Meneja
Uendeshaji wa Kampuni ya Udalali ya Flamingo, Nyalila Noel akipandika
hati ya mahakama katika basi la Shirikisho la soka Tanzania (TFF),
ambayo inaruhusu kukamatwa kwa mali za shirikisho hilo.(Picha na Habari Mseto)
Meneja
Uendeshaji wa Kampuni ya Udalali ya Flamingo, Nyalila Noel akibandika
hati ya mahakama katika basi la Shirikisho la soka Tanzania (TFF),
ambayo inaruhusu kukamatwa kwa mali za shirikisho hilo.
Dereva
la basi dogo la TFF (kulia), akisoma hati ya mahakama iliyotolewa kwa
ajili ya kukamatwa kwa mali za TFF kutokana na deni la sh. milioni 51
linazodaiwa na Safina Holding.
Hati ya mahakama.
'Sasa tunafunga na kuondoka nalo'.
Wafanyakazi
wa Jay Ambe Break Dowan wakichakalika na ufungaji wa basi la TFF tayari
kwa ajili ya kuondoka nalo kutokana na deni wanalodaiwa na Safina
Holding.
Gari dogo aina ya Toyota Crown lenye namba T 643 BJW likiwa
limezuia gari la Jay Ambe Break Down lisitoke katika lango kuu la
kutoka na kuingia katika Ofisi za TFF, baada ya mali za shirikisho hilo
kukamatwa na dalali wa mahakama.
Hati
ya kukamata mali za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ikiwa
imebandikwa katika basi kubwa aina ya Youtong kwa ajili ya utekelezaji
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah akizungumza na waandishi wa habari wakati wa sakata hilo.
Na Mwandishi Wetu
UONGOZI
wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), leo umejikuta kwenye wakati mgumu
baada ya madalali wa Kampuni ya Flamingo Auction Mart, kutinga katika
ofisi za shirikisho hilo na kukamata baadhi ya mali zake ili zipigwe
mnada kufidia deni wanalodaiwa.
Shirikisho
hilo linadaiwa na Safina Holding ya jijini Dar es Salaam zaidi ya sh
milioni 50, baada ya kuwaweka katika hoteli ya kampuni hiyo maeneo ya
Kijitonyama, waamuzi wa michuano ya Kombe la Kagame mwaka 2012.
Sakata
hilo liliweza kudumu kwa muda wa saa nne kuanzia saa tano asubuhi na
kudumu hadi saa tisa mchana, baada ya TFF kukubali kulipa sh milioni 20
kati ya sh 51,507,012 zilizokuwa zikidaiwa.
Awali,
madalali hao wa Flamingo, walifika Ofisi za TFF, Karume Ilala na
kujadiliana na Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Angetile Osiah na
kushindwa kufikia muafaka, hali iliyowalazimu kuita gari maalumu ‘break
down’ mali ya Jay Ambe na kulifunga basi dogo aina ya Toyota Coaster.
Baada
ya gari hilo kufungwa ili likokotwe kupelekwa ‘yadi’ ya Flamingo,
mlinzi wa TFF aliamua kukimbilia geti la kutokea na kulifunga na
kuwafanya madalali hao washindwe kutoka nalo.
Jambo
hilo lilizidisha sintofahamu na kuwafanya baadhi ya watu kuingia ndani
kushuhudia kinachoendelea, huku maofisa wa Flamingo wakihangaika
kuwasiliana na Jeshi la Polisi kwa ajili ya kupatiwa msaada wa kuweza
kutekeleza amri ya mahakama.
Usumbufu
huo wa kuzuia madalali wasitekeleze amri halali ya mahakama,
ulisababisha kero kwa watu mbalimbali waliofika Karume, kwa kushindwa
kuingia ama kutoka katika ofisi hizo.
Wakati
majadiliano yakiendelea, zilipatikana taarifa kuwa TFF wameomba walipe
sehemu ya fedha wanazodaiwa kwa ahadi ya kumalizia zilizobaki, ili
magari yake yasichukuliwe, hali iliyomfanya dereva wa gari lililozuia
mlango kwenda kuliondoa na kuruhusu shughuli zingine kuendelea.
Ilipofika saa tisa mchana, Osiah alijitokeza na kuwaeleza waandishi wa habari kuwa wamemuagiza mhasibu akachukue fedha benki.
Akizungumzia
adha hiyo, Osiah alisema wao hawakujua kama tukio hilo litatokea, kwa
kuwa barua waliyokuwa nayo haikueleza hivyo, na kudai kushangazwa na
hatua hiyo, wakati barua kutoka Flamingo ikionekana kuchanganya tarehe
ya zoezi hilo kufanyika.
Osiah
alisema walipata nguvu za kugoma magari hayo yasichukuliwe kutokana na
kugundua kuna makosa ya tarehe katika barua hiyo, huku akikiri kudaiwa
sh milioni 28.
“Sisi
tunadaiwa mil 28/-, ila mambo ya kimahakama ndio maana ikafikia hiyo na
pia tumewashangaa sana Safina, badala ya mambo tuyamalize wenyewe, wao
wanayakuza na fedha hizo zilitokana na hifadhi ya waamuzi katika
michuano ya Chalenji,” alisema Osiah.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi wa Flamingo, Deogratius Luziga, alisema wao
walifikia hatua hiyo ya kutaka kuondoka na magari hayo kama amri ya
mahakama ilivyowaagiza na kudai kuwa tatizo kubwa ilikuwa ni dharau za
Osiah na kuwa angefanya hivyo toka awali wasingechukua muda wote huo
katika zoezi hilo.
“Tumekubaliana
mara baada ya kutuomba sana, tumekubali watangulize milioni 20/-
kwanza, halafu milioni 31/- watamaliza ndani ya siku 14, kwani hii
mahakama inaruhusu na bila hivyo, tutafanya kama tulivyokusudia kwa kuwa
bado ni mali yetu sisi,” alisema Luziga.
Awali, Osiah alionekana kuchanganyikiwa na kuwasihi madalali hao kuachana na zoezi hilo la kuchukua magari hayo.
“Naombeni
muache kufanya hivyo ambavyo mnataka kufanya, mimi sasa hivi namwambia
mhasibu wetu mwende naye benki akawape fedha zenu zote jamani, msifanye
hivi,” alisihi Osiah.
No comments:
Post a Comment