri kwa Rais Kikwete juu ya njia mwafaka ya kutatua hali ya
machafuko, wabunge wengi wali kukasirishwa na jinsi hali ilivyo mkoani
Mtwara. Chanzo chetu kwenye kikao hicho kilieleza kuwa wabunge hao
walichukizwa na jinsi Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya walivyokuwa
wakipingana kimsimamo. Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Joseph
Simbakalila, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mjini, Wilman Ndile na Kamanda wa
Polisi Mkoa Linus Sinzumwa wamehusishwa.
Licha ya baadaye kuonekana kuwa kitu kimoja,
wabunge hao walidai kuwa walishindwa kutumia nafasi zao katika kutatua
tatizo hilo, ambalo hadi juzi Serikali ilisema walikuwa wamekufa watu
watano, wakiwamo wanajeshi wa JWTZ waliofariki katika ajali wakati
wakienda kutuliza machafuko.
Chanzo hicho kilieleza kuwa iwapo mapendekezo ya
wabunge hao yatapelekwa kwa Rais Kikwete kama michango ya wabunge hao
ilivyokuwa, huenda rungu likawaangukia pia viongozi wa kisiasa wa CCM
mkoani humo. Miongoni mwa wanasiasa hao, chanzo hicho kimesema ni wale
waliotoa kauli za waziwazi kuunga mkono msimamo wa kutoruhusu gesi
kusafirishwa nje ya mkoa huo.
“Hapa wapo wabunge, madiwani na viongozi wa ngazi mbalimbali wa CCM,” kilieleza chanzo hicho.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge walipendekeza
mkakati wa kutatua uzembe uliofanyika Mtwara, unapaswa kuchukuliwa kwa
uangalifu usije ukasababisha madhara mengine kwa Chama na Serikali.
Walisema suala hilo halina budi kuchukuliwa kwa
uangalifu hasa ikizingatiwa kuwa Chama cha CUF ndicho chenye nguvu
mkoani humo ukilinganisha na vyama vingine vya upinzani.
Wabunge hao walikituhumu chama hicho kuwa kimekuwa
kikijaribu kutumia vurugu hizo kama kigezo cha ushawishi wa kukubalika
mkoani humo.
MWANANCHI
Taarifa zilizopatikana jana mjini hapa zimeeleza kuwa tayari maazimio ya wabunge hao wa CCM yamewasilishwa kwa Rais Kikwete.
Taarifa ambazo hazijathibitishwa pia zinaeleza
kuwa leo Kamati ya Uongozi ya Bunge huenda ikatangaza Bungeni maazimio
yao kuhusu vurugu za Mtwara.
Kamati ya Uongozi ilianza kukutana kuanzia
Jumatano jioni na hadi jana wajumbe walikuwa wamejifungia wakijadili
namna wanavyoweza kushiriki na kuishauri Serikali kuhusu hatua mwafaka
za kuchukua.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment