ITUMIENI SIKUKUU KULIPAKA RANGI PENZI LENU, FANYENI HAYA


HUU ni msimu wa sikukuu, ni kipindi ambacho wapenzi hukitumia kulipaka rangi penzi lao. Najua kwa watu wanaopendana kwa dhati kila siku ni sikukuu kwao lakini leo nataka nikukumbushie yale ambayo nimekuwa nikiyazungumzia kwamba yanafaa wapenzi kufanyiana katika sikukuu.
Unaweza ukashindwa kuyafanya yote lakini angalia hata moja la kumfanyia mwenza wako kutokana na uwezo wako na kamwe usikubali siku ipite hivihivi.
Ifanye iwe siku ya furaha
Hakuna kitu kibaya kama wapenzi katika siku hizi kununiana ama kuudhiana. Hizi ni siku za furaha hivyo basi, hakikisha unafanya kila uwezavyo kumfanya mwenza wako awe na uso wa tabasamu muda wote.
Hivi inakuwaje pale mnaposherehekea sikukuu ya Idd kisha mpenzi wako akababatiza ujumbe wa mapenzi katika simu yako kutoka kwa mtu mwingine? Ikitokea hivyo lazima siku itakuwa mbaya kwenu. 
Ndiyo maana nikasema jitahidi sana katika sikukuu hii kuyaondoa yale makovu yaliyokuwa katika penzi lenu ili mfungue ukurasa mwingine wa penzi lenu. Jiweke mbali na mambo yanayoweza kuwatibulia furaha.


Zawadi ni muhimu
Siku zote zawadi ni chachandu katika penzi. Kumbuka katika suala la uhusiano, zawadi ni zawadi bila kujali ukubwa wake. Hii itategemea tu na uwezo wako hivyo ni vizuri ukamwandalia zawadi nzuri sana mwenza wako.

Endelea kusoma habari hii kwa kubofya hapa chini




Kadi maalum
Usisahau kumwandalia mpenzi wako kadi ya kumtakia Idd njema. Kumbuka kadi utakayomnunulia ‘mtu’ wako inatakiwa kuwa tofauti na ile utakayompelekea rafiki yako wa kawaida au mzazi wako. Hili ni la muhimu sana kulizingatia. Angalia rangi za kadi, ujumbe na ukubwa wa kadi. 
Kama wewe ni mwanaume, kadi ya Idd utakayompelekea Salum iwe tofauti na ile utakayompelekea Saumu ambaye ni mpenzi, mchumba au mke wako. Hakikisha kadi utakayompelekea la-azizi wako inamvutia na kutamani kuisoma kila mara kutokana na jinsi ilivyo.



‘Surprise’
Rafiki yangu mmoja amenieleza kwamba katika sikukuu hii ya Idd atamshangaza mpenzi wake ‘surprise’ kwa kumnunulia gari na kumvisha pete ya uchumba. Sijui wewe umejiandaa kumfanyia ‘surprise’ gani yule umpendaye. 
Binafsi najua nitamshangaza vipi shemeji yenu na najua hicho nitakachomfanyia atashindwa kuamini masikio na macho yake. Na wewe pia jiandae kumfanyia ‘surprise’ yoyote mwenza wako.



Nendeni ‘OUT’
Yawezekana katika kipindi chote cha uhusiano wenu hamjawahi hata siku moja kutoka wote kwenda sehemu yoyote tulivu au yenye shamrashamra na mkafurahia. 
Kimsingi kutoka na mwenza wako kuna faida kubwa sana, hivyo basi si vibaya katika sikukuu hii mkatenga fedha ambazo zitawafanya siku hiyo mwende sehemu ambayo hamjawahi kwenda pamoja.
Kama wewe na mwenza wako mlikuwa na utaratibu wa kwenda ‘out’ kila wikiendi, safari hii mnaweza kupanga kwenda sehemu nyingine tofauti ikiwezekana hata kutoka nje ya mji mnaoishi. Kwa mfano kama mko Dar mnaweza mkaenda zenu Bagamoyo au Zanzibar, ni suala la kujipanga tu.

Kuna mengi ya kufanya mnapotoka ‘out’, mojawapo ni kubadilishana mawazo juu ya maisha yenu na kuombana msamaha pale mlipotokea kukwaruzana. Yaani ni kipindi cha kulikarabati penzi lenu na hata pale mtakapokuwa mnarudi inakuwa ni kama vile mmefungua ukurasa mpya wa penzi lenu.
Nimalizie kwa kusema tu kwamba, kila atakachokufanyia mwenza wako kiwe kidogo ama kikubwa ni vyema ukakithamini huku ukiweka akilini mwako kwamba uwezo wake umeishia hapo, kikubwa ni kwamba ameonesha jinsi anavyokupenda, mengine ni majaaliwa.

Nawatakia sikukuu njema yenye furaha na amani ila niwashauri umakini katika kila jambo.

No comments

Powered by Blogger.