DK. MWAKYEMBE AILIPUA TRA

WAZIRI wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe ameishutumu Mamlaka ya Mapato (TRA), kuwa ni kikwazo katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya kuboresha Bandari ya Dar es Salaam ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN).

Amesema hali imewafanya watu wengi wanaoitumia bandari hiyo kulalamikia madudu yanayofanywa na TRA, hasa tatizo la kufeli kwa mfumo wa mawasiliano ya kompyuta unaotumiwa na mamlaka hiyo kutoza kodi mbalimbali.

Alitoa shutuma hizo baada ya kutakiwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ajibu baadhi ya maswali yaliyoulizwa na Watanzania wanaofanya biashara na wale wanaoishi katika Jiji la Guangzhou, Jimbo la Guangdong ambalo ni jiji kubwa la biashara lililoko kusini mwa China.

ENDELEA KUSOMA HABARI KWA KUBOFYA HAPA CHINII

Katika kikao hicho cha kuhitimisha ziara ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, nchini China ambapo alikuwa akizungumza na wafanyabiasha waishio katika jimbo hilo.

Mmoja ya Watanzania hao, Stanley Mwakipesile ambaye ni mfanyabiashara wa Kariakoo alisema utoaji wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam ni tatizo kubwa kutokana na mfumo wa kutoza kodi unaotumiwa na TRA kutofanya kazi siku nyingine na hivyo kusababisha mteja kutozwa fedha nyingi.

Alisema kutokana na kero hiyo, wafanyabiashara wengi kutoka nchi jirani wameikimbia bandari hiyo na sasa wanatumia Bandari ya Mombasa, jambo ambalo alisema ni hasara kwa nchi. 

“Inakuwaje kila siku pale TRA system inakuwa down? Kuna urasimu mwingi tu pale cha ajabu wakati wao ndio hawafanyi kazi, lakini mteja anatozwa eti kachelewesha kutoa mzigo,” alisema Mwakipesile.

Dk. Mwakyembe katika kujibu hoja za mfanyabiashara huyo, alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na akasema eneo linalolalamikiwa sana ni TRA kuwatoza wateja tozo za ziada hata kipindi ambacho watendaji wa mamlaka hiyo hawafanyi kazi kwa kisingizio cha mfumo kutofanya kazi.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kweli TRA ni tatizo, hasa hili la system down kwa kweli ni kero na linawaumiza watu wengi wanaotumia bandari yetu. Ni lazima tukae tuone namna ya kutatua tatizo hili,” alisema Mwakyembe.

Alisema licha ya kuwepo agizo kutoka serikalini la kutaka TPA na TRA wafanye kazi saa 24, lakini watendaji wa TRA wanafanya kazi kwa saa 12 tu na wanalala kwa siku 10 katika mwezi mzima.

Alisema wakati TRA wanaenda kulala, mteja ahudumiwi na wanapokuja kuendelea na kazi kesho yake, wanawatoza wateja tozo ya kuchelewesha mzigo wakati makosa siyo ya wateja bali ni ya watendaji wa mamlaka hiyo ya kukusanya kodi kwa Tanzania.


RAI

No comments

Powered by Blogger.