Moshi/Dar. Habari za uhakika kutoka ndani ya
Jeshi hilo zimedokeza kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta
Jenerali Said Mwema anatarajiwa kustaafu mwezi ujao na haijafahamika
kama ataongezewa mkataba ama la.
Vyanzo mbalimbali vimedai kuwa japokuwa IGP Mwema
anasita kukubali kuongezewa muda, lakini Rais Jakaya Kikwete anaonelea
aongezewe muda ili wamalize pamoja uongozi wao mwaka 2015.
IGP Mwema ambaye alikuwa Ofisi ya Polisi wa
Kimataifa (Interpol) Jijini Nairobi, Kenya, aliteuliwa kushika wadhifa
wake huo mwaka 2006 na Rais Kikwete, kumrithi Omar Mahita ambaye
alistaafu.
Habari zinasema endapo IGP Mwema hatapewa mkataba
wa ama miaka miwili, basi ni dhahiri Rais Kikwete atakuwa na kibarua
kigumu cha kuanza mchakato wa kumtafuta mrithi wake.
IGP Mwema anachukuliwa kama mmoja wa viongozi wa
juu wa Jeshi hilo aliyelifanyia mapinduzi makubwa aliposhika madaraka
hayo, ikiwamo kuja na dhana ya ulinzi shirikishi ama Polisi Jamii.
Tayari mabadiliko hayo yameaanza kufanyika kwa
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni jijini Dar es Salaam, Charles
Kenyela kuhamishiwa makao makuu ya jeshi hilo.
Taarifa zaidi zimepasha kuwa nafasi nyingine ya
juu ambayo kuna dalili ya kuwepo kwa mabadiliko ni ya Mkurugenzi wa
Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), inayoshikiliwa na Robert Manumba.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya jeshi hilo
aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa (jina linahifadhiwa), amehamishiwa
makao makuu wakati tayari kuna taarifa za yeye kustaafu.
Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini,
Advera Senso alipotakia kueleza juu ya taarifa hizo za mabadiliko ndani
ya jeshi hilo, kutokana na muda wa kustaafu kwa maofisa hao kufika
alisema hizo ni taarifa za hisia.
“Hizo ni taarifa za hisia zako tu, lakini huwezi
kuniuliza swali la mwezi wa saba leo, tusubiri muda ukifika tuone
itakuaje,” alisema Senso.
Pia kuhusu taarifa za Kamanda wa Polisi Kinondoni,
Charles Kenyela kuhamishia makao makuu alisema; “Subirini nitatoa
taarifa kwani mbona kila mabadiliko yanayotokea ya makamanda huwa
ninatoa taarifa hivyo subirini”.
Habari zisizo rasmi zimelidokeza gazeti hili kuwa
huenda DCI Manumba akapumzishwa kutokana na hali yake ya kiafya
kuonekana kutorejea vizuri, licha ya kupatiwa matibabu nchini Afrika
Kusini.
Kulingana na taarifa hizo, Kamishna Isaya Mngulu ndiye
anayetajwa sana kuweza kumrithi Manumba na hata kupandishwa cheo kutoka
Naibu Kamishna hadi Kamishina ni maandalizi hayo.
Inaelezwa kuwa Kamishna Mngulu alikuwa astaafu
rasmi Oktoba mwaka huu, lakini kitendo cha kupandishwa cheo kunaongezea
nguvu tetesi kuwa ndiye anayeandaliwa kushika wadhifa wa DCI.
Habari nyingine zinadai kuwa wapo makamanda wa
polisi wa mikoa ambao nao wanapaswa kustaafu kwa mujibu wa sheria, baada
ya kutimiza umri wa miaka 60, lakini kuna dalili ya kupewa mikataba.
Taarifa zilizopatikana zinaeleza kuwa mabadiliko
hayo yanakuja huku Jeshi la Polisi likikabiliwa na changamoto nyingi
ikiwamo baadhi ya askari wake zaidi ya 70 kuuawa katika matukio
mbalimbali, yakiwamo ya kushiriki katika uhalifu na wengine kukamatwa
wakishiriki kufanya uhalifu.
Baadhi ya matukio hayo ni pamoja na lile la askari
polisi aliyeuawa kwa kupigwa risasi mkoani Kagera, askari polisi
waliochukua fuko la Sh 150 milioni walilookoa kutoka kwa majambazi
jijini Dar es Salaam.
Matukio mengine ni gari la polisi kukamatwa likiwa
limebeba bangi, pamoja na askari watatu kukamatwa wakiwa na kichwa cha
mtu Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro.
Wakati jeshi hilo lilikabiliwa na matukio hayo,
hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete aliwapandisha vyeo maofisa 21 wa Jeshi
la Polisi kuwa Makamishna wa Polisi (CP) na Naibu Makamishna wa Polisi
(DCP), huku wengine wakiwa tayari wamefikisha umri wa kustaafu.
Miongoni mwa waliopandishwa vyeo vya CP ni Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamhanda ambaye awali alikuwa
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi na Suleiman Kova na Isaya Mngulu,
ambao walikuwa Manaibu Kamishna wa Polisi.
Waliopandishwa vyeo kuwa Manaibu Kamishna wa
Polisi ni Elice Mapunda, Brown Lekey, Hamdani Omar Makame, Keneth
Kasseke, Abdulrahman Kaniki, Thobias Andengenye, Adrian Magayane,
Sospeter Kondela, Simon Sirro na Ernest Mangu.
Wengine ni Kamanda wa Kikosi cha Usalama
Barabarani, Mohamed Mpinga, Hussein Laisser, Anthony Joel, S. Mwami,
Adolfina Chialo, Mpinga Michael Gyumi, Ally Mlenge, Herzon Gyimbi na
Jonas Mugendi.
Kabla ya vyeo vipya walikuwa Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi.
Habari hii imeandikwa na Daniel Mjema na Ibrahim Yamola.
MWANANCHI
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment