Wapitanjia wakiwa karibu na kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania(KKKT)Usharika wa Kunduchi eneo la Mtongani jijini
Dar es salaam jana.
Bomu la machozi lilipuliwa jana mchana karibu na kanisa hilo wakati polisi wakiwafurumusha wahalifu waliojificha ndani ya jengo lililopo jirani na kanisa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema
jana wakati akitoa ufafanuzi kuhusu madai ya kulipuliwa kanisa la
Kunduchi.
Alisema polisi iliarifiwa na wasiri kuwa wahalifu walikuwa
wakitumia jengo hilo lililo mita 150 kutoka kanisani kupanga uhalifu na
wengine waliligeuza kijiwe cha mihadarati na kamali.
Hali hiyo ilisababisha majirani kukimbia kwa hofu wakidhani bomu
limelipua kanisa wakihusisha tukio hilo na lile la Jumapili iliyopita
ambapo bomu liliporushwa kwenye Kanisa Katoliki la Mtakatifu Yoseph
Mfanyakazi la Olasiti, jijini Arusha na kuua waumini watatu na kujeruhi
67.
Taharuki na hofu zilizagaa sehemu nyingi nchini kutokana na kuenea taarifa za mlipuko.
Kamanda Kenyela, akizungumza na wanahabari alisema uvumi huo wa
kanisa kulipuliwa, ulizagaa ndani na nje ya jiji na kueleza kuwa polisi
ilichukua hatua hiyo baada ya kupata taarifa za wahalifu waliojihami
ndani ya jengo hilo lisilokaliwa na watu.
Alisema polisi walipofika nje ya jengo hilo walithibitisha kuwa
lilikuwa na watu kama ilivyodaiwa na kwamba walikuwa wanavuta bangi,
kucheza kamari na kupanga uhalifu.
Aliwatetea askari wake kuwa wasingeingia moja kwa moja kwani hawakufahamu watu hao walikuwa na silaha za aina gani.
“Namna ya kuwapata haikuwa rahisi, waliamua kurusha bomu la
machozi kuwashtua , kishindo hicho kiliwatawanya watu hao ambao wengine
walikimbilia baharini na wengine kanisani, “ alisema na kuongeza:
“Kanisani kulikuwa na waumini, walitusaidia kuwakamata watu sita
walikimbilia humo,”aliowataja kuwa ni mwanafunzi wa kidato cha nne
katika Sekondari ya Boko na mtoto mwenye miaka 13 (majina yanahifadhiwa
kwa sababu ya umri).
Wengine ni mwanafunzi wa kompyuta wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
tawi la Mbezi Beach Japhet Nicodemas (20), kondakta wa daladala
Kasimu Seif (21) Nasir Kajembe (25) na Hussein Sadiki (18) wakazi wa
Kunduchi, hata hivyo wengine zaidi ya 40 walitoroka.
Wahalifu hao kwa mujibu wa Kenyela walikutwa na bangi, silaha
kadhaa zikiwamo nondo. Kenyela alipoulizwa sababu za kutumia bomu badala
ya mbinu nyingine, alisema ni maamuzi ya polisi kulingana na tukio.
Alisema polisi wapo kwenye misako ambayo itawalazimu ikibidi kutumia silaha kusaka wahalifu.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment