Dar es Salaam. Tume ya Mabadiliko ya Katiba jana
ilizindua rasimu ya Katiba Mpya inayopendekeza kuwapo kwa mabadiliko
makubwa kwenye mfumo wa utawala, yakiwamo ya kuwa na Serikali Tatu;
Shirikisho la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Tanzania Bara
na Serikali ya Zanzibar.
Mabadiliko mengine yaliyosheheni kwenye rasimu
hiyo ni kufutwa kwa viti maalumu vya ubunge, suala la maadili ya
viongozi wa taifa, umri wa urais kubaki kama ulivyokuwa na kuruhusiwa
kwa wagombea binafsi katika ngazi zote; urais, ubunge, udiwani mpaka
ngazi za mitaa.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mwenyekiti wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alisema Tume pia
imependekeza kuingizwa kwenye Katiba Mpya mambo kadhaa kama Tunu, Dira
na Misingi ya Taifa.
“Tulitaka kuifanya rasimu hii iwe fupi kadri
iwezekanavyo, lakini kutokana na wingi wa maoni tumeifanya iwe na Ibara
240. Katiba ya sasa ina Ibara 152,” alisema Jaji Warioba na kuongeza:
“Tumeendelea kuitambua misingi mikuu minne ya
taifa ambayo ni Uhuru, Haki, Udugu na Amani. Lakini pia tukaongeza
misingi mingine mitatu ambayo ni Usawa, Umoja na Mshikamano.
Tumependekeza Katiba yetu mpya iwe na misingi saba.”
Jaji Warioba alisema Tume pia imetambua mambo
kadhaa kuwa ni Tunu za Taifa: “Tunu ya kwanza ni Utu. Tunaamini kuwa
watu wote ni sawa, tusiwe na ubaguzi wala tofauti zozote. Tunu nyingine
ni Uzalendo, Uadilifu, Umoja, Uwazi Uwajibikaji na Lugha ya Kiswahili.”
Jaji Warioba alisema pia kuwa Tume imebainisha
malengo ya Taifa ambayo yatakuwa mwongozo wa Mihimili ya Dola; Serikali,
Bunge na Mahakama.
“Malengo hayo yatakuwa ya aina mbalimbali. Kuna
malengo ya kisiasa, kiuchumi, kimazingira na mengine mengi
yatakayofafanuliwa baadaye,” alisema.
Jaji Warioba alisema Tume pia imependekeza Katiba ijayo ionyeshe wazi maadili ya kijamii, kiutawala na kiuongozi.
“Tumependekeza kuwapo maadili ya viongozi, miiko
na kiundwe chombo cha kusimamia maadili. Tunapendekeza sekretarieti ya
maadili ya viongozi iliyopo, iwe tume kamili,” alisema.
Muundo wa Serikali Tatu
Jaji Warioba alisema baada ya kupitia maoni mengi,
Tume imeridhika kwamba inafaa Tanzania iwe na mfumo wa Serikali tatu,
yaani Serikali ya Shirikisho, Serikali ya Tanzania Bara na Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar.
MWANANCHI
“Tumependekeza Serikali ya Muungano iwe na mawaziri wasiozidi 15
na wabunge 75. Wabunge 50 kutoka Bara, 20 Zanzibar na wabunge watano wa
kuteuliwa na Rais,” alisema wabunge wa kuteuliwa watatoka katika kundi
la watu wenye ulemavu tu.
Alisema Serikali hiyo ya Muungano itakuwa
inaongozwa na Rais Mtendaji. Alitaja mambo yatakayoingia kwenye Muungano
kuwa ni Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ulinzi na
usalama, uraia na uhamiaji, sarafu na Benki Kuu, mambo ya nje, usajili
wa vyama vya siasa na ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya kodi
yatokanayo na mambo ya Muungano.
Mikutano 1,942
Jaji Warioba alisema rasimu hiyo ya Katiba
imekamilika baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kufanya mikutano 1,942
ambayo ilihudhuriwa na watu 1,306,500.
“Watu 395,000 walitoa maoni ya ana kwa ana na
makundi 160 maalumu yalitoa maoni yao. Pia tulizungumza na viongozi wa
kitaifa; walioko madarakani na wastaafu. Viongozi 43 walitoa maoni,”
alisema.
Jaji Warioba alisema baada ya maoni hayo, walikuwa
na miezi mitatu kuyachambua na kuandaa rasimu ya Katiba, lakini
wakalazimika kuongeza muda huo hadi Mei mwaka huu.
“Kutokana Sheria, Rasimu hii itachapishwa kwenye
Gazeti la Serikali na baadaye kwenye magazeti kabla ya Mabaraza ya
Katiba kuanza kazi,” alisema Jaji Warioba .
Alisema mchakato huo wa Mabadiliko ya Katiba
ulioanza kwa Sheria iliyotungwa Novemba 2011 na baadaye kufanyiwa
mabadiliko Februari 2012, umepangwa kumalizika ndani ya miezi 18...
“Hivyo Tume imekusudia kumaliza mchakato huo Novemba Mosi mwaka huu,”
alisema.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment