Na Mahmlud Zubeiry, Marakech
USIKU TIMU
ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars usiku jana imekiona cha moto
mbele ya askari wa Uwanja wa Marakech, baada ya kufanyiwa vurugu na
kuzimiwa taa ishindwe kufanya mazoezi kwenye Uwanja huo siku moja kabla
ya mchezo wao na wenyeji wao Morocco leo, kuwania tiketi ya kucheza
Fainali za Kombe la Dunia. Sheria
za FIFA zinasema timu mgeni, itapewa fursa ya kufanya mazoezi katika
Uwanja utakaotumika kwa mechi dhidi ya wenyeji katika muda ambao mechi
itachezwa, lakini jana usiku msafara wa Stars ulipofika Uwanja wa Marakech
ulizuiwa kuingia ndani na askari wa uwanjani hapo. Juhudi
za Kocha mkuu wa Stars, Kim Poulsen kuwaelewesha askari wa Uwanja huo
sheria ili wairuhusu timu kuingia uwanjani hazikuzaa matunda na ikabidi
viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) waingilie kati, nao pia
wakachemsha.
|
Dk Dau getini |
|
Mtanzania anaruka geti ili kufungua mlango Stars ikafanye mazoezi |
|
Baadhi ya wachezaji wa Stars, kutoka kulia Juma Kaseja, Amri Kiemba, Mrisho Ngassa na Salum Abubakar baada ya kuingia uwanjani |
|
Crescentius Magori kushoto akishuhudia marefa wa mchezo huo wakikagua pasipoti za wachezaji wa Stars |
|
Wasiwasi; Kutoka kulia DK Dau, Mh Zitto Kabwe, Mh Mohamed Dewji na Magori wakijadiliana uwanjani |
Ikawadia
zamu ya viongozi wa Kamati ya Ushindi ya Stars, inayodhaminiwa na
Kilimanjaro Premum Lager, ambao nao walichemsha- ndipo baadhi wa
Watanzania waishio hapa na wachache waliosafiri kutoka Dar es Salaam
walipoongeza nguvu.Walikwenda kufungua geti kwa nguvu, wakawaweka kando askari waliokuwa wanawazuia na kuiingiza timu uwanjani kufanya mazoezi. Hata hivyo, Stars ilipofika uwanjani ililazimika kusubiri tena, kwani wenyeji Simba wa Atlasi walikuwa wakiendelea na mazoezi.Baada
ya nusu saa, Morocco walimaliza awamu yao na Stars wakaanza kupasha
misuli moto. Hata hivyo, baada ya dakika 34, taa za Uwanja huo zilizimwa
na uwanjani kuwa giza totoro, lakini viongozi wa TFF wakaenda kuomba,
zikawashwa na timu ikafanya mazoezi kwa dakika 10 zaidi. Naibu
Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, Mh. Amos Makalla aliyekuwapo
wakati wa vurumai zote hizo, alisikitishwa mno na kitendo hicho akisema
si cha kiungwana na si cha kiunamichezo.
|
Makipa mazoezini; Juma Kaseja amedaka, Ally Mustafa 'Barthez' anamshuhudia kushoto |
|
Mtanzania amemdhibiti askari wachezaji waingie uwanjani |
|
Wachezaji wakiingia uwanjani kufanya mazoezi |
|
Watanzania wamefanikiwa kufungua geti |
|
Mpambano, Kim Poulsen na askari, nyuma ni Mgoyi |
Makamu
wa Rais wa TFF, Athumani Nyamlani alisema Morocco walikuja kucheza Dar
es Salaam walipokewa vizuri na wakahudumiwa vizuri hadi wanaondoka,
ajabu leo wanaifanyia ‘unyama’ Tanzania.Mkuu
wa Msafara wa Stars hapa, Crescentius John Magori alisema watapeleka
malalamiko FIFA, waandaji wa michuano ya kufuzu kwa Kombe la Dunia na
kwa kuwa ushahidi upo, anaamini Morocco watachukuliwa hatua.Mwenyekiti
wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe alishauri Stars
icheze chini ya angalizo kwa kuwasilisha barua FIFA mapema ili wakae
wanajua kuhusu hali halisi Morocco.Kwa
ujumla kilichotokea leo kimewatia woga Watanzania wengi waliopo hapa
kuelekea mchezo wa kesho, ambao Stars inahitaji ushindi ili kujiimarisha
katika mbio za kuelekea Brazil 2014. Hata
ulinzi wa msafara wa Stars kutoka hotelini hadi uwanjani hakuwa wa
kutosha na ilishuhuidiwa mara kadhaa ukiingiliwa na magari mengine
barabarani wakati timu ikienda uwanjani kwa mazoezi.Wenyeji nchini Morocco wanasema inapowadia mechi, huwa wanaogopa kwa sababu mara nyingi hutokea vurugu ya damu kumwagika.Kwa ujumla Stars inaingia katika mchezo wa kesho katika hali ya wasiwasi na woga mkubwa. Stars itashuka dimbani saa 3:00 usiku kesho kwa saa za hapa sawa na saa 5:00 za Tanzania kucheza na Morocco.Stars
inashika nafasi ya pili katika Kundi C, ikiwa na pointi sita nyuma ya
Ivory Coast yenye pointi saba, ambayo kesho itakuwa ugenini ikimenyana
na Gambia katika mchezo mwingine wa kundi hilo.
|
Wachezaji Stars Uwanja wa Marekch |
Stars
ilitua hapa Jumatatu ikitokea Ethiopia ambako iliweka kambi ya wiki
moja na kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Sudan, ulioisha kwa sare ya
bila mabao.Kabla
ya kuja hapa, Stars iliweka kambi ya wiki moja katika hoteli ya
Tansoma, Dar es Salaam ikijifua Uwanja wa Karume na siku chache kabla ya
kuondoka ilialikwa Ikulu na Rais Jakaya Kikwete, aliyewapa hamasa kwa
hotuba nzuri.
MUNGU IBARIKI TAIFA STARS MUNGU IBARIKI TANZANIA
HABARI NI KWA HISANI YA MAHMLUD ZUBEIRY , MARAKECH
No comments:
Post a Comment