Mchali akionyesha mkono aliokatwa.Picha na Rehema matowo
Kuna
mikasa mbalimbali huwatokea watu katika suala zima la mapenzi, kiasi
cha kusababisha baadhi yao kutopenda tena kuingia kwenye jambo hilo
wakiliona kama ni kitu kisichofaa, ingawa ukweli unaweza kuwa sio huo.
“Sitaki
tena wanaume, ni watu wabaya, wameniumiza moyo wangu mno,” anasema Hawa
Francis, mkazi wa Ubungo, Dar es Salaam. Sababu kubwa ni kero ambazo
amewahi kuzipata katika suala zima la uhusiano. Vivyo hivyo wapo wanaume
hawataki kuoa, kwa maelezo kuwa kuna wanawake wamewahi kuwatesa.
Kama
wewe ni kati ya watu ambao umekata tamaa na suala la uhusiano, fahamu
kuwa si wewe pekee.Kuna kundi kubwa la watu wameshatendewa kiasi cha
kufanya wasiwe na raha tena.
Mkasa wa mwanamke kukatwa mkono
Ilikuwa
Agosti 7, mwaka huu, saa mbili usiku. Ilikuwa ni siku iliyobadili
historia ya maisha yake. Baada ya kuwa katika mapenzi na mwanaume huyo
kwa zaidi ya miaka 17, wakipendana na kuitana majina yote mazuri
unayoyajua yakiwamo kuambiwa ‘mpenzi wangu nakupenda, nikinywa maji
nakuona kwenye glasi’…leo mapenzi yamegeuka shubiri.
ENDELEA KUSOMA MKASA HUU KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Mwanamke
huyo, Mchali Kihiyo (35), mama wa watoto sita, aliyepoteza viungo vyake
kutokana na ukatili wa kijinsia uliofanywa na mwanaume ambaye wamekuwa
na uhusiano nae (jina limehifadhiwa).
“Uhusiano
wetu ulikuwa mzuri, hata hivyo kwa sasa naona mambo yamekuwa magumu
kwangu, leo hii mimi sina mkono wa kushoto na nimeondolewa sehemu ya
viungo vyangu vya upande mmoja,”anasema Mchali,akibubujikwa machozi
kutokana na ulemavu alioupata.
Chanzo cha ulemavu
Anasema
maisha yao ya uhusiano yalikuwa ya furaha kwa kipindi chote lakini
yamegeuka shubiri baada ya mwanamume wake huyo kuonyesha dalili ya
kutompenda kama awali, hali ambayo anaitafsiri kama labda alikuwa na
mwanamke mwingine.
Mchali,
anasema mikasa na mateso ilianza miaka mitatu iliyopita baada ya kuhisi
kwamba mwanamume wake huyo amezaa na mwanamke mwingine. Ubaya zaidi
ulimtokea baada ya mtoto wa huyo mwanamke mwingine, kutumbukia kwenye
kisima cha maji na kisha kupoteza maisha.
“Kifo
cha mtoto huyo, ndicho kilichozaa tatizo hili la ukatili dhidi yangu na
kunisababishia ulemavu, kwa kuwa huyo mwanaume wangu na huyo mwanamke
aliyezaa nae, walidai kwamba mimi ndiyo nilimtupia majini marehemu mtoto
wao ili afe,”anasema mama huyo.
Vitisho kabla ya ulemavu
Mchali,
anasema mara baada ya msiba wa mtoto kumalizika, mwanamume wake huyo
alihamia kwa mke mdogo lakini akawa anarejea nyumbani na kumtukana huku
akitishia kufanya lolote analofikiri linafaa.
Anasema
baada ya mateso na vitisho kuzidi aliamua kuondoka kwa mumewe huyo toka
mwezi Aprili mwaka huu na kuamua kurudi kwa wazazi wake huku akiwaacha
watoto wake kwenye nyumba waliyokuwa wakiishi.
Anasema
alilazimika kuwaacha watoto kutokana na agizo la mumewe, aliyekataa
asiwachukue, hivyo akaanza maisha mengine ya upweke bila watoto huku
akiendesha maisha yake kwa biashara ya kuuza samaki.
Anasema
mwanzoni mwa mwezi huu, aliugua malaria na kukaa nyumbani bila kwenda
kwenye biashara zake. Agosti saba mwaka huu, alipata nafuu na kuamua
kwenda kumsalimia kaka yake, anayeishi mbali kidogo na nyumbani kwao na
ndipo yakamkuta yaliyomkuta.
Anaeleza
kuwa alikaa kwa kaka yake hadi muda wa futari wakafuturu na kushangaa
simu yake ikiita, kuangalia ni namba ya mpenzi wake huyo. Alipoipokea,
aliulizwa aliko, yeye alimweleza yuko kwa kaka yake na kumtaka amfuate
mnadani akale nyama kitendo ambacho anasema alipingana nacho.
Anasema
baadaye aliamua kurudi nyumbani na kusindikizwa na wifi yake hadi
karibu na nyumba yao ikiwa ni saa mbili usiku.Walipoagana, ghafla
akashangaa kusikia sauti ya mumewe ikimuita, alipogeuka alimwona, kisha
akamuuliza alikotoka na kumwambia alikuwa kwa kaka yake.
Kipigo na ulemavu
Anasema
mara baada ya kumjibu mwanamume huyo alianza kumpiga na hatimaye
alianguka chini na mumewe akatoa panga na kuanza kumkatakata sehemu
mbalimbali za mwili wake.
Hakika
hujafa hujaumbika. Mchali amecharangwa kwa mapanga kuanzia chini ya
goti mguu wa kushoto hadi kwenye makalio, amekatwa sehemu zaidi ya saba
mwilini.
Ni kama alitaka kumkata shingo
Anasema
kwa namna anavyoona ni kama alidhamiria kumuua akisema kuwa mara nyingi
akiwa na huo upanga alikuwa analenga kumtenganisha shingo. Alichofanya
mama huyo ni kuweka mikono shingoni kuzuia panga, kitendo
kilichosababisha mkono wake wa kushoto kukatwa kabisa.
Hawezi kukaa
Mwandishi
wa makala haya baadaye alimwomba mwanamke huyo angalau akae chini,
kwani muda mwingi wa mahojiano alikuwa amelala, ndipo alipojibiwa kwamba
hawezi kukaa kwa vile kuna nyama kubwa kwenye makalio ambayo
imeshindikana kushonwa.
Mama
huyo anasema wakati mumewe akimcharanga mapanga, mama yake mzazi
aliendelea kupiga ngolo (yowe) kuomba msaada, kaka yake alikwenda lakini
akashindwa kutoa msaada kwa kuwa shemeji yake huyo alikuwa akimkimbiza
na panga.
Anasema
kelele za mama yake zilisaidia kuokoa maisha yake, kwa kuwa majirani
walijitokeza, hivyo mwanamume huyo akaanza kuwakimbiza akitaka kuwadhuru
kitendo ambacho mama huyo aliona ndiyo nafasi pekee kukimbilia ndani.
Matibabu
Mchali,
anasema baadaye ndugu zake, walitafuta usafiri na kufanikiwa kupata
matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC ambako alilazwa kwa siku nne
na kurejea nyumbani kutokana na ushauri wa daktari anayemhudumia.
Kwa
mujibu wa mama huyo, daktari anayemtibu alimtaka Mchali akubali
kutibiwa majeraha akiwa nyumbani ili kuepuka maambukizi ya magonjwa
nyemelezi pamoja na kuepuka gharama za matibabu.
“Sina
uwezo wa kukabiliana na gharama za matibabu kwa kuwa siwezi kutembea,
nalazimika kukodi gari na kwa wiki naoshwa mara tatu. Nisaidieni ndugu
zangu, ndoa yangu imenifikisha hapa,” anasema.
Mchali na hali ya ukatili mkoani Manyara
Kamanda
wa Polisi mkoa wa Manyara, Akili Mpwapwa anasema mtuhumiwa bado
hajakamatwa kwa vile hajulikani aliko, huku akiahidi kuendelea
kulifanyia kazi suala hilo.
Akielezea
zaidi ukatili mkoani Manyara, anasema upo, japo ni mdogo ikilinganishwa
na mikoa mingine. Anaamini kuwa bado changamoto ni kubwa kwa wanawake
ambao wengi wao wamekuwa wakinyanyasika.
Sababu
kubwa za kunyanyasika kwa wanawake ni mfumodume. Akasisitiza kuwa Jeshi
la Polisi mkoani humo linaendelea kuelimisha jamii madhara ya ukatili
na kusema jitihada hizo zinapaswa kuigwa na wananchi na asasi nyingine
kuhakikisha ukatili wa kijinsia unatokomezwa.
Msimamo wa wanaharakati
Mkurugenzi
wa asasi ya kiraia ya Kwieco, inayojihusisha na utoaji wa msaada wa
kisheria na haki za binadamu mkoani Kilimanjaro,Wakili Elizabeth Minde,
anasema hali ni mbaya hasa kwa wanandoa wa kike, kwani wengi ndani ya
ndoa hawana nguvu.
Taifa lilipofikia
Hali
ya ukatili dhidi ya wanawake nchini bado ni kubwa kutokana na takwimu
zinazoonyesha asilimia 39 ya wanawake wenye umri kati ya mika 15 hadi 49
wanafanyiwa vitendo vya ukatili.
Waziri anena
Naibu
waziri wa maendeleo ya jamii jinsia na watoto, Ummy Mwalimu alikiri
ukatili dhidi ya wanawake kuongezeka na kusema vitendo kama kupigwa na
kubakwa ni matukio yanayoongoza zaidi na yanafanywa na wanaume, huku
akisisitiza kuendelea kuangalia namna ya kufanya ili wanawake nchini
waendelee kufurahia maisha.
Safari ya ndoa
Kwa
mujibu wa Mwanasaikolojia, Modesta Kimonga anayefanya shughuli zake za
ushauri Mkoani Mbeya, ndoa inaweza kufananishwa na safari ndefu yenye
matukio yasiyotazamiwa, mengine yenye kupendeza na mengine yenye
kuumiza.
Anasema
mafanikio katika ndoa hayapimwi kwa panda shuka za safari bali
yanapimwa kwa jinsi wenza wanavyoshughulikia hali hizo Ndio kusema ni
suala la msingi kwa walio kwenye ndoa kujifunza namna ya kupambana na
changamoto zinapotokea, siyo kutesana au kukimbiana.
Ushauri zaidi
Mshauri
maarufu wa ndoa nchini Uingereza, Hussain Zahid anasema katika makala
ya kitabu chake cha ‘My marriage’ yaani ndoa yangu kuwa msingi wa kuwa
na ndoa nzuri ni kupata muda wa kuzungumza baina ya wanandoa wenyewe ili
kuondoa tofauti zao.
“Kila
mtu ajione analo deni la kumpenda na kumfanyia mema mwenza wake. Kila
mtu ajifunze kauli nzuri na matendo mazuri kwa mwenzi wake…kwamba kabla
ya kufanya lolote, tafakari, ungefurahi kufanyiwa hilo unalotaka
kulifanya,” anaonya.
Staili mpya ya maisha kwa baadhi ya wanawake
Tafiti
zinaonyesha kwamba kutokana na uwepo kwa mikwaruzo mingi katika
mapenzi, kuna wanawake hawataki tena kuolewa. Kama lengo ni kupata
mtoto au watoto, huwa tayari kuzaa na yeyote hata kama ni mume wa mtu,
kisha jukumu la kulea kwa asilimia kubwa hufanya wao au kwa kushirikiana
na hao waliozaa nao.
Hata
hivyo wataalamu mbalimbali wa masuala ya ndoa, wanashauri watu kuacha
tabia hiyo ya kuzaa tu, badala yake wapende kuzaa wakiwa kwenye ndoa kwa
sababu mtoto ambaye hana mzazi mmoja, huathiriwa sana na matatizo ya
kisaikolojia.
Mfano wa utafiti
Kulingana
na utafiti uliotolewa hivi karibuni na Ofisi ya Taifa ya Takwimu
Marekani, uko uwezekano mkubwa wa watoto wenye kulelewa na mzazi mmoja
kuwa na tabia mbaya zaidi ya watoto wenye wazazi wote.
“Kama
ni suala la kuiga tabia na matendo mabaya, watoto ambao wana mzazi
mmoja wanaharibika mara tano zaidi ya watoto ambao wana wazazi wote
wawili,” inasema sehemu ya utafiti huo.
Utafiti
unaongeza kuwa hata wanapofika kwenye umri wa ujana, vijana ambao wana
mzazi mmoja, wanaharibika zaidi ya wale ambao wana wazazi wote; Wana
uwezekano wa kuharibika mara tatu zaidi ya vijana ambao wanaishi na
wazazi wote wawili.
Si wote huharibika
Hata
hivyo utafiti unasisitiza kuwa si watoto wote wenye mzazi mmoja huwa na
tabia mbaya, bali kinachosemwa ni kwamba kwa asilimia kubwa watoto wa
aina hiyo huharibika zaidi ya wale ambao wanalelewa na wazazi wote
wawili. Wanaoathirika zaidi ni wale ambao wazazi wao wametalakiana, hasa
kwa sababu mara nyingi hata nguvu za kulea watoto hupungua kutokana na
wazazi au mzazi husika kuwa na msongo wa mawazo.
Matendo
mabaya kama vile ya mzazi mmoja kuteswa na mwingine au mtoto kuona mama
au baba yake akimshtaki mwenzi wake, huchangia kwa kiasi kikubwa
kuendelea kumuathiri mtoto kitabia.Tabia kama za kupigana au mateso
mengine kabla ya wanandoa kuachana, huchangia kuharibu maisha ya mtoto
kwa kuona labda kupigana ndio njia nzuri ya kupambana na mtu
anayekukwaza au mwingine kutishwa na uhusiano kwamba unaweza kusababisha
mateso.
Sababu ya migogoro na tiba yake
Mtafiti
maarufu wa masuala ya ndoa kutoka Urusi, Korotayev, A, katika chapisho
lake alilolipa jina “Division of Labor by Gender’ yaani mgawanyiko wa
majukumu katika jinsia, anasema msingi wa kuwa na uhusiano mbaya katika
ndoa nyingi ni kutokuwa na fursa ya kukaa pamoja na kukubali kuondoa
kasoro.
“Hakuna
mtu ambaye yuko safi kwa asilimia 100. Umekaa tumboni mwa mama yako na
kuna wakati mnagombana, iwe mtu ambaye mmekutana tu mitaani?”anahoji
Korotayev, huku akiwasisitiza watu walio kwenye ndoa kubuni mbinu za
kupendana na kufanya mikakati mingine ya maisha badala ya kuendekeza
ugomvi, kufikiria kuachana au kutafuta wapenzi wengine.
MWANANCHI




No comments:
Post a Comment