Dar es Salaam. Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu amewataka viongozi wa chama hicho kutafakari na kudhibiti madhara yanayoweza kukikumba hasa baada ya hatua yake ya hivi karibuni ya kumvua nyadhifa zote, Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe na wenzake wawili.
“Bahati nzuri wamevuliwa uongozi siyo uanachama, binafsi nadhani viongozi wanatakiwa kutafakari na kudhibiti madhara zaidi kwa chama, wakishupaza shingo, lolote litakalotokea watakuwa ni sehemu ya lawama,” Profesa Baregu alisema Dar es Salaam jana.
Zitto, aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani Arusha, Samson Mwigamba walivuliwa uongozi Novemba 22 mwaka huu, kwa tuhuma za kuandaa waraka wa Mkakati wa Mabadiliko 2013, uliolenga kufanya mabadiliko makubwa ya kiuongozi wakati wa uchaguzi mkuu wa ndani wa chama hicho kinyume na katiba, sheria na itifaki za chama.
Profesa Baregu alisema pamoja na viongozi hao kuvuliwa madaraka, mema waliyokifanyia chama hicho hayawezi kuyeyuka na kwamba makosa yao yasikuzwe kiasi cha kufuta mazuri yao katika kujenga chama hicho.
“Ni vigumu kuamini kwamba makosa ya Zitto, Dk Kitila na Samson Mwigamba yanaweza kuyeyusha mema waliyokifanyia chama kama barafu inavyoyeyuka juani.”
Profesa Baregu ambaye alikuwapo katika kikao kilichowavua uongozi Zitto na wenzake alisema kinachotakiwa kufanyika sasa ni kujenga uhusiano ndani ya chama na hasa kipindi hiki cha mpito kuelekea uchaguzi mkuu wa ndani ambao umeanza Novemba 22 na unatarajiwa kumalizika Juni mwakani.
Alitaka hatua dhidi yao zizingatie Katiba ya chama hicho ili kuhakikisha kuwa hazivurugwi na mamlaka nyingine zilizopo ndani ya Chadema akisema mkutano wa Baraza Kuu unaweza kubadili uamuzi wa Kamati Kuu.
“Kinachotakiwa kufanywa ni kuwatangazia wanachama misingi, taratibu na kanuni za kuzingatia katika harakati zao ili kuondoa hali ya watu kufanya mambo kwa kificho,” alisema na kuongeza:
“Ni wazi wengi wapo katika kampeni, ichukuliwe kuwa walioshughulikiwa wamebambwa na iwe njia ya kuonyesha ukomavu katika kustahamiliana.”
Alisema asingependa kuona siasa za kulipizana visasi na kusisitiza kwamba hata kama mwanachama ana chuki binafsi na mwenzake, hatakiwi kutumia chuki hiyo kumhukumu.
“Tuhuma zinazotolewa dhidi ya Zitto na wenzake kwamba wamenunuliwa na chama fulani cha siasa zinahitaji maelezo na vielelezo vya kina ili kuwaaminisha wengi. Nasema hivi kwa sababu historia yao inadhihirisha kuwa wana uchungu na chama chao. Chama kinachoongozwa kwa demokrasia na kinachotarajiwa kushika madaraka ya kuongoza nchi, lazima kionyeshe uwezo mkubwa wa kuvumiliana, kutafakari, kusamehe, kuaminiana na kujenga umoja wenye lengo la kuelekea kusudio lake.”
Lwakatare
Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare alisema chama hicho kipo imara na hakiwezi kuyumba kwa sababu ya uamuzi huo.
Lwakatale ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho alisema: “Mfumo wa ulinzi ndani ya chama upo imara, yakitolewa maelezo na ngazi za juu kinachofuata baada ya hapo ni utekelezaji.”
Alisema kilichotokea ni kitu cha kawaida na ni mwanzo wa chama kujiimarisha.
Temeke wapinga
Baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu na Baraza Kuu la Chadema hicho Wilaya ya Temeke wamepinga hatua iliyochukuliwa na Kamati Kuu ya kuwavua nyadhifa viongozi hao.
Mwenyekiti wa Vijana Mkoa wa Temeke, ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu na Mkutano Mkuu, Joseph Patrick aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa mgogoro huo haulengi kujenga chama, bali unakibomoa.
“Chama chetu kimekuwa na tabia ya kuingia kwenye migogoro kila panapokaribia uchaguzi wa ndani. Hii inasababisha kuchafuana na kutukanana miongoni mwetu kiasi cha kuitana wahaini, wasaliti na wengine kuwaita wenzao wanatumika kwa lengo la kuwadhoofisha mbele ya wanachama,” alisema na kuongheza:
“Tumeona mifano mingi ya namna hii. Wakati Chacha Wangwe akiwa hai alipotangaza kuwania uenyekiti, mgogoro wa namna hii ulijitokeza, aliitwa majina yote na hakuwahi kusemwa vizuri kwenye chama, hakuchafuliwa na watu walio nje ya chama, bali viongozi wenzake waliotofautiana kimsimamo.”
Alisema hali hiyo ilijitokeza pia kwa Zitto alipotangaza kuwania uenyekiti kama ilivyokuwa wakati wa chaguzi za viti maalumu na mabaraza ya chama.
Alisema ni vyema viongozi wakaitisha mkutano mkuu wa dharura na kuwaeleza wanachama mambo mbalimbali ikiwamo ni kwa nini wameamua kusambaza waraka ambao alisema unakidhalilisha chama badala ya waliouandika.
Katibu Chadema ahojiwa
Katibu wa Chadema Mkoa wa Dar es Salaam, Herry Kilewo amehojiwa na Polisi kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kutokana na madai ya Zitto kutishiwa kuuawa.
Katika mahojiano hayo, Kilewo aliongozwa na Mwanasheria wake, Mussa Mfinanga, Mwanasheria wa Chadema John Malya na pia alikuwapo Diwani wa Ubungo, Boniface Jacob. Mfinanga alisema Novemba 11 mwaka huu, chombo kimoja cha habari kiliripoti kuwa Zitto ametishiwa kuuawa na mteja wake Kilewo.
Mfinanga alisema baada ya madai hayo, Jeshi hilo lilimwita Zitto kutoa maelezo yake na kisha kuona haja ya kumhoji Kilewo shutuma hizo. Alisema mteja wake amejidhanini mwenyewe na yupo nje kwa dhamana bila ya masharti yeyote.
Msemaji wa Polisi, Advera Senso alikiri kuhojiwa kwa Kilewo akisema ni kawaida kwa jeshi hilo kumuita mtu na kumhoji kwa mujibu wa taratibu na sheria zake.
Imeandikwa na Fidelis Butahe, Beatrice Moses, Pamela Chilongola na Editha Majura.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment