Mkuu wa Kitengo Cha Moyo toka Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Robert
Mvungi akiwaonesha waandishi wa habari mtambo wa Cath Lab unaosaidia
kuangalia mishipa ya damu inayokwenda kwenye moyo. (picha zote: Eliphace
Marwa)
Mkuu wa Kitengo Cha Moyo toka Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Robert
Mvungi akiwaonesha waandishi wa habari (hawapo pichani) mchoro
unaoonesha matundu katika moyo
Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Agnes
Kuhenga (kushoto) akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari (hawapo
pichani) juu ya gharama za matibabu katika kitengo cha magonjwa ya moyo
katika hospitali ya Taifa Muhimbili, katikati ni Mkuu wa Kitengo hicho
Dkt. Robert Mvungi na wa mwisho kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa
Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Marina Njelekela.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Marina
Njelekela akiwaonesha waandishi wa habari moja ya chumba cha kupumzika
wagonjwa mara baada ya kufanyiwa upasuaji wa moyo.
Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili ina uwezo wa kufanya tiba zote za upasuaji wa magonjwa ya moyo
na hakuna tena haja kwa Serikali kupeleka wagonjwa wote wa maradhi hayo
India, imeelezwa.
Kutokana na uwezo huo, uongozi wa hospitali
hiyo umeiomba Serikali fedha inazotumia kutibu mgonjwa mmoja nje ya nchi
dola 10,000 za Marekani, ili kupeleka wagonjwa hao hospitalini hapo
iwatibu kwa dola 6,000.
Akizungumza hospitalini hapo jana na
waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk Marina
Njelekela, alisema wametoa ombi hilo kwa maelezo kuwa iwapo Serikali
itatumia kituo cha moyo cha Muhimbili, fedha inazotumia kutibu wagonjwa
wa moyo nje ya nchi zitaiwezesha kuimarika zaidi.
Muhimbili imepata
uwezo huo baada ya baadhi ya madaktari wake kupata mafunzo India na
Israeli na tangu huduma hizo zianze mwaka 2008 wagonjwa 453 wenye
maradhi ya moyo wamefanyiwa upasuaji.
"Upasuaji
wa moyo unaofanyika katika hospitali yetu ni sawa na upasuaji
unaofanywa katika vituo vikubwa vya upasuaji moyo duniani kote," alisema
jana Dk Njelekela.
Miongoni mwa huduma zinazotolewa na
hospitali hiyo katika kitengo hicho cha moyo ni upasuaji wa kuziba
matundu kwenye moyo, kubadilisha valvu ambazo zimebana na kushindwa
kuruhusu damu kupita kwenye moyo au kulegea na kufanya damu kuvuja
kwenda sehemu isiyohusika na kurudisha moyo katika hali yake ya kawaida
ya afya.
Njelekela pia alisema pamoja na kufanya upasuaji, huduma
nyingine ambazo zinafanywa na kituo hicho cha moyo ni kliniki za
magonjwa ya valvu, moyo kupanuka, mishipa kuziba, mapigo kushuka,
magonjwa ya moyo ya kuzaliwa kwa watoto na upasuaji moyo na mishipa ya
damu.
Takwimu za Serikali zinaonesha kuwa hadi Aprili, Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii ilipeleka wagonjwa 402 kupata matibabu nje ya nchi.
Kati yao, 189 walikuwa na matatizo ya moyo, 39 saratani, 34 figo na 140
magonjwa mengine. Wagonjwa hao ni ambao matibabu yao yalishindikana
nchini.
Dk Njelekela alisema kituo hicho kina vifaa vya kisasa na
vya hali ya juu na mahususi kumudu matibabu ya magonjwa makubwa ya
moyo.
"Tunaendelea kutafuta taasisi zenye uzoefu mkubwa wa
matibabu ya moyo ili kuanzisha ushirikiano utakaowezesha kupata
wataalamu wao kuja kushirikiana na wa nchini ili kutibu magonjwa
makubwa ya moyo kama njia ya kuongeza uwezo kitaaluma.
Alisema
Serikali imetoa fedha kununulia mtambo mkubwa wa kuchunguza mishipa na
shinikizo ndani ya moyo na maradhi makubwa ya moyo ya kuzaliwa.
"Huu
ndio mtambo ambao kwa kipindi kirefu umekuwa ukisababisha Serikali
kupeleka wagonjwa wengi wa moyo India," alisema Dk Njelekela na kuongeza
kuwa mtambo huo ambao umenunuliwa kwa Sh bilioni 3.6 ulifungwa hivi
karibuni na wataufanyia majaribio mwezi ujao.
Alisema ndio
unaosaidia kuangalia mishipa ya damu inayokwenda kwenye moyo na
kuangalia moyo unavyofanya kazi na pia kama mtu anatakiwa kufanyiwa
upasuaji.
Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa Hospitali hiyo,
Agnes Kuhenga alisema mgonjwa mwenye rufaa kutoka hospitali za mikoa
atatibiwa kwa Sh 10,000 kumwona daktari, Sh 20,000 akilazwa na
akifanyiwa upasuaji atalipa Sh 50,000.
Pia alisema kutokana na
sera ya msamaha, wagonjwa watachujwa kuhakikisha hakuna matumizi mabaya
ya sera hiyo. Alisema wataweka utaratibu wa kuomba Serikali kutoa fedha
zote kwa hospitali kwa wagonjwa watakaopewa huduma kwa njia ya msamaha.
Pia
Kuhenga alisema kuna wagonjwa wa kulipia (private) ambao ni wateja
wenye uwezo wa kulipia fedha taslimu au kupitia bima za afya ambazo zipo
sasa.
Mkuu wa Kituo hicho, Dk Robert Mvungi alisema kina uwezo
wa kulaza wagonjwa 88 kwa wakati mmoja vikiwamo vitanda vyenye hadhi ya
kulaza viongozi wakuu wa Serikali akiwamo Rais.
"Juzi alikuja
kutibiwa hapa Rais wa Comoro... tuna vitanda vyenye hadhi hiyo," alisema
Mvungi na baadaye waandishi wa habari walijionea vyumba vya upasuaji
vilivyo na hadhi na mitambo ya hali ya juu.
No comments:
Post a Comment