HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

» »Unlabelled » MAUAJI YA KUTISHA MKOANI SIMIYU

 
 Polisi na wananchi wakiangalia mabaki ya nyumba iliyochomwa moto  

Wiki iliyopita katika ukurasa huu, tuliwaletea ripoti maalumu kuhusu mauaji ya kinyama yaliyotokea mkoani Simiyu kupitia Baraza la Kimila maarufu kama Dagashida.
Pamoja na mambo mengine, ripoti hiyo ilieleza hali ilivyo mbaya na kwamba katika mwaka mmoja uliopita, wastani wa watu watatu waliuawa na Dagashida kila wiki wakiwamo wanawake na watoto. Pia wanavijiji wa maeneo husika wanavyoshindwa kutoa ushirikiano kwa polisi wakihofia ukatili au kuuawa na kundi hilo.
Leo tunaendelea na ripoti hiyo ambayo pamoja na mambo mengine inaeleza namna Dagashida linavyotumika katika jamii, viongozi wanavyochapwa bakora, pia juhudi na msimamo wa Jeshi la Polisi na harakati za kusambaratisha baraza hilo.
Baraza Linatumika kwa visasi
Katibu wa Umoja wa Wazazi mkoani humo, Fadhil Murani anasimulia akisema kuwa mbaya zaidi baraza hilo limekuwa likitoa hukumu kwa kutumia hisia na tuhuma zisizokuwa na uhakika.
“Halafu mtuhumiwa wakishamweka katikati, haruhusiwi kujitetea wala kuzungumza chochote, matokeo yake wanamchoma moto au wanamuua kwa mapanga,” anasema Murani.
Anasimulia kuwa asilimia kubwa ya vijana wa baraza hilo kwa sasa wanatumiwa na watu wenye fedha katika ugomvi wa mipaka ya ardhi na mashamba.
“Kwa mfano, kama una adui yako ukapeleka pesa kidogo kwa wazee wa baraza hilo au ukawanunulia pombe, halafu ukamshtaki mtu, lazima utasikia yule mtu kavamiwa usiku na kuuawa kwa mapanga au watampigia mbiu na kamchoma moto,” anasema Murani.
Mmoja wa wanavijiji kutoka Kata ya Mahuni, Deo Ngulyati anasema kuwa malengo halisi ya kuwepo kwa baraza hilo yamepotea kwani limegeuka kuwa adui na hasara katika ustawi wa jamii.
“Zamani lilikuwa ni baraza linalosaidia ukuaji wa ustawi wa jamii na kuchochea maendeleo, walidhibiti migogoro, walihamasishana kwenye misiba na majanga, kujenga huduma za kijamii na walizuia uhalifu,” alisema Ngulyati.

ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI

Mwenyekiti anachapwa bakora
Taarifa nyingine kutoka ndani katika vijiji mbalimbali mkoani humo, zinaeleza kuwa baraza hilo limekuwa likitoa adhabu ya viboko kwa viongozi wa Serikali za Mitaa.

Baadhi ya viongozi wa kijiji (majina tunayo), wanadaiwa kukutana na adhabu hizo hivi karibuni kabla ya Mkoa mpya wa Simiyu kuanza kazi rasmi.
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Salum Msangi anasema kuwa taarifa za kuwepo kwa adhabu hiyo miongoni mwa viongozi wa vijiji anazo na kwamba imekuwa ikiendelea, huku viongozi hao wakiona aibu kusema.
“Sisi taarifa tunazipata, ila kuna baadhi wanaogopa kushtaki, sijui wanaona aibu?” anasema.
Hata hivyo, mmoja kati ya viongozi hao ambaye ni mwenyekiti wa Kijiji cha Nyamiswi, Leah Muhami anakiri kuwepo kwa unyanyasaji huo. “Wazee wa baraza hilo hivi karibuni walitaka kuniweka katikati wakitaka kuniadhibu, lakini nilionyesha msimamo wangu wakashindwa,” anasema Leah.
Anasema kuwa alikumbwa na mkasa huo baada ya kuwatetea baadhi ya wanakijiji waliotaka kudhulumiwa ardhi. “Hilo ndilo lilikuwa kosa langu, usipokuwa na msimamo watakusumbua sana,” anasema.
Ni tegemeo la Wanasiasa
Zipo pia taarifa za uhakika kwamba Dagashida limekuwa likitumika pia kisiasa kwa baadhi ya wanasiasa kama ngao yao kutimiza azma zao.
Ukweli wa taarifa hizo unathibitishwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima mkoani humo, David Nyalamu anayesema: “Dagashida ndiyo kikao cha mwisho katika harakati za kampeni za uchaguzi kwa viongozi wa kisiasa mkoani Simiyu.”
Nyalamu anasema kuwa kabla ya kupiga kura katika hatua za mwisho kwenye uchaguzi, wazee wa baraza hilo ndiyo hufahamishana nani anayetakiwa kuwa kiongozi.
“Watakayemjadili kwenye vikao vyao, ujue tayari ameshafanikiwa kuwa kiongozi, hatua hizo hufanyika kwa mbunge, diwani au mwenyekiti wa kijiji,” anasema Nyilamu.
Anaongeza kuwa ushindi hupatikana kutokana na ushawishi uliopo kwa baraza hilo, ukalinganisha na elimu ndogo kwa wanakijiji.
“Nikwambie, huku ni Watanzania wachache wanaojua kusoma na kuandika kwa hiyo watakaa kila sehemu kuwapigia kura wanakijiji kwa kiongozi wanayemtaka,” anasema.

Hata hivyo Katibu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), wilayani Itilima, Jumaa Iadhi amekana tuhuma hizo akisema hazina ukweli wowote.
“Dagashida ni sehemu ya wanakijiji, kwa hivyo sisi tunafanya kampeni zetu kwa kuwajumuisha wanakijiji wote, wala hatutumii ushawishi wa kundi hilo bali sisi ndiyo tunatengeneza ushawishi kwa wote,”anasema Iadhi.
Changamoto kwa polisi
Moja kati ya changamoto kubwa na ya muda mrefu kwa Jeshi la Polisi mkoani Simiyu ni hofu ya kuendelea kusambaa kwa mauaji na hukumu hizo.
Baadhi ya askari Polisi mkoani humo wamezungumza kwa nyakati tofauti juu ya changamoto inayoendelea kujitokeza kupitia baraza hilo.
Mmoja kati ya askari hao aliyeomba jina lake lihifadhiwe, anasema kuwa vijana wa baraza hilo wakishatekeleza hukumu yao kwa raia hukimbilia msituni na kujificha mfano wa Kundi la Al- Shabaab wakiwindana na polisi.
Anaongeza kuwa changamoto nyingine iliyopo ni viongozi wa Serikali za Mitaa na viongozi wa kisiasa kutotoa ushirikiano.
“Hakuna mwanasiasa, awe diwani au mwenyekiti wa kijiji anayeingia bila kushirikisha baraza hilo. Kwa hivyo wanapokuwa madarakani wanakosa ujasiri wa kuwakemea kwa maovu wanayoyafanya,” anasema askari huyo.
Akichangia hoja hiyo, askari mwingine katika kundi hilo anasema kuwa kwa sasa kuna baadhi ya wanakijiji wameshaanza kutoa taarifa za matukio ya mauaji yanapofanyika.
“Tukimkamta mmoja wa vijana wa baraza hilo changamoto nyingine inajitokeza kwenye ushahidi mahakamani. Hakuna mwanakijiji atakayekubali kusimama mahakamani kutoa ushahidi, kwa hofu ya kuuawa. Inabidi mtuhumiwa aachiwe huru kwa kukosa ushahidi,” anasema askari huyo.
Mapambano ya Jeshi la Polisi
Kamishna Msaidizi wa Polisi na Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Simiyu, Salum Msangi anakiri kuwepo kwa baraza hilo akisema kwa sasa baraza hilo linaongozwa na kundi la vijana matapeli wa kimila.

“Zamani lilikuwa ni baraza linalosaidia ukuaji wa ustawi wa jamii na kuchochea maendeleo. Walidhibiti migogoro, walihamasishana kwenye misiba na majanga, kujenga huduma za kijamii na walizuia uhalifu, lakini kwa sasa ni kundi la wahuni,” anasema Kamanda Msangi.
Katika harakati za kupambana na baraza hilo, Kamanda Msangi anasema kuwa baada ya kuhamishiwa mkoani humo, walianzisha operesheni maalumu katika wilaya na vijiji vyote kupiga marufuku Dagashida.
“Lakini pia tulianza kutoa elimu kwa kila kijiji, hali ilikuwa ni mbaya sana ya ukatili wa baraza hilo, mfano Kijiji cha Longolambogo,”anasema Msangi.
Kamanda Msangi anafafanua kuwa takwimu alizonazo zinaonyesha kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, wanakijiji watano walikuwa wakiuawa na baraza hilo kila siku mkoani humo kwa tuhuma mbalimbali ikiwamo visasi.
“Nilipoingia Simiyu hali ilikuwa mbaya sana. Tulipokea ripoti za matukio kama hayo, hata ya watu watano kuuawa kwa siku. Kuona hivyo kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa tulizunguka Mkoa wa Simiyu wote kupiga marufuku uwepo wa baraza hilo…,”anaeleza Kamanda Msangi.
Maelezo hayo ya Kamanda Msangi yanamaanisha kuwa katika kila siku saba za wiki watu 35 waliuawa mkoani Simiyu na katika mwezi mmoja wastani wa watu 150 waliuawa katika matukio yaliyohusisha kikundi cha Dagashida.
Anaongeza: “Kwa sasa tumekuwa tukipokea taarifa za matukio kama hayo baada ya mwezi mmoja.”
Anataja wilaya inayoendelea kuathirika na unyama huo kuwa ni Itilima, lakini anasema kwamba Jeshi la Polisi limeamua kupambana kuhakikisha Dagashida linakomesha ukatili wake..
Hata hivyo, anakiri kuwepo kwa changamoto ya kukosa ushirikiano kutoka kwa wananchi wakihofia usalama wao.
Itaendelea wiki ijayo


MWANANCHI

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments: