Spika wa Bunge, Anne Makinda
*Ofisi ya Spika yatuhumiwa kufuja fedha za Bunge
*Yadaiwa kutoa hongo za safari kwa makamishina
*Dk. Kashililah aikingia kifua, asema haina doa
*Dk. Kashililah aikingia kifua, asema haina doa
TUHUMA
za matumizi mabaya ya fedha za Bunge na upendeleo kwa baadhi ya wabunge
zimeanza kuiandama Ofisi ya Spika wa Bunge. Spika wa Bunge, Anne
Makinda, ametajwa kwa jina kuhusika katika tuhuma hizo, akidaiwa kutumia
mamlaka yake kushinikiza safari za nje kwa makamashina wa Bunge na
kugawa vyeo kwa maslahi yake binafsi, lengo likiwa kulinda wadhifa wake.
Taarifa zilizolifikia MTANZANIA Jumatano kutoka katika viunga vya Bunge mjini Dodoma, zimeeleza kuwa Spika Makinda, amekuwa akitumia mamlaka yake ya uspika kuwapangia safari za nje ya nchi makamishina wa Bunge ili kuwaweka karibu yake.
Taarifa zilizolifikia MTANZANIA Jumatano kutoka katika viunga vya Bunge mjini Dodoma, zimeeleza kuwa Spika Makinda, amekuwa akitumia mamlaka yake ya uspika kuwapangia safari za nje ya nchi makamishina wa Bunge ili kuwaweka karibu yake.
Taarifa hizo zimedai kuwa lengo la Spika Makinda kuwaweka karibu makamishna wa Bunge ni kujenga jeshi lenye nguvu la kumlinda dhidi ya baadhi ya wabunge ambao wamekuwa hawaridhishwi na mwenendo wake kiuongozi, hatua ambayo imewasukuma kuanza kupanga mikakati ya kumng’oa kwa kumfitinisha na baadhi ya viongozi wakuu wa dola.
Duru za habari kutoka mjini Dodoma zimedai kuwa, Spika Makinda, alishawishi mamlaka zilizo chini ya ofisi yake kuwapangia makamishana wa Bunge safari ya kwenda nchini India kwa ajili ya kukagua hospitali ambazo wamekuwa wakitibiwa viongozi wa kitaifa.
Kwamba, huku akitambua kuwa safari hiyo haina umuhimu kwa makamishina hao, aliridhia wakae nchini humo kwa muda wa siku 10 huku wakilipiwa kila kitu na Ofisi ya Bunge.
Taarifa hizo zinakwenda mbali zaidi kwa kueleza kuwa baadhi ya watumishi wa Bunge walio chini ya Ofisi ya Spika wamekuwa wakishirikiana na mawakala wa usafiri wa anga wanaotoa tiketi za safari kwa wabunge kuongeza bei ya tiketi hizo tofauti na ile ya kawaida.
Mbali na kuelekezewa tuhuma hizo, Spika Makinda, pia anadaiwa kukiuka kanuni za Bunge kwa kujipa mamlaka ya kumteua mmoja wa wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge anayedaiwa kuwa mshirika wake wa karibu kisiasa na mtu ambaye amekuwa akimpa msaada mkubwa wa ushauri wa kuliongoza Bunge.
Inadaiwa kuwa uamuzi huo wa Spika Makinda ni wa kulipa fadhila kwa mshirika huyo na pia kuzidi kumuweka karibu katika mwendelezo wa kumsaidia kiuongozi.
Hata hivyo, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah, wakati akizungumza na MTANZANIA Jumatano jana kupitia simu yake ya kiganjani kuhusu mlolongo huo wa tuhuma dhidi ya Ofisi ya Spika, alisema zinatolewa na wabunge ambao hawana uelewa wa jambo wanalozungumza.
Dk. Kashililah alisema ni kweli makamishina wa Bunge walifanya safari katika siku za karibuni ya kwenda India kukagua hospitali wanazotibiwa viongozi kwa sababu hiyo ni moja ya majukumu yao ya kawaida.
Alisema makamishina wa Bunge walikwenda India kwa ajili ya ukaguzi wa hospitali hizo ikiwa ni maandalizi ya utaratibu mpya wa kutibiwa kwa bima ya afya kimataifa.
“Kuna utaratibu mpya wa bima ya afya wa ndani na nje ya nchi, wao walikwenda kukagua ubora wa huduma wa hospitali hizo, ni kazi yao kabisa kabisa,” alisema Dk. Kashililah.
Alipoulizwa kuhusu tuhuma za upangaji bei ya safari baina ya mawakala wa usafiri wa anga na baadhi ya maofisa wa Bunge walio chini ya Ofisi ya Spika, Dk. Kashilillah alisema madai hayo hayana ukweli na kuwataka wanaohoji utaratibu wa safari za wabunge kutambua kuwa kwa sasa kuna utaratibu wa kununua tiketi kwa njia ya mtandao ambazo zimekuwa hazionyeshi bei.
“Hayo malipo ambayo hayawekwi wazi sijui ni yapi, ninavyofahamu ni kwamba, sisi tunavyoingia mkataba na hawa mawakala, kuna malipo mbalimbali mengine hayawekwi wazi.
“Malipo haya ni yale ya usafiri, malazi na huduma nyingine muhimu katika nchi anayosafiri mhusika, na haya huwa hatulipi kwa fedha taslimu, huwa tunalipa baadaye. Huwa tunafanya malipo haya baada ya siku 90 hadi miezi sita, inategemea maana wanaosafiri ni wengi kuliko uwezo wetu wa kulipa,” alisema Dk. Kashilillah.
Dk. Kashililah pia alizungumzia hatua ya Spika Makinda kumteua mmoja wa wenyeviti wa kamati za Bunge kwa kueleza kuwa Spika ana uwezo huo.
“Spika amemteua Mwenyekiti wa kamati kwa mamlaka aliyo nayo, anao uwezo wa kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria na hata wakati amemteua alisema wazi amemteua kwa mamlaka aliyo nayo.
“Alikwenda Kamati ya Kanuni, akawaambia kuwa kuna kamati kubwa ambayo nimeiomba, kamati ya kanuni ikasema sawa na akakubaliwa. Kamati ya kanuni ilimpa uwezo akateua Mwenyekiti kisha akaomba Kaimu ateuliwe na wajumbe wa kamati hiyo.
“Anayo mamlaka makubwa ya kutosha kufanya hivyo, Spika anao uwezo wa kuteua ama kuifuta kamati yoyote kisheria, kama utakumbuka aliwahi kuifuta Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC),” alisema Dk. Kashililah.
Alitoa wito kwa wabunge na wananchi wote kuacha kuzusha maneno yenye mwelekeo wa kuzua kashfa kwa viongozi kwa kueleza kuwa ofisi yake iko wazi wakati wote, hivyo kama kuna mwananchi au mbunge mwenye dukuduku juu ya jambo lolote linalohusu Ofisi ya Bunge yuko huru kufikisha malalamiko yake au kuwayasilisha kwa barua na atajibiwa.
MTANZANIA



No comments:
Post a Comment